Mechi kumi vigogo kwa Fadlu Simba

Muktasari:
- Katika kipindi hicho cha misimu mitatu wakiendelea kuisindikiza Yanga kubeba makombe ya ligi, timu hiyo imenolewa na makocha saba tofauti, wapo waliokaimu nafasi ya kocha mkuu wengine wakiwa makocha wakuu moja kwa moja.
Dar es Salaam. Baada ya misimu mitatu ya tabu ambayo Simba wameipitia wakati watani zao wa jadi Yanga wakiwa na shangwe kubwa, msala umekwenda kumuangukia Kocha Fadlu Davids ambaye ana kazi kubwa ya kufanya kuirudisha timu hiyo kwenye kilele cha furaha.
Ipo hivi; Simba ambayo misimu minne mfululizo kuanzia 2017-2018 hadi 2020-2021 ilikuwa ikitamba kwa kubeba makombe ya Ligi Kuu Bara, kibao kimewageukia misimu mitatu iliopita wakijikuta wakiwasindikiza Yanga.
Katika kipindi hicho cha misimu mitatu wakiendelea kuisindikiza Yanga kubeba makombe ya ligi, timu hiyo imenolewa na makocha saba tofauti, wapo waliokaimu nafasi ya kocha mkuu wengine wakiwa makocha wakuu moja kwa moja.
Makocha hao ni Masoud Juma (kaimu kocha mkuu), Zoran Maki (kocha mkuu), Juma Mgunda (kaimu kocha mkuu), Pablo Franco (kocha mkuu), Suleiman Matola (kaimu kocha mkuu), Roberto Oliveira 'Robertinho (kocha mkuu) na Abdelhak Benchikha (kocha mkuu).
Kuondoka kwa Benchikha na kuja Fadlu, Simba imedhamiria msimu huu kufanya mapinduzi ndani ya Ligi Kuu Bara huku kiu yao kubwa ikiwa ni kubeba taji hilo linaloshikiliwa na Yanga.
Katika kuwania taji hilo, Fadlu anapaswa kuhakikisha anaanza vizuri mechi 10 za kwanza ambazo zinaonekana si rahisi kupata ushindi kama hajajipanga vyema kutokana na aina ya wapinzani anaokwenda kukutana nao.
Baada ya ratiba ya ligi kutoka wiki iliyopita huku Simba mechi yao ya kwanza ikiwa Agosti 18 mwaka huu nyumbani dhidi ya Tabora United, Fadlu anapaswa kuangalia watangulizi wake walianzaje na mwisho wa siku walifeli wapi kubeba ubingwa uliochukuliwa na Yanga.
Mechi kumi za kwanza zinaonyesha timu hiyo iliyochagua kuutumia Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge kwa mechi zao za nyumbani, itakutana na wapinzani wake wakubwa, Azam (ugenini) na Yanga (nyumbani).
Misimu mitatu nyuma, Simba pia walikutana nazo ndani ya mechi 10 za kwanza zilizotibua hesabu zao za ubingwa kwani mara tatu walizocheza dhidi ya Yanga wakati huo, haikushinda hata moja, iliambulia sare mbili na kupoteza moja kwa kichapo kizito cha mabao 5-1. Hata ule msimu wa mwisho kwao kubeba ubingwa, hawakushinda dhidi ya Yanga zaidi ya kutoka 1-1.
Kwa upande wa mechi dhidi ya Azam, ndani ya misimu mitatu iliyopita, wamekutana mara mbili katika mechi 10 za kwanza, Simba ilishinda moja na kupoteza moja.
Mbali na vigogo wenzake, pia Simba itapambana dhidi ya Tabora United (nyumbani), Fountain Gate (nyumbani), Namungo (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Coastal Union (nyumbani), Tanzania Prisons (ugenini), Mashujaa (ugenini) na JKT Tanzania (nyumbani).
Fadlu anaweza kutembea na faili la Gomes ambaye alikuwa kocha wa mwisho kuipa kombe la ligi Simba, licha ya kwamba mechi 10 za kwanza hakuanza vizuri, lakini alizichanga vizuri karata zake mbele ya safari na kumaliza mabingwa kwa kukusanya pointi 64 ambazo kwa namna ushindani ulivyo hivi sasa, hizo ni chache zaidi kukusanywa na bingwa.
Gomes wakati anaipa Simba ubingwa wa mwisho wa ligi msimu wa 2020-2021, matokeo ya mechi 10 za kwanza alijikuta akikusanya pointi 20 kati ya 30, akishinda mechi sita, sare mbili na kupoteza mbili.
Baada ya hapo, msimu wa 2021-2022, Simba mechi 10 za kwanza ilikusanya pointi 24, licha ya kutopoteza mechi hata moja ikishinda saba, lakini ilimaliza msimu nafasi ya pili ikiambulia pointi 61.
Msimu wa 2022-2023, Simba ambayo ilimaliza ligi nafasi ya pili kwa pointi 73, mechi 10 za kwanza ilikusanya pointi 21 kati ya 30, ilishinda mechi sita, sare tatu na kupoteza moja, huku msimu wa 2023-2024 walimaliza nafasi ya tatu na pointi 69. Mechi 10 za kwanza walikusanya pointi 23, walishinda mechi saba, sare mbili na kupoteza moja.
Akizungumzia utayari wa kikosi chake kuelekea msimu mpya wa 2024-2025, Kocha Fadlu amesema anaridhishwa na vijana wake juu ya kile wanachokifanya kwenye uwanja wa mazoezi.
“Kwa maandalizi tuliyofanya na mechi tulizocheza kikosi changu kimeimarika sana, naridhishwa na vijana wangu wanafuata maelekezo yangu, kuna shida ndogondogo ambazo naamini zitatatuliwa kwa muda na kuwa na kikosi bora na shindani," alisema Fadlu.
Kocha huyo ambaye aliiongoza Simba kushika nafasi ya tatu katika Ngao ya Jamii mwaka huu huku akipoteza mbele ya Yanga kwa bao 1-0, amesema kabla ya mechi hizo za Ngao ya Jamii, alikiandaa kikosi chake kwa kucheza mechi za kirafiki ili kutafuta utimamu wa mwili kwa wachezaji wake.
“Kabla ya mechi dhidi ya Yanga na Coastal Union tulikuwa na mechi za kirafiki mfululizo lengo lilikuwa ni kutafuta utimamu wa mwili kwa wachezaji wangu ambao kwa asilimia kubwa wapo fiti na wanaendelea kuimarika siku hadi siku.
“Kijumla timu ipo tayari kwa mashindano na maeneo mengine ambayo yana kasoro ndogondogo naendelea kuyafanyia kazi kabla ya mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Tabora United Agosti 18, mchezo ambao nahitaji matokeo mazuri ili kuiweka timu yangu kwenye hali nzuri ya ushindani,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.
MECHI 10 ZA KWANZA 2024-2025
Simba v Tabora United
Simba v Fountain Gate
Azam v Simba
Simba v Namungo
Dodoma Jiji v Simba
Simba v Coastal Union
Simba v Yanga
TZ Prisons v Simba
Mashujaa v Simba
Simba v JKT Tanzania
MATOKEO MECHI 10 2023-2024
Mtibwa 2-4 Simba
Simba 2-0 Dodoma Jiji
Simba 3-0 Coastal
Prisons 1-3 Simba
Singida 1-2 Simba
Simba 2-1 Ihefu
Simba 1-5 Yanga
Simba 1-1 Namungo
Simba 3-0 Kagera
KMC 2-2 Simba
USHINDI: 7
SARE: 2
KUPOTEZA: 1
POINTI: 23
MWISHO WA LIGI: NAFASI YA TATU (POINTI 69)
MECHI 10 ZA KWANZA 2022-2023
Simba 3-0 Geita Gold
Simba 2-0 Kagera Sugar
Simba 2-2 KMC
Prisons 0-1 Simba
Simba 3-0 Dodoma Jiji
Yanga 1-1 Simba
Azam 1-0 Simba
Simba 5-0 Mtibwa
Singida BS 1-1 Simba
Simba 1-0 Ihefu
USHINDI: 6
SARE: 3
KUPOTEZA: 1
POINTI: 21
MWISHO WA LIGI: NAFASI YA PILI (POINTI 73)
MECHI 10 ZA KWANZA 2021-2022
Biashara Utd 0-0 Simba
Dodoma Jiji 0-1 Simba
Simba 1-0 Polisi TZ
Simba 0-0 Coastal
Simba 1-0 Namungo
Ruvu 1-3 Simba
Simba 2-1 Geita
Simba 0-0 Yanga
KMC 1-4 Simba
Simba 2-1 Azam
USHINDI: 7
SARE: 3
KUPOTEZA: 0
POINTI: 24
MWISHO WA LIGI: NAFASI YA PILI (POINTI 61)
MECHI 10 ZA KWANZA 2020-2021
Ihefu FC 1-2 Simba
Mtibwa Sugar 1-1 Simba
Simba 4-0 Biashara United
Simba 3-0 Gwambina
JKT Tanzania 0-4 Simba
Prisons 1-0 Simba
Simba 0-1 Ruvu
Simba 5-0 Mwadui
Simba 2-0 Kagera
Yanga 1-1 Simba
USHINDI: 6
SARE: 2
KUPOTEZA:2
POINTI: 20
MWISHO WA LIGI: MABINGWA (POINTI 64).