Mechi za uamuzi Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Jambo la kwanza linaloweza kutokea katika raundi hii ni Yanga kujihakikishia rasmi ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa Simba na Azam zitapoteza mechi zao za leo na yenyewe ikaibuka na ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar kesho.

Wakati mechi za raundi ya 27 ya Ligi Kuu Tanzania Bara zikianza kuchezwa leo katika viwanja tofauti, upo uwezekano wa mambo matatu kuamriwa baada ya matokeo ya michezo yake kabla hata ya raundi tatu zitakazobakia msimu kuhitimishwa.

Raundi hiyo itaanzia kwa mechi tatu zitakazochezwa leo ambazo ni kati ya Kagera Sugar na Simba, Tabora United dhidi ya Mashujaa na KMC itakayokabiliana na Azam FC wakati kesho pia kutakuwa na mechi baina ya Tanzania Prisons na Ihefu, Mtibwa na Yanga, JKT Tanzania dhidi ya Singida Fountain Gate na mechi kati ya Dodoma Jiji na Namungo huku keshokutwa kukiwa na mechi baina ya Geita Gold na Coastal Union.

Jambo la kwanza linaloweza kutokea katika raundi hii ni Yanga kujihakikishia rasmi ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa Simba na Azam zitapoteza mechi zao za leo na yenyewe ikaibuka na ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar kesho.

Ushindi wa Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu kesho, utaifanya ifikishe pointi 71 ambazo hazitoweza kufikiwa na Simba na Azam FC ikiwa zenyewe zitapoteza mechi zao.

Kama ikipoteza mbele ya KMC, Azam FC iliyo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na pointi zake 57 itaweza kuishia kumaliza ikiwa na pointi 66 wakati Simba iliyo katika nafasi ya tatu na pointi zake 56 itaweza kuishia kwenye pointi 68, jambo litakaloifanya Yanga itangaze ubingwa msimu huu ambao utakuwa wa wa tatu kwake mfululizo

Jambo la pili linaloweza kutokea ni timu za Coastal Union, Tanzania Prisons na KMC kukwepa rasmi kushuka daraja moja kwa moja na hivyo kubaki na kibarua chepesi cha kukwepa mechi za mchujo.

Hilo litatimia ikiwa Tabora United itapoteza mbele ya Mashujaa na Mtibwa kupoteza kwa Yanga kwani hata zikipata ushindi katika mechi tatu zitakazobakia hazitoweza kufikia pointi zile ambazo timu za Coastal Union, Tanzania Prisons na KMC zimekusanya  hadi sasa ambapo kila moja ina pointi 33.

Jambo la tatu linaloweza kutokea ni ndoto za Mtibwa Sugar kujihakikishia kubaki moja kwa moja ligi kuu kufutika ikiwa itapoteza mchezo wake dhidi ya Yanga kesho na Ihefu, Singida Fountain Gate na Dodoma Jiji kila moja ikapata ushindi au kutoka sare katika mechi yake.

Mtibwa ikipoteza mbele ya Yanga, maana yake itakuwa na uhakika wa kumaliza ligi ikiwa na pointi 29 ambazo zitaifanya imalizie ikiwa katika nafasi nne za chini ambapo ikiwa ni zile mbili za mkiani, itashuka daraja moja kwa moja lakini kama ikimaliza katika nafasi ya 13 au 14, itacheza mechi za mchujo za kuwania kubaki Ligi Kuu.

Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry alisema kuwa pamoja na kuwa katika nafasi finyu ya kutwaa ubingwa, watajitahidi kushinda mechi yao dhidi ya KMC na iliyobakia ili kuona watavuna nini mwishoni mwa msimu.

"Tutaendelea kucheza mpaka dakika ya mwisho maana kwenye mpira lolote linaweza kutokea. Timu imefanya kazi kubwa maana hatujapoteza mecghi nyingi mfululizo za Ligi hadi tulipokuja kufungwa mechin iliyopita (dhidi ya Simba," alisema Ferry.

Kocha wa Tabora United, Masoud Juma, alisema kuwa nafasi waliyopo sio nzuri na wanahitajika kushinda mechi zao zilizobakia hasa dhidi ya Mashujaa leo.

"Tunafahamu kabisa kuwa hautakuwa mchezo mwepesi kwa sababu kila Timu inahitaji kufanya vizuri kwa maana ya kuvuna alama zote tatu ili kuweza kujiimarisha kwenye msimamo, tumejiandaa kupambana na tunaamini kuwa kila kitu kitakuwa sawa".

"Kwa upande wa Afya za wachezaji wote wapo vizuri, wanahari, morali na kwamba kila mmoja yupo tayari kutumika kesho isipokuwa,  tutawakosa wachezaji wawili kutokana na changamoto mbalimbali. Jerome Lambele amefiwa na dada yake hivyo amekwenda kwenye msiba nyumbani kwao Kigoma , Emotan Cletus bado anasumbuliwa na nyama za paja," alisema Juma.

Kocha wa Mashujaa FC, Mohammed Abdallah 'Baresi' alisema nia yao ni kupata ushindi katika mechi ya leo.

"Kwa sasa kila mechi ni muhimu na hutakiwi kupoteza kwani ukifanya hivyo unazidi kudidimia huku ukimpa fursa mwenzako kusogea jambo ambalo hatuhitaji kuliona kwa upande wetu," alisema Baresi.