Robertinho: Nileteeni huyu

SIMBA imeendelea kujifua kishua huko Dubai chini ya kocha mpya Mbrazili, Roberto Oliveira 'Robertinho' lakini kubwa zaidi mtaalamu huyo wa mbinu amewaambia mabosi wa timu hiyo anataka mshambuliaji wa kati mwingine haraka iwezekanavyo huku akitaja sifa anazotaka.
Robertinho baada ya kukaa na timu kwa siku zisizopungua nne, amekiangalia kikosi chake kwenye kila eneo na kuona kuna uhitaji wa kusajili straika wa maana ambaye atasaidiana na John Bocco na Habib Kyombo lakini akitaka mwenye sifa za ziada kuliko wawili hao.
Msimu huu, Simba ilianza kwa kusuasua eneo la ushambuliaji kutokana na kutokuwa na muendelezo wa ubora kwa Bocco na Kyombo ndipo kaimu kocha mkuu wa muda huo, Juma Mgunda akaamua kuwa anamtumia Moses Phiri kama mshambuliaji wa mwisho licha ya kwamba siyo nafasi yake halisi lakini akaonekana kuimudu na kufunga mabao 10 kwenye ligi kabla ya kupa majeraha ya kifundo cha mguu 'enka'.
Kocha huyo aliyeichukua Simba mwanzoni mwa mwezi huu akitokea Vipers ya Uganda amesema sifa ya kwanza anataka mshambuliaji ambaye yuko fiti zaidi siyo wa kuja kupewa muda, pili anamtaka mwenye nguvu na mwenye uwezo wa kuwapita mabeki na tatu awe anaweza kufunga katika kila nafasi anazopata.
"Nimeitazama timu, ina wachezaji wazuri ambao kila mmoja akitimiza wajibu wake tunaweza kufikia malengo, ni maeneo machache yanahitaji maboresho lakini kwa sasa nahitaji zaidi mshambuliaji mwenye nguvu, kasi pia awe na muendelezo mzuri wa kufunga atakayesaidiana na waliopo.
"Lazima awe yule ambaye anaweza kuingia kwenye kikosi moja kwa moja, akipata nafasi anafunga na kulingana na wale waliopo anatakiwa mtu mwenye nguvu na kasi," alisema Robertinho.
Taarifa za kuaminika kutoka Simba zinaeleza tayari kocha huyo amepewa nafasi ya kuchagua mshambuliaji anayemtaka huku viongozi nao wakiendelea na mazungumzo na Mkongomani Jean Baleke wakimtaka kwa mkopo kutokea TP Mazembe.
Inaelezwa kuna ambao kocha huyo alipendekeza awali lakini kutokana na muda Simba wakamwambia ni ngumu kwa sasa kuwapata na sasa wanapambana kwa siku chache zilizobaki kuhakikisha wanapata jembe jipya.
Huenda ndani ya siku mbili kuanzia sasa Simba ikamtambulisha mshambuliaji wake mpya na akawa ndiye mchezaji wa mwisho wa kigeni kusajiliwa kwenye dirisha dogo hili baada ya Mrundi Said Ntibanzokiza 'Saido' iliyomshusha kutokea Geita Gold.
Ikumbukwe Dirisha Dogo la usajili litafungwa Jumapili ya Januari 15, 2023 itakapofika saa 00:00 usiku.