Mbrazil Simba kuleta mashine mbili

Muktasari:

  • Habari kutoka ndani ya Simba zinasema awali kocha huyo alitakiwa aje mapema jana aondoke na msafara wa timu, lakini kuna mambo yamembana na kutarajiwa kuingia muda wowote kuanzia leo kisha kutambulishwa rasmi kama kocha mkuu akiziba nafasi ya Zoran Maki.

Jana Simba ilivuka Bahari ya Hindi kwenda Zanzibar kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023, huku mabosi wa klabu hiyo wakijipanga kuwafanyia sapraizi mashabiki kwa kumtambulisha kocha mkuu mpya, Robertinho Oliviera.

Awali ilitarajiwa kocha huyo kutoka Vipers ya Uganda angewahi msafara huo, lakini mambo yamekwama na sasa anatarajiwa kutambulishwa jijini Dar es Salaam ndani ya wiki hii kabla ya kuanza majukumu ya kuinoa timu hiyo inayojiandaa na mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mwanaspoti limejiridhisha, kocha huyo, atatambulishwa kama kocha mpya wa Simba muda wowote ndani ya wiki hii wakati huo kikosi kikiwa kinaendelea na Mapinduzi, huku akitua sambamba na nyota wawili wapya ambao klabu imeanza kufanya mipango ya kuwasajili.

Mashine ya kwanza itakayotua na kuanza kasi chini ya Robertinho ni beki wa kushoto mzawa na mwingine ni straika Kwame Opuku anayepewa nafasi kubwa japo kuna mgawanyiko kwa baadhi ya viongozi, kwani pia kuna jina la Mcameroon.

“Wiki hii kuna sapraizi kwa mashabiki, ngoja muda ufike ndo mtajua, achana na ishu ya kocha kuna mashine nyingine mbili zitakazokuja sambamba na ujio wa Mbrazili huyo,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba.

Chanzo hicho kilisema kikosi cha Simba kama ikiwa bado inaendelea na mashindano hayo huenda Robertinho akaifuata timu hiyo kwenye mashindano hayo wakati huo ikiwa inanolewa na makocha, Juma Mgunda na Mussa Hassan Mgosi.

Mgosi atakwenda kwenye mashindano hayo kama kocha msaidizi, kwa vile Seleman Matola inaelezwa hataenda kwa sababu ya majukumu yake mapya na ishu zake za masomo.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema awali kocha huyo alitakiwa aje mapema jana aondoke na msafara wa timu, lakini kuna mambo yamembana na kutarajiwa kuingia muda wowote kuanzia leo kisha kutambulishwa rasmi kama kocha mkuu akiziba nafasi ya Zoran Maki.

“Kuna mambo yamemkwamisha tofauti na tulivyopanga awali, lakini kila kitu kipo sawa na huenda akatambulishwa Dar kabla ya kwenda Zanzibar kushuhudia timu kwenye Mapinduzi,” kilisema chanzo chetu makini kutoka ndani ya Simba.

Aidha inaelezwa bilionea wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ amewaeleza viongozi wengine kama timu yao itatolewa mapema kwenye mashindano hayo watafute nchi ya karibu kama Afrika Kusini au mkoa wa karibu kama Morogoro kwa ajili ya kuweka kambi, ili Robertinho apate nafasi ya kufanya mazoezi na wachezaji.

Simba imepangwa Kundi C la Kombe la Mapinduzi 2023 ikiwa na KVZ na Mlandege, wakati kwenye Ligi ya Mabingwa pia ipo Kundi C na AC Horoya, Vipers na Raja Casabalanca.