Moloko agomea mapumziko Yanga

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi anapiga hesabu kali za kuhakikisha mastaa wa kikosi chake wanapata muda wa kupumzika pindi wanapotumika sana, ila yupo mmoja ambaye ametumia fursa kivingine.

Ipo hivi: Winga wa timu hiyo, Jesus Moloko ambaye yupo kwenye kiwango kikubwa hataki mapumziko hayo kuna wakati anamwambia Kocha Nabi kwamba anahitaji kucheza zaidi ili kujiweka fiti.

Wakati Moloko anatua Yanga kwa mara ya kwanza Agosti 23, 2021 alisaini mkataba wa miaka miwili akitokea AS Vita ya DR Congo, hakuanza na kasi walioitarajia hadi ikatishia ajira yake, ila msimu huu ameanza kwa kasi na huduma yake imekuwa muhimu kwenye timu.

Kama kawaida kwenye kikosi cha Nabi ni kama kombolela mchezaji anayecheza vizuri ndiye anayepangwa ndicho kitu kinachomfanya Moloko akaze buti.

Moloko aliliambia Mwanaspoti :”Tukitoka kucheza michuano ya kimataifa mara nyingi kocha anatoa mapumziko, lakini mimi huwa namwambia asinipe nahitaji kucheza ili kujiweka kwenye ufiti zaidi.

Aliongeza: “Kuna ushindani wa namba mkali aliyepo benchi akipewa nafasi anapambana kwa kadiri kuisaidia timu, ndio maana sitaki kuichezea kabisa nafasi ninayopata nahitaji huduma yangu iwe muhimu kikosi cha kwanza.”

Alisema kila mchezaji anahitaji mafanikio ya timu hiyo akiwa miongoni mwa wachezaji walioitumikia kwa dakika nyingi kiwanjani hivyo anatamani kuwa miongoni mwa mastaa waliotumika zaidi.

“Ukifuatilia kwa ukaribu dakika nilizocheza sio nyingi msimu huu ukilinganisha na msimu uliopita kutokana na majeraha ya mara kwa mara hilo halina afya kwangu ninapopata muda wa kucheza natakiwa kuutumia;

“Nitapambana kikosini hadi pale timu itakapofikia malengo nitapumzika nikiwa sina utimamu wa mwili au nimepata shida katika kujiandaa ama kwenye mchezo hilo Kocha Nabi analifahamu.”

Kuhusu Monastir alisema hautakuwa mchezo rahisi wanahitaji maandalizi kujiweka fiti tayari kwaajili ya kuandika historia mpya Jumapili.

“Hautakuwa mchezo rahisi tunakutana na timu ambayo pia ina malengo sawa na sisi kunapata matokeo.”