Mbrazili Simba akomalia matano

Muktasari:

  • Robertinho alisema kila mchezaji anatakiwa kubadilisha akili yake na kuiweka kwenye wivu wa mafanikio kwani yale malengo ya kufanya vizuri kila mchezo yanatakiwa kuwa jambo la kwanza kuliko kitu kingine chochote.

KOCHA wa Simba, Oliveira Robertinho amesema kuna mambo matano ndani ya kikosi hicho anapambana kuyabadilisha na tangu ameanza kazi ndani ya muda mfupi kuna mengine ameanza kuyafanyia kazi.

Robertinho alisema jambo la kwanza amefanya mabadiliko ya kimfumo kutokea 4-2-3-1, aliyokuta timu inatumia mara ya mwisho na chini yake anapenda kutumia mifumo miwili 4-2-4 au 4-1-3-2.
Alisema si rahisi wachezaji kushika kwa uharaka mifumo hiyo miwili kutokana ni mipya kwao ila katika michezo minne kikosi kikiwa chini yake kwa kiasi kikubwa wachezaji wamejitahidi kufanya vile ambavyo anahitaji.

"Nikipata muda wa kutosha kukaa na timu, kufanya nayo mazoezi mengi tofauti tofauti kama ilivyokuwa kule Dubai naimani kutakuwa na mabadiliko makubwa na kila mchezaji atafanya vile ambavyo nahitaji kwenye mifumo hiyo miwili mipya," alisema Robertinho na kuongeza;

"Jambo la pili nahitaji kila mchezaji muda mwingi anapokuwa uwanjani anakimbia tunapokuwa na mpira ili kutengeneza shambulizi la haraka na kama tukiupoteza tutafute kwa haraka urudi kwenye himaya yetu,"

"Nimewaeleza wachezaji wangu kwenye mazoezi jambo la tatu kila ambaye atakuwa anajituma kulingana na majukumu yake yalivyo atapata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kwenda kuisaidia timu.

"Nimewambia hivyo kwani nataka kuona kila mchezaji anashindana vya kutosha akiwa katika uwanja wa mazoezi ili akipata nafasi kwenye mechi apambane vya kutosha ili kuisaidia timu kufanya vizuri.

"Hayo yote siyo rahisi ndani ya muda mfupi kuona yanabadilika kwa haraka na kila mchezaji kufanya vile nahitaji ambavyo nahitaji kuona kutoka kwake kulingana na majukumu ya nafasi anayocheza."

Katika hatua nyingine Robertinho alisema jambo la nne anapenda kuona kila mechi Simba inacheza vizuri soka la kuvutia na kumiliki mpira na mwisho wa mchezo inapata ushindi kama malengo yao yalivyo.

Robertinho alisema kila mchezaji anatakiwa kubadilisha akili yake na kuiweka kwenye wivu wa mafanikio kwani yale malengo ya kufanya vizuri kila mchezo yanatakiwa kuwa jambo la kwanza kuliko kitu kingine chochote.

"Simba nimekutana na wachezaji wenye vipaji na uelewa mkubwa naamini hayo mabadiliko yote yataanza kuwa na faida kwenye kikosi kwa kucheza soka la kuvutia, kushambulia kwa kasi muda wote kama falsafa zangu zilivyo," alisema Robertinho.