Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mdamu soka ndiyo basi 

Muktasari:

  • Tangu apate ajali hiyo, mchezaji huo alifanyiwa upasuaji na kuendelea kujiuguza kabla ya hivi karibuni Mwananchi kumtembelea nyumbani kwake kumjulia hali na kubainika bado anaishi katika hali ya mateso na maumivu kutokana na majeraha aliyoyapata ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kumsaidia.

Dar es Salaam. Pamoja na watu wengi kuendelea kujitolewa kumsaidia Gerald Mathias Mdamu aliyewahi kutamba katika soka kupitia timu kadhaa ikiwamo Polisi Tanzania, imeelezwa sasa anaweza kupona lakini atakuwa mtazamaji tu wa mchezo huo.

Hii ni kutokana na taarifa aliyofahamishwa na daktari aliyemfanyia upasuaji wa kwanza baada ya ajali ya gari ya Julai, 2021.

Nyota huyo wa zamani wa Mwadui, amefahamishwa wazi kwamba kwa sasa hataweza tena kucheza soka, kitu ambacho amekipokea kwa uchungu na kukubali hali halisi.

Mdamu alipata ajali hiyo wakati basi la timu aliyokuwa akiitumikia wakati huo, Polisi Tanzania lilipoacha njia na kugonga mti na kusababisha kuvunjika miguu, wakati wakitoka mazoezi mjini Moshi kujiandaa na mechi mbili za kufungia msimu wa 2020-2021.

Tangu apate ajali hiyo, mchezaji huo alifanyiwa upasuaji na kuendelea kujiuguza kabla ya hivi karibuni Mwananchi kumtembelea nyumbani kwake kumjulia hali na kubainika bado anaishi katika hali ya mateso na maumivu kutokana na majeraha aliyoyapata ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kumsaidia.

Mmoja ya wadau walioshtushwa na hali ya Mdamu alikuwa ni daktari aliyemfanyia upasuaji kutoka Moi, Dk Kennedy Nchimbi ambaye aliomba mchezaji huyo aende hospitalini hapo ili kumfanyia uchunguzi kabla ya kumweleza ukweli kwamba hataweza tena kucheza soka.

Hata hivyo, mchezaji huyo ameikubali hali ya kuishi plani nyingine baada ya kushauriwa na daktari ya nini kifanyike, ili maisha yake mengine yaendelee, huku akijulishwa pia anatakiwa kufanyiwa upasuaji mwingine ili kurekebisha tatizo lake la kutokwa na usaha katika majeraha aliyonayo.

Mwananchi linaendelea kukuletea muendelezo wa taarifa za Mdamu, ili kujua hali yake itakavyokuwa inaendelea, huku baadhi ya wadau wakijitolea kwa namna wanavyojaaliwa, ili kuona anakuwa sawa.


Majibu ya daktari

Daktari bingwa wa magonjwa ya mifupa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), Kennedy Nchimbi, amesema Mdamu, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia.

Mwananchi lilifunga safari hadi hospitali ya Muhimbili chumba 119 na kuonana na daktari huyo ili kufafanua kitaalamu nini cha kufanya ili staa huyo aweze kukaa sawa.

Daktari huyo alisema; "Wakati tunamfanyia upasuaji wa kumtibu mguu wake wa kushoto, lengo la kwanza ilikuwa ni kuhakikisha anabakia na mguu wake, hilo lilifanikiwa na ndio furaha yetu, lakini amepata kovu kubwa, kiwiko cha chini cha mguu wa kushoto au enka jointi imegandamana engo ambayo sio sahihi, ndio maana akitembea anashindwa kukanyagia kisigino, maana mfupa wake ulivunjika kwa kiasi kikubwa sana."

"Nini kifanyike inabidi atengenezewe kiatu cha mguu wa kushoto, ambacho kitakuwa kinaakisi jinsi mguu ulivyopinda ambacho kitafidia gepu la juu, atakuwa na uwezo wa kutembea kukanyaga moja kwa moja.

"Sehemu ya paja la mguu wa kushoto, panapotoa maji na kukauka ni dalili aidha ya jipu la kwenye mfupa au ni infeksheni iliyopo juu, akifanyiwa vipimo na upasuaji inarekebishika na itaisha.

"Gharama za upasuaji kwa hospitali za  ni Shilingi 600,000 (laki sita), ukiachanganya na gharama za dawa, kiatu, X ray inaweza ikafika Sh.1.5 milioni, hivyo namshauri asiende hospitali binafsi zina gharama kubwa ambazo atashindwa kuzimudu." anasema Dk Nchimbi.


Baada ya matibabu

Dokta Nchimbi alisema, Mdamu hataweza kurejea tena uwanjani, huo ni mwisho wake wa kucheza soka, isipokuwa anaweza akasomea ukocha.

"Spoti zingine anaweza akafanya, ila mpira haitawezekana tena, ila kwa kuwa kipaji chake ni soka anaweza akakiendeleza kwa kufundisha wengine (kocha)," anasema Dk Nchimbi na kuongeza;

"Ni afadhali mtu kupata matibabu kwa mtu sahihi, wakati sahihi, tusianze mambo ya kienyeji, matibabu ya majeraha ya michezo wenzetu nje wanaita Sports Injury, hii ni matibabu ya kibingwa bobezi sio kila mtu anaweza akafanya na sisemi hivyo kuipa sifa taasisi yetu, nasema hivyo kwa kuwa wapo madaktari bingwa wabobezi wanaoweza wakatibu, hizo hospitali zote mnazoziona mjini wanategemea madaktari wa hapa hapa."


Mapokeo ya Mdamu 

Baada ya daktari kumwambia anachotakiwa kukifanya, Mdamu alipata matumaini ya kurejea kwa afya yake na kukubaliana na mapungufu yaliyomfika kama ulemavu wa kuishi nao.

"Kinywa changu sasa kiseme nimekubali sitacheza tena soka, ila nitaendeleza karia yangu kwa njia ya ukocha, nimefarijika kuona kuna njia ya kupona usaha unaonitoka, nirudi tena kwa Watanzania nawaomba wanasaidie kunichangia pesa ya kutibiwa, ili nikafanye upasuaji tena.

"Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania , Kidao Wilfred, alinipigia niende TFF, nikazungumze nao  ili zikitokea kozi za ukocha watanipa nafasi ya kujifunza bure.

"Ni neema ya Mungu, sikutegemea kuwa hai, namshukuru sana daktari Nchimbi kunipokea kwa mara nyingine na kujitoa muda wake bure ili mradi nipone, sina chakumlipa, maana amenipa matumaini mapya."


Mke wa Mdamu

Mke wa Mdamu aliyejitambulisha kwa jina la Juliana ambaye amebahatika kupata naye watoto wawili ambao Bryton (9) anasoma darasani la tatu, Yully (4) anasoma chekechea, anasema anatamani mumewe apone ili aishi kwa amani.

Anasimulia changamoto, alizopitia tangu mume wake alipopata ajali mwaka 2021 hadi 2024 ni pindi anapoona huzuni inayotawala sura yake na maneno anayoambiwa kwamba anatamani kupona na kusimamia majukumu yake kama baba wa familia.

"Kwanza wakati anapata ajali nilikuwa na mtoto wa miezi sita ambaye ni Yully, hivyo nilikuwa namuacha kila siku kwa majirani, nikiwa nakwenda hospitali, alipofikisha miezi nane nikamwachisha kunyonya.

"Kati ya maneno machungu ambayo alikuwa yananichoma moyo kutoka kwa Mdamu, nikienda kumuona hospitali, alikuwa anasema kuna siku utakuta nimejikaba na shuka nife, nikawa namnunia, halafu natoka nje nalia, kisha narudi kumwambia tunakuhitaji sana na watoto wako, akisikia watoto alikuwa anarudi nyuma.

Anatamani mume wake atibiwe tatizo la usaha unaomtoka katika paja ya mguu wa kushoto, ambao haujawahi kukauka tangu alipopata ajali.

"Nafanya kazi ya kumkamua na kumsafisha, akiwa anaenda kukaa na wenzake najitahidi kumuweka sawa ili angalau nguo isichafuke na asiwe anajisikia vibaya, lakini lazima utatoka kuna alama zinaonekana za uchafu katika nguo zake," anasema mkewe na kuongeza;

"Nikiwa naamka asubuhi kwenda kuuza chakula sehemu ninakofanya kazi, ana kauli moja hivi anasema yaani wewe unakwenda kutafuta mimi nalala kitandani, inaniumiza sana, natamani niitunze familia yangu, huwa namwambia jambo la msingi kwetu ni kumuona anapona na linarudi tabasamu lake la kwanza."


Wadau wamwaga noti

Wadau mbalimbali wamekuwa wakiendelea kumsaidia Mdamu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nalo limeibuka kumuokoa jahazi la matibabu ya mchezaji huyo.

Mara baada ya habari za Mdamu kuwa anaendelea kuteseka na kuhitaji msaada, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kumpiga tafu, ikiwamo Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji kabla ya TFF nayo kujitosa baada ya Rais Wallace Karia kuiagiza familia ya mchezaji huyo wa zamani wa Mwadui na Polisi Tanzania kumpeleka Mdamu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo gharama za matibabu hayo zitalipwa na shirikisho hilo.

"Hongereni kwa kazi nzuri, mnayofanya, hatukuwa tunafahamu kwamba bado anauhitaji wa matibabu, lakini naomba apelekwe Muhimbili, na gharama za matibabu yake iletwe invoice TFF tutalipa," imesema taarifa ya Karia akizungumza na Mwananchi.


Kigogo wa Yanga

Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji ambaye pia ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) amemchangia Mdamu kiasi cha Sh 1,500,000 zitakazokwenda kumsaidia wakati akitafuta kupona majeraha yake.

Arafat alisema ameguswa binafsi na kuamua kumchangia Mdamu, baada ya kuona taarifa zake za uhitaji kupitia gazeti na mitandao ya Mwananchi.

"Nimeona taarifa za Mdamu kupitia kwenu Mwananchi kwa ujumla niwapongeze kwa hili ambalo mmefanya,  kweli zinasikitisha sana, alikuwa kijana ambaye anajitafuta kupitia kipaji chake cha kucheza soka," alisema Arafat huku akiongeza;

"Mimi binafsi nimemchangia Sh 1.5 milioni, ili aweze kupigania afya yake kuwa sawa, naamini Mdamu afya yake itarejea ili aweze kuungana nasi kulijenga Taifa letu."

Pia Taasisi ya Mwamnyeto nayo leo imefika nyumbani kwa mchezaji huyo na kumpa kiasi cha shilingi 1 milioni kwa ajili ya matibabu yake.


Wasikie polisi

Katibu Mkuu wa Polisi Tanzania, ASP Michael Mtebene amesema kama taasisi watakaa na kuangalia namna nzuri ya kumsaidia mchezaji huyo, huku akiweka wazi pia wanaguswa kwa maana moja au nyingine kwa sababu alikuwa ni mchezaji wao.

"Tumeona kampeni mbalimbali ambazo zinaendelea na sisi kama taasisi tunaguswa kwa sababu alikuwa ni mchezaji wetu, hatujamtupa kama ambavyo wengi wao wanazungumza ila, wadau wa soka wanapaswa kutambua kila sekta ina taratibu zake," alisema Mtebene.