Msuva acheza dakika 90 Saudia, apania mambo makubwa

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Ameonja utamu huo kwa kucheza kwa dakika 90 wakati Al-Najma ikiwa ugenini ambako ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Ohod Club.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva mwenye miaka 30, ameonja kwa mara nyingine tena utamu wa Ligi Daraja la Kwanza, Saudia huku akibebeshwa msala wa Mgambia, Ousmane Barry ambaye ndiye aliyekuwa akiongoza idara ya ushambuliaji ya Al-Najma.

Msuva ambaye ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Taifa Stars, ameonja utamu huo kwa kucheza kwa dakika 90 wakati Al-Najma ikiwa ugenini ambako ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Ohod Club na kuambulia pointi moja ambayo imewafanya kuwa katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza kati ya timu 18 wakiwa na pointi 20.  

Pamoja na ugeni wake, Msuva ambaye alipatia umaarufu akiwa na Yanga alianza rasmi kwenye mchezo huo na kubebeshwa majukumu ya Ousmane ambaye amejiunga na Al-Ula ya Ligi Daraja la Pili nchini humo mwezi uliopita. Ameondoka Al-Najma akiongoza orodha ya wafumania nyavu kwenye ligi hiyo akiwa na mabao 13.  

Licha ya kwamba hakufunga wala kutoa asisti, Msuva alitumika kama mshambuliaji wa kati (namba tisa), eneo ambalo awali alikuwa akicheza kwenye ligi hiyo wakati akiwa na Al-Qadsiah ambayo sasa ndiyo inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 41 baada ya michezo 20 kuchezwa.

Msuva aliyefunga bao pekee la Tanzania kwenye Afcon mwaka huu, alisema mabao yatakuja ni suala la muda tu kwake ambacho anapambana ni kuzoeana kwa haraka na wachezaji wenzake wapya kwenye kikosi hicho ili kufanikisha kwa wepesi mipango ya timu.

"Nina furaha kupata nafasi ya kucheza mchezo wangu wa kwanza na timu yangu mpya, ujue kuna kitu kwangu waliona ndio maana wakanisajili na mimi sipo tayari kuwaangusha," alisema Msuva na kuongeza;

"Napambana kuendana na wenzangu, hii ni hatua ya kawaida kwa mchezaji yoyote mpya, kuhusu ligi ni kweli kwamba ni ngumu lakini kwa bahati nzuri hii sio mara yangu ya kwanza kucheza, nina uzoefu wa kutosha tu hivyo nipo tayari kuwa msaada kwa timu yangu."

Wakati akiwa Saudia kwenye awamu yake ya kwanza, Msuva alipachika mabao manane na kuisaidia Al-Qadsiah kusalia kwenye Ligi Daraja la Kwanza nchini humo, kuna kipindi timu hiyo ilikuwa kati ya timu nne ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kushuka daraja