Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi sita kali za CAF wikiendi

Hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ngazi ya klabu inaanza kuchezwa wikiendi huku timu nne za Tanzania zikishuka dimbani.

Yanga na Simba zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na zote zinaanzia nyumbani, wakati Azam na Singida Black Stars zikicheza ugenini Kombe la Shirikisho Afrika.

Ukiweka kando wawakilishi wa Tanzania, kwa jumla wikiendi kuna mechi sita kali za CAF tunazokwenda kushuhudia.

Ukali wa mechi hizo unatokana na historia ya timu zinazokwenda kukutana na rekodi zao.


SIMBA VS PETRO LUANDA

Hii itapigwa Novemba 23, 2025 majira ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Ni mechi ya kundi D linaloundwa na timu za Simba, Petro Luanda, Esperance na Stade Malien.

Utamu wa mechi hii unatokana na aina ya timu zinazokwenda kukutana. Simba imekuwa na wakati mzuri sana uwanja wa nyumbani, licha ya kwamba msimu huu haijashinda zaidi ya kuambulia sare katika mechi mbili dhidi ya Gaborone 1-1 na Nsingizini 1-1.

Hata hivyo, tangu mara ya mwisho Machi 29, 2024 Simba ifungwe nyumbani bao 1-0 na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali, haijapoteza ikiwa nyumbani kunako michuano ya CAF. Kuanzia hapo, Simba imeshuka dimbani mara nane, imeshinda tano na sare tatu.

Inakutana na Petro Luanda, timu inayoshinda popote ikifanya hivyo hatua za mtoano msimu huu ambapo mechi zote nne imeibuka na ushindi ugenini na nyumbani.

Pia timu hiyo katika mechi nne za awali kabla ya kufuzu makundi, imefunga mabao kumi, haijaruhusu nyavu zake kutikiswa ikizichapa Cercle de Joachim (6-0) na Stade d'Abidjan (4-0). Wakati Simba ikifunga mabao matano na kuruhusu moja.

Ukali wa safu ya ushambuliaji wa Petro Luanda ndio unatajwa kuwa mwiba mchungu kwa Simba ambayo yenyewe haijapoteza nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja katika michuano ya CAF.

Katika misimu mitatu iliyopita kwenye ushiriki wa michuano ya CAF, Petro Atletico imeishia makundi (2022-2023), robo fainali (2023-2024) na hatua ya pili (2024-2025) zote Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa Simba, imeishia robo fainali mara mbili Ligi ya Mabingwa Afrika (2022-2023) na (2023-2024), huku 2024-2025 ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.


YANGA VS FAR RABAT

Dimba la New Amaan lililipo Zanzibar, linakwenda kutumika kwa mechi hii ya Kundi A katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Itakuwa Jumamosi Novemba 22, 2025 saa 10 jioni.

Yanga inaingia uwanjani ikiwa na rekodi ya kucheza hatua ya makundi ya CAF kwa msimu wa nne mfululizo ikifanya hivyo 2022-2023 (Kombe la Shirikisho), 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026 zote ikiwa Ligi ya Mabingwa.

Rekodi kubwa zaidi ya Yanga katika CAF ni kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.

Wapinzani wao, AS FAR Rabat, wana mataji mawili ya CAF, Ligi ya Mabingwa walilibeba mwaka 1985 na Kombe la Shirikisho (2005).

Mechi hii imebeba maana kubwa kwa kila upande kutokana na kundi lake kutajwa ni gumu. Mbali na wawili hao, kuna Al Ahly na JS Kabylie, timu zote zikiwa na rekodi zake bora CAF.

Umuhimu wa Yanga kushinda, unaifanya mechi hii kuwa na mvuto wa aina yake ikizingatiwa ndiyo mechi ya kwanza ya Kocha Pedro Goncalves upande wa kimataifa tangu akabidhiwe kikosi cha Yanga kutoka kwa Romain Folz.


AS MANIEMA VS AZAM

Stade des Martyrs, dimba lililopo Kinshasa nchini DR Congo ndipo kutafanyika mechi hii ya Kombe la Shirikisho Afrika, Novemba 23, 2025 saa 10 jioni.

Ni mechi ambayo mshambuliaji wa Azam, Jephte Kitambala anakutana na waajiri wake wa zamani kwani kabla hajatua viunga vya Chamazi msimu huu, alikuwa akiitumikia AS Maniema. Pia kocha mkuu wa Azam, Florent Ibenge, anakutana na ndugu zake Wakongomani.

Azam ikiwa ndio mara yao ya kwanza kucheza hatua ya makundi katika mashindano ya CAF, matumaini yao ni kuanza vizuri na uwepo wa Ibenge mwenye rekodi nzuri kunako mashindano hayo, yanaifanya mechi kuwa ya mvuto.

Mbali na hilo, namna kundi lilivyo likiwa na timu za Azam, Wydad, Maniema na Nairobi United, inatoa picha kwamba kuna timu moja inayopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi.

Wydad inaonekana kuwa hatari zaidi katika kundi hili kutokana na rekodi zake za mashindano ya CAF kulinganisha na wapinzani wake kwani imebeba Ligi ya Mabingwa mara tatu na CAF Super Cup moja. Hakuna timu nyingine iliyobeba wala kufika fainali ya CAF katika kundi hili la B.

Wydad ambayo inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri, inaacha nafasi moja kwa timu tatu kuwania kuvuka kwenda robo fainali, hivyo Azam, Maniema na Nairobi United kazi ipo.


CR BELOUIZDAD VS SINGIDA BS

Kwa mara ya kwanza, Singida Black Stars inashiriki mashindano ya CAF na kufuzu makundi ikiwa inafundishwa na Miguel Gamondi.

Mechi hii ya Kundi C katika Kombe la Shirikisho Afrika itachezwa Jumamosi Novemba 22, 2025 saa 4 usiku kwenye Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Algiers nchini Algeria.

Mechi hii ina utamu wake kutokana na makocha wanaokwenda kukutana kwani wote wamewahi kupita Yanga. Gamondi na Sead Ramovic.

Gamondi wakati anaondoka Yanga Novemba 2024, mikoba yake ilichukuliwa na Ramovic ambaye sasa yupo CR Belouizdad.

Msimu wa 2024-2025, Gamondi aliiacha Yanga ikiwa imefuzu makundi Ligi ya Mabingwa, Ramovic akashindwa kuivusha zaidi ya hapo, sasa wanakutana wakiwa na timu tofauti hatua ya makundi. Ngoja tuone itakuwaje.

Akizungumzia mechi hiyo, Ramovic amesema: “Najua Singida ni timu mpya kwenye michuano hii, lakini hawatakuja hapa kutembea. Wanakuja kupambana, mimi pia nataka hilo. Uzoefu wangu Tanzania najua utasaidia. Najua aina yao ya uchezaji ilivyo, nimeiona ni moja ya timu shindani.

“Tunawaheshimu, lakini hatutawaacha wapumue. Hapa ni nyumbani kwetu na tutajua namna ya kuwakaribisha.”


AL AHLY VS JS KABYLIE

Mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly watakuwa nyumbani katika Dimba la Cairo International lililopo Cairo nchini Misri, kuikaribisha JS Kabylie, ikiwa ni mechi ya Kundi A ya michuano hiyo.

Al Ahly yenye mataji 12 ya Ligi ya Mabingwa na moja Kombe la Shirikisho, inaikaribisha JS Kabylie ambayo yenyewe ina mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa. Pia ina rekodi ya kushinda mataji matatu mfululizo ya CAF Cup 2000, 2001 na 2002, mashindano hayo sasa ndio yanaitwa Kombe la Shirikisho.

Kwa michuano ya CAF, timu hizi zote zina msuli mnene, lakini kwa miaka ya karibuni, Al Ahly ndio wababe zaidi ya JS Kabylie.

Hesabu za kila mmoja kuanza vizuri hatua ya makundi ndio inachangia utamu wa mechi hii ikizingatiwa kundi lenyewe limekaa kimtego.

Ukiiacha Yanga ambayo haina taji lolote la CAF, katika Kundi A kuna Al Ahly, JS Kabylie na FAR Rabat ambazo zinapigana vikumbo kutanua rekodi zao.


AL MASRY VS KAIZER CHIEFS

Uwanja wa Suez uliopo Suez nchini Misri, utazikutanisha timu hizi katika Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika ambalo pia lina Zamalek ya Misri na Zesco ya Zambia.

Hili ni kundi pekee katika michuano ya CAF msimu huu lenye timu mbili zinazotoka taifa moja. Al Masry na Zamalek.

Uwepo wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika kundi hili, kuna ugumu wake kwani timu hizo tatu ukiiweka kando Zesco, zitapigana vikumbo kuwania nafasi mbili za kufuzu robo fainali.

Al Masry imekuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho ambapo mara ya mwisho ilikuwa 2021-2022 ikiishia robo fainali ikiondosha na RS Berkane iliyokwenda kubeba ubingwa.

Kuondoka kwa Nasreddine Nabi ndani ya Kaizer Chiefs, timu imebaki mikononi mwa Khalil Ben Youssef and Cedric Kaze ambao wamepewa jukumu la kuiongoza hatua ya makundi.

Mtihani wa makocha hao waliokuwa wasaidizi wa Nabi ambao pia alikuwa nao ndani ya Yanga, unaanza ugenini kwa Al Masry.

"Tunajua kwamba katika mashindano haya kuna klabu nyingi bora, hivyo tunafurahi sana kuhusu changamoto iliyo mbele yetu," amesema Kaze.