Mshtuko, Eriksen akidondoka tena uwanjani na kuzimia
Baadhi ya wachezaji wa Ukraine na Denmark wakiwa wamemzunguka kiungo wa Denmark, Christian Eriksen wakati alipokuwa akipewa huduma ya kwanza baada ya kuanguka ghafla. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Juni 12, 2021, Christian Eriksen alianguka uwanjani katika mchezo baina ya Denmark na Finland wa Kombe la Euro ambapo baadaye vipimo vilibainisha kuwa tatizo hilo lilitokana na kusimama kwa mapigo ya moyo.
Mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya Denmark na Ukraine, leo Jumapili, Juni 7, 2026 imesitishwa kufuatia kuanguka ghafla kwa kiungo wa Denmark, Christian Eriksen.
Hiyo ni mara ya pili kwa Eriksen kuanguka uwanjani ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni Juni 12, 2021 alipoanguka uwanjani katika mechi ya Kombe la Euro baina ya Denmark na Finland kutokana na tatizo la kusimama kwa mapigo ya moyo.
Video za tukio hilo zimemuonyesha Eriksen akishika kifua chake kabla ya kuanguka ghafla katika dakika ya 65 ya mchezo.
Mechi hiyo iliyokuwa ikichezwa katika mji wa Odense, Denmark baadaye ilisitishwa.
kiungo wa Denmark, Christian Eriksen. Picha na Mtandao
Wachezaji wa Denmark na Ukraine waliunda duara kumzunguka Eriksen alipokuwa akipatiwa huduma ya kwanza na wahudumu wa afya uwanjani hapo.
Baada ya mchezo huo kusitishwa, wachezaji pamoja na benchi la ufundi la timu zote mbili walisimama kwa kushikana mikono mabegani huku wakiwa wameunda duara.
Hata hivyo baadaye Daktari wa Denmark, Morten Boesen ambaye alisaidia kuokoa maisha ya mchezaji huo mwaka 2021, amesema kuwa Eriksen yuko sawa kiafya.
“Christian anaendelea vizuri na ametoka nje ya uwanja mwenyewe.
"Alipoteza fahamu kwa muda mfupi, lakini alirejewa na fahamu haraka sana na tuliweza kuwasiliana naye mara moja.
"Atafanyiwa uchunguzi zaidi hospitalini ili kubaini chanzo cha tukio hilo. Tunaendelea kuwasiliana naye pamoja na madaktari wa hospitali.
"Lakini Christian anaendelea vizuri, na aliniomba niwatumie salamu zake wachezaji wote na kuwaeleza kwamba yuko salama,” amesema daktari huyo.
Kiungo wa Denmark, Christian Eriksen alipoanguka ghafla mwaka 2021 wakati wa mechi ya Mashindano ya Euro iliyochezwa jijini Copenhagen dhidi ya Finland. Picha na Mtandao
Kumbukumbu ya 2021
Mwaka 2021, Eriksen alianguka ghafla wakati wa mechi ya Mashindano ya Euro iliyochezwa jijini Copenhagen dhidi ya Finland, na alipewa huduma ya uokoaji wa maisha ya CPR baada ya kupata mshtuko wa moyo uliosababisha moyo wake kusimama kufanya kazi.
Baadaye alipandikizwa kifaa maalumu cha kusaidia kurejesha mapigo ya moyo kinachojulikana kwa jina la kitaalam kama Implantable Cardioverter-Defibrillator (ICD).
Baada ya kupona, Eriksen hakuweza kuendelea kuichezea Inter Milan, ambayo alijiunga nayo akitokea Tottenham Hotspur mwaka 2020, kutokana na kanuni za nchini Italia kuwazuia wachezaji kushiriki mashindano wakiwa wamepandikizwa kifaa cha ICD.
Mkataba wake ulivunjwa mwaka 2021 na Eriksen alirejea katika soka la England Januari 2022 kwa kujiunga na Brentford FC kabla ya kuhamia Manchester United katika majira ya joto mwaka huohuo.
Aliichezea Manchester United katika mechi 107 na kufunga mabao manane, akishinda Kombe la Carabao 2023 na FA 2024.
Eriksen aliiondoka Manchester United mwishoni mwa mkataba wake mwaka 2025 na kwa sasa anaichezea VfL Wolfsburg ya Ujerumani.