Miaka 10 ya kadi nyekundu Kariakoo Derby

Miaka 10 ya kadi nyekundu Kariakoo Derby

Muktasari:

  • Huwezi  kuamini kama ndani ya miaka 10 tangu mwaka 2011-2021 mchezo wa watani wa jadi, Yanga na Simba umekula vichwa vya wachezaji wengi kutokana na presha kubwa na kasi ya hali ya juu sana kiasi ambacho hata wachezaji wenye majina makubwa wameshindwa kuhimili mikiki hiyo.

Huwezi  kuamini kama ndani ya miaka 10 tangu mwaka 2011-2021 mchezo wa watani wa jadi, Yanga na Simba umekula vichwa vya wachezaji wengi kutokana na presha kubwa na kasi ya hali ya juu sana kiasi ambacho hata wachezaji wenye majina makubwa wameshindwa kuhimili mikiki hiyo.

Presha na kasi kubwa katika mechi hiyo ni vitu vinavyowafanya wachezaji wa klabu hizo kushindwa kudumisha nidhamu ya mchezo kwa dakika 90 na matokeo yake wamekuwa wakipata kadi nyekundu ingawa wakati mwingine lawama zimekuwa zikitupwa kwa waamuzi.

Ngoja nikupe orodha ya wachezaji saba waliokumbana na kadi nyekundu katika kipindi hiki cha miaka 10 ya dabi ya Kariakoo.

HARUNA NIYONZIMA

Ni kiungo mwenye ubunifu mkubwa aliyepata mafanikio makubwa akiwa Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo, lakini kwa sasa amerejea nyumbani kwao, Rwanda, anaitumikia AS Kigali.

Machi 8, 2015, alikuwa miongoni mwa wachezaji waliopata kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Simba.

Alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 74 baada ya kuupiga mpira wavuni wakati mwamuzi wa mchezo huo akiwa tayari amepuliza kipyenga kuashiria ‘offside’.

Mchezo huo uliisha kwa Yanga kupoteza bao 1-0, bao lililofungwa na Emmanuel Okwi ambaye misimu mitatu iliyopita alikuwa akiitumikia Simba.


MBUYU TWITE

Ni Mnyarwanda aliyepata mafaniko makubwa akiwa Yanga, itakumbukwa Septemba 27, 2015 katika mchezo dhidi ya Simba na walishinda mabao 2-0, alishindwa kumaliza mchezo huo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu.

Alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo, Israel Nkongo dakika za nyongeza (90+8) baada ya kuchelewesha muda kwa makusudi wakati alipokwenda kurusha mpira kipindi timu yake ikiwa mbele mabao 2-0.


ABDI BANDA

Kwa sasa amesajiliwa Mtibwa Sugar, alipoondoka Simba alienda kukipiga Afrika Kusini, ingawa anakumbukwa kwa tukio lake la kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza cha mchezo uliopigwa Februari 20, 2016.

Alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 21 baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma, wakati Yanga walipofanya shambulizi la kushtukiza.

Mnamo dakika ya 25, Yanga walifanya shambulizi lingine la kushtukiza na Banda alimchezea tena rafu Ngoma ambaye alikuwa akielekea langoni mwa Simba, mwamuzi wa mchezo huo, Jonisia Rukyaa alimuonyesha Banda kadi ya pili ya njano na kumpa kadi nyekundu, kwenye mchezo huo Simba ilipoteza mabao 2-0.


JONAS MKUDE

Mkude ni mchezaji tegemezi wa Simba, ingawa kwa sasa anatajwa kuwa kwenye ushindani wa namba na wachezaji wengine wawili wa kigeni ambao ni Thadeo Lwanga na Sadio Kanoute, wanaocheza nafasi ya kiungo mkabaji.

Mkude miongoni mwa wachezaji wanaoingia kwenye orodha ya wachezaji waliotolewa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu katika mchezo wa watani wa jadi.

Alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 26 ya kipindi cha kwanza baada ya kumsukuma mwamuzi mpaka akaanguka chini.

Kiungo huyo wa Simba alifanya kitendo hicho baada ya mwamuzi wa mchezo huo kulikubali bao lililofungwa na mshambuliaji wa Yanga, Amiss Tambwe, ambae alifunga kutokana na kuukontroo mpira kwa kutumia mkono wake wa kulia, licha ya Simba kuwa pungufu mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.


BESALA BOKUNGU

Mkongomani aliyesajiliwa Simba kwa ajili ya kuziba pengo la Shomari Kapombe, alikuwa ni beki wa kulia mwenye matumizi mazuri ya akili lakini alijikuta akiingia kwenye orodha ya wachezaji waliopata kadi nyekundu kwenye mechi ya watani wa jadi iliyopigwa Februari 25, 2017.

Alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mnamo dakika ya 55 baada ya kumchezea rafu aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa, ambaye alikuwa amebakiza mita zisizopungua mbili kuingia eneo la 18 la Simba.

Hata hivyo, licha ya Simba kumpoteza Bokungu, lakini waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.


HASSAN KESSY

Kabla ya kutimkia Nkana FC ya Zambia, Kessy alikuwa ni mchezaji aliyehamia Yanga akitokea Simba, lakini akiwa Yanga alijikuta akiwa miongoni mwa wachezaji waliopata kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Simba.

Aprili 24, 2018, alionyeshwa kadi mbili za njano na kupewa kadi nyekundu dakika ya 49 baada ya kumchezea rafu mbaya beki wa kushoto wa Simba, Asante Kwasi.

Katika mchezo huo Yanga ilipoteza bao 1-0, bao ambalo lilifungwa na beki wa kati wa Simba, Erasto Nyoni.


MUKOKO TONOMBE

Mukoko ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa tegemezi ndani ya Yanga, lakini ameingia katika orodha ya wachezaji ambao walishindwa kumaliza dakika 90, za mechi ya watani wa jadi kutokana na utovu wa nidhamu aliouonyesha katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Katika mchezo huo ambao ulipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, alionyeshwa kadi hiyo dakika ya 46, baada ya kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Simba, John Bocco, dakika ya 43, kipindi cha kwanza.

Mchezo huo wa fainali ulimalizika kwa Yanga kupoteza bao 1-0, kadi nyekundu aliyoipata Mukoko katika mchezo huo itamfanya kiungo huyo aukose mchezo wa Ngao ya Jamii ambao utachezwa kesho Jumamosi hii.