Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MZEE WA FACT: Ratiba na miundombinu ni Kansa ya ligi yetu

Ligi Kuu ya Tanzania inashika namba sita barani Afrika kwa ubora. Hiki ni moja ya vitendawili vigumu zaidi kuvielezea na mtu akavielewa.

Namba kwa ubora, ubora wa nini?

1. Miundombinu?

2. Vipaji?

3. Pesa?

4. Mafanikio?

5. Utawala bora?

Haya yote ukiyaweka kwenye uhalisia wake, ligi yetu haiwezi hata kuwa katika kumi bora. Lakini kwa maajabu ya Mungu, ni namba sita. Ingekuwa hii nafasi ya sita imepatikana kwa kupigiwa kura, tungesema kulikuwa na uchakachuaji.

Kanuni zinazotumika kupima ubora wa ligi ni za kuunga unga sana ndio maana zinatoka na majibu kama haya.

Moja ya changamoto zinazoikabili ligi yetu na kuwafanya watu wengi kutilia shaka nafasi yake barani Afrika ni mambo rahisi sana kama miundombinu na ratiba.

Achana na matatizo ya uamuzi haya ni mtambuka sana. Na pia yapo dunia nzima, hata kwa nchi zilizoendelea na kutumia teknolojia kubwa lakini bado waamuzi ni tatizo.

Kutoa mafunzo ya kina kwa waamuzi, au kufunga teknolojia kama VAR au GLT kunahitaji pesa nyingi, hilo tuliache. Tuipime ligi yetu kwa vitu viwili vyepesi, miundombinu na ratiba.

Ni vyepesi kwa sababu vinahitaji maamuzi tu, wala sio pesa nyingi au maarifa makubwa sana.


MIUNDOMBINU

Unaweza kusema kwamba miundombinu bora inahitaji uwekezaji mkubwa na uwekezaji mkubwa unahitaji pesa nyingi. Kwa hiyo mtu anaweza kuhoji kwamba kusema kwamba yanahitajika maamuzi pekee, labda sio sahihi.

Ukweli ni kwamba ligi yetu inachezwa kwenye miundombinu mibovu sana ambayo inatumia pesa nyingi sana. Yaani pesa inayotumika kwa miundombinu hii mibovu ingeweza kutumika nusu yake tu na kuifanya kuwa bora sana.

Achana na majukwaa, nazungumzia eneo tu la kuchezea. Viwanja vyetu vinaharibika kwa sababu tu nyasi hazimwagiwi maji.

Tanzania ni moja ya nchi zenye vyanzo vingi sana vya maji na mabomba ya maji yapo viwanjani na maji yanatoka. Nyasi zinakauka, uwanja unafungiwa kisha pesa nyingi zinatumika kuukarabati.

Ukishakaa sawa, unafunguliwa nyasi hazimwagiwi, uwanja unaharibika unafungiwa tena. Pesa nyingine inatumika kufanya ukarabati.

Huo ndio mzunguko wa hali ya viwanja vyetu. Mwanza, Tabora, Mbeya, Kigoma, Dodoma na kadhalika. Unaweza kujiuliza, huu ni mradi wa watu kwa ajili ya upigaji, au? Gharama zinatumika kufanya marekebisho ya uwanja mara kwa mara, zingetumika nusu yake tu kuimarisha mifumo ya umwagiliaji, maisha yangekuwa mepesi.

Uwanja wa Sokoine Mbeya ulifungiwa umechezewa mechi moja tu tangu ufunguliwe, Mbeya City vs Fountain Gate, tayari umeharibika.

Mechi ya Tanzania Prisons na Azam FC ilichezwa kwenye shamba la mpunga, sio uwanja. Hapo unaweza kufungiwa tena hela ikatumika tena kufanya marekebisho, na ukarudi vilevile.



RATIBA

Pata picha kwenye nchi kubwa kama Tanzania ambayo ligi inachezwa kila kona, halafu mechi ni kila baada ya siku mbili. Machi Mosi kulikuwa na mechi moja tu ya ligi, Yanga na Simba, ambayo ilianza saa mbili usiku.

Saa 10 jioni na saa 12 jioni, ingewezekana kukawa na mechi zingine, lakini hawakuweka, badala yake mechi zote zikawa Machi 2.

Halafu timu zilizocheza siku hiyo, zikawa na mechi nyingine Machi 5. Nitaitolea Azam FC kama mfano.

Ilicheza Machi mbili dhidi ya Pamba Jiji, mjini Mwanza halafu ikacheza na Tanzania Prisons Machi tano mjini Mbeya. Maana yake baada ya mechi ya Machi pili, kukawa na safari ya kutoka Mwanza kwenda Mbeya. Huu ni umbali wa kilomita zaidi ya mia tisa. Kusafiri kwa barabara ni safari ya zaidi ya saa 15. Ok, tuseme hawa ni Azam, watoto wa Bakhresa, mtu mwenye pesa zake kwa hiyo watapanda ndege.

Hakuna ndege ya moja kwa moja kutoka Mwanza kwenda Mbeya ni hadi ufike Dar es Saalam na kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya ndege ni moja tu kwa siku, saa kumi jioni.

Kwa hiyo baada ya mechi, Machi pili wakasafiri Machi tatu hadi Dar es Salaam na jioni wakapanda ndege kwenda Mbeya. Hiyo siku imekufa bila mazoezi wanafika Mbeya na kufanya mazoezi ya siku moja, kesho yake mechi.

Kwa utaratibu wa sayansi ya michezo, ni muhimu sana kufanya mazoezi ya kurudisha mwili kwenye hali ya kawaida (recovery), siku moja baada ya mechi, hawakupata nafasi.

Kwanini ile mechi ya Machi 2 isingechezwa Machi Mosi saa kumi jioni, halafu Machi 2 wakapata muda mzuri wa kurudisha miili katika hali ya kawaida, na Machi tatu wakasafiri kwa utulivu? Kuliona hili inahitaji pesa kiasi gani kuliona? Machi 19, Kigoma na Machi 22 Singida.

Kwa barabara huu ni umbali wa zaidi ya kilomita 700, safari ya zaidi ya saa 10 barabarani. Singida hakuna uwanja wa ndege, hivyo kama ndege itatumika, basi ni hadi Dodoma.

Kutoka hapo ni kwa basi maana yake hiyo ni Machi 20, siku inakufa hivyo, bila kurudisha miili ya wachezaji katika hali ya kawaida. Machi 21 ni mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mechi ya Machi 22.

Ukiwa na ratiba ya aina hii tegemea wachezaji kuwa na uchovu na kusababisha mechi kupooza. Mbaya zaidi hali hii husababisha majeraha kwa wachezaji kwa sababu hucheza wakiwa na utimamu mdogo wa mwili.

Na ratiba ya aina hii sio Azam tu, ni kwa timu zote. Haya, Azam, Simba na Yanga wanaweza kuwa na jeuri ya kupanda ndege, vipi hawa wengine, wenzangu na mimi? Hivi kupanga ratiba vizuri kunahitaji pesa kiasi gani?


HITIMISHO

Ligi yetu ni nzuri na ina ushindani mkubwa sana wageni wengi wamekiri. Lakini wakati maeneo mengine yakiboresheka, miundombinu na ratiba imebaki palepale.

Ni muhimu wasimamizi wa ligi kuumiza sana kichwa kwenye hilo. Kwa sababu hapa yanahitajika maamuzi tu...sio mtaji mkubwa wa pesa.

Iamuliwe tu kwamba ligi itachezwa KMC Complex, Azam Complex, Meja Isamuhyo, Aman Complex na Gombani tu, basi. Hakuna uwanja wa kufanyiwa marekebisho kati ya Mwanza, Dodoma, Mbeya, Tabora na Kigoma. Vile ni viwanja vya kufumuliwa na nyasi kupandwa upya kabisa.