Mdhamini mpya Simba afanya kufuru, aizima Yanga

Mdhamini mpya Simba afanya kufuru, aizima Yanga

Muktasari:

  • Klabu ya Simba imeingia mkataba wa miaka mitano na kampuni ya michezo ya kubashiri ‘M-Bet' wenye thamani ya Sh26.1 bilioni.

MTENDAJI mkuu wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez amesema kitendo cha kampuni ya M-Bet kuweka udhamini kwao ni baada ya kuona thamani yao.

Kampuni hiyo imeingia mkataba wa miaka mitano na Simba wenye thamani ya Shilingi bilioni Ishirini na sita na milioni mia moja na itini na nane na Elfu tano (26,168,5000).

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Barbara amesema  M-Bet ni kampuni kubwa ya kubashiri Tanzania na imewekeza katika klabu kubwa Tanzania na Afrika Mashariki na ndio maana wamesaini mkataba huo.

“M-Bet imekidhi mahitaji yetu, huwezi kuona wanaenda sehemu nyingine kuweka udhamini katika klabu za hapa’’  amesema Barbara na kuongeza;

“Mkataba wetu na M-Bet ni upande wa timu ya wakubwa tu, timu za vijana na wanawake hauhusiani mkataba huu, labda kama tutafungua ukurasa mpya".

Barbara ameongeza akisema, ”Wadhamini wetu wote wanne wamejipanga vilivyo kuisapoti timu yetu ndani na nje ya nchi.

Kampuni hiyo inaingia kama mdhamini mkuu wa klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake na Sportpesa na mgawanyo wa fedha utakuwa kama ifuatavyo;

Mwaka wa kwanza - Sh4.670 bilioni
Mwaka wa pili - Sh4.925 bilioni
Mwaka wa tatu - Sh5.205 bilioni
Mwaka wa nne - Sh5.514 bilion
Mwaka wa tano - Sh5.853 bilioni.

Jumla ni Sh26,168,5000 ya mkataba huo kwa miaka mitano ndani ya Simba.