Meneja Uwanja wa Mkwakwani Tanga asimamishwa kwa uzembe
Mwonekano wa Uwanja wa Mkwakwani, uliopo Tanga ambao unatumiwa na Klabu ya Coastal Union. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, amemsimamisha kazi meneja wa Uwanja wa CCM Mkwakwani akimtuhumu kushindwa kusimamia ipasavyo miundombinu ya uwanja huo.
Tanga. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah, amemsimamisha kazi Meneja wa Uwanja wa CCM Mkwakwani, Akida Machai, kwa tuhuma za kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya usimamizi wa uwanja huo.
Uamuzi huo umetangazwa Jumatano, Machi 11, 2016 wakati Abdallah alipofanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo ili kukagua hali ya miundombinu na uendeshaji wake.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Abdallah amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na chama katika kuboresha uwanja huo hauonekani kuwa na matokeo kutokana na usimamizi hafifu wa meneja.
“Hapa tunalipa umeme, maji yanalipwa na Chama Cha Mapinduzi. Lengo ni kuwafanya wananchi waendelee kunufaika na mpira wa miguu pamoja na michezo mingine. Tunapotoa fedha tunataka kuona matokeo,” amesema Abdallah.
Ameongeza kuwa hata yeye binafsi amechangia Sh50 milioni kwa ajili ya ukarabati wa uwanja huo, hivyo haikubaliki kuona miundombinu yake ikiendelea kudorora.
“Mimi mwenyewe nimetoa shilingi milioni hamsini kukarabati uwanja huu. Haiwezekani uwanja ukaonekana kama mbuga ya wanyama kwa sababu ya uzembe wa usimamizi,” amesisitiza.
Aidha, amesema viti vilivyoletwa kwa ajili ya kufungwa uwanjani hapo vimekaa kwa muda mrefu bila kufungwa hadi kuanza kuota majani.
Amesema hali ya usimamizi uwanjani hapo wakati fulani ilipelekea uwanja huo kufungiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kutokana na hali hiyo, Abdallah ameagiza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Tanga kukaa haraka na kutafuta meneja mpya atakayesimamia ipasavyo uwanja huo.
Pia ametoa maelekezo ya kuondolewa kwa baa iliyopo nje ya uwanja wa Mkwakwani akidai haikidhi vigezo na imekuwa ikizuia mashabiki na wachezaji kuingia kwa urahisi wakati wa mechi, jambo ambalo tayari TFF lilishawahi kulilalamikia.
Kwa upande wake, Meneja aliyesimamishwa kazi, Akida Machai, ameshukuru kwa nafasi aliyopatiwa ya kusimamia uwanja huo na kumtakia mafanikio meneja mpya atakayeteuliwa.
Kuhusu suala la kufungwa kwa viti uwanjani hapo, Machai amesema tayari aliwasilisha bajeti kwa uongozi wa chama ndani ya wiki moja tangu viti hivyo vifike, akisisitiza kuwa hakuwa na uwezo wa kugharamia kazi hiyo kwa fedha zake binafsi.