Mourinho arejea rasmi Real Madrid, Perez akishinda uchaguzi
Muktasari:
- Perez, mwenye umri wa miaka 79, amepata asilimia 65 ya kura kayuu na kuendelea kuiongoza Madrid kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Madrid, Hispania. Kocha raia wa Ureno, Jose Mourinho, rasmi amerejea kuinoa Real Madrid baada ya rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, kuthibitishwa kuendelea kuiongoza timu hiyo kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika jijini Madrid Jumapili Juni 7.
Mourinho mwenye umri wa miaka 63 amesaini mkataba wa miaka mitatu mwezi uliopita kurejea Bernabeu, lakini utekelezaji wa makubaliano hayo ulikuwa ukisubiri matokeo ya uchaguzi wa urais wa klabu hiyo.
Baada ya ushindi wake kutangazwa rasmi, Perez amesema anafurahia kurejea kwa Mourinho ambaye aliwahi kuifundisha Madrid mwaka 2010 hadi 2013.
"Tunajivunia kumkaribisha tena mmoja wa makocha bora duniani, Madridista wa kweli," amesema Perez.
Muda mfupi baadaye, Mourinho alisambaza video kwenye mitandao ya kijamii akisema: "Ndiyo, Florentino Perez ameshinda. Bila shaka."
Perez, mwenye umri wa miaka 79, amepata asilimia 65 ya kura na kuendelea kuiongoza Madrid kwa muhula mwingine wa miaka mitano. Ushindi huo unamaanisha ataendelea kuwa rais wa klabu hiyo kwa jumla ya miaka 23 katika vipindi vyake viwili vya uongozi.
Katika kampeni zake za uchaguzi, Perez aliahidi kufanya usajili mkubwa angalau wa Euro 150 milioni (Sh460 bilioni) kwa nyota mmoja mkubwa, pamoja na kuongeza wachezaji wengine watatu katika kikosi hicho.
Majina yanayotajwa kuhusishwa na usajili huo ni pamoja na Nico Paz, Jacobo Ramon na Victor Munoz.
"Nitatoa ofa kwa klabu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki hii, ambayo itakuwa malipo makubwa zaidi kuwahi kutolewa na Real Madrid kwa mchezaji, angalau euro milioni 150 (Sh460 bilioni)," alisema Perez wiki iliyopita.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez wakati akizungumza na wanachana wa Klabu hiyo baada ya kutangazwa mshindi wa urais. Picha na Mtandao
Aliongeza: "Si Michael Olise, si Jeremy Doku, si Erling Haaland wala Harry Kane. Lakini ni mchezaji anayezidi kiwango cha viungo wa kawaida. Ni Galactico wa kweli."
Licha ya kauli hiyo, taarifa kutoka Hispania zinaeleza kuwa nyota wa Bayern Munich, Michael Olise, ndiye anayewindwa zaidi na Perez.
Katika uchaguzi huo, mpinzani wake, mfanyabiashara Enrique Riquelme, amepata asilimia 35 ya kura. Riquelme alikuwa ameahidi kumleta Jurgen Klopp kuwa kocha na kumteua Raul Gonzalez kama mkurugenzi wa michezo iwapo angeshinda.
Baada ya kushindwa, Riquelme amesema: "Kwetu huu si mwisho. Ni mwanzo. Wanachama wa klabu hawatasubiri tena miaka 20 bila kupiga kura."
Ushindi wa Perez sasa umefungua njia ya kukamilika kwa taratibu za kumtoa Mourinho katika klabu ya Benfica kwa kulipa kipengele chake cha kuvunja mkataba kinachofikia Euro 15 milioni (Sh46 bilioni).
Kocha wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho. Picha na Mtandao
Mourinho anarejea Madrid miaka 13 baada ya kuondoka, akiwa aliiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa La Liga, Kombe la Mfalme na Super Cup ya Hispania katika kipindi chake cha kwanza.
Kocha huyo sasa anakabidhiwa jukumu la kujenga upya kikosi cha hicho ambacho tayari kimesajili mabeki Ibrahima Konate na Denzel Dumfries, huku nyota kadhaa akiwamo Dani Carvajal na David Alaba wakitarajiwa kuondoka.
Mbali na usajili huo,Mourinho pia anakabiliwa na kazi ya kurejesha utulivu ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo kufuatia migogoro iliyotokea msimu huu, ikiwamo ugomvi uliowahusisha Federico Valverde na Aurelien Tchouameni.
Aidha, kocha huyo anatarajiwa kufanya tathmini ya kina katika idara za afya na maandalizi ya mwili baada ya Real Madrid kukumbwa na majeraha mengi msimu uliopita, hali iliyochangia kushuka kwa kiwango cha timu hiyo.