Mwakinyo njia panda

Muktasari:

  • Wakati Bodi ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Uingereza (BBBC) ikimfungia Hassan Mwakinyo kuzichapa nchini humo, chanzo cha msimamo huo kimetajwa kuwa ni kutokana na matukio mbalimbali ikiwamo ya ndani na nje ya ulingo.


Dar es Salaam. Wakati Bodi ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa Uingereza (BBBC) ikimfungia Hassan Mwakinyo kuzichapa nchini humo, chanzo cha msimamo huo kimetajwa kuwa ni kutokana na matukio mbalimbali ikiwamo ya ndani na nje ya ulingo.

Jana, mtandao wa ngumi za kulipwa wa Dunia (Boxrec) ulithibitisha bondia huyo namba moja nchini kufungiwa kwa muda usiojulikana kuzichapa nchini humo, ikiwa ni uamuzi wa BBBC.

Msimamo huo umekuja ikiwa ni siku 15 tangu bondia huyo alipochapwa na Liam Smith kwa Technical Knock Out (TKO) raundi ya nne ya pambano lililokuwa la raundi 12 lililopigwa mjini Liverpool.

“Kuna sababu nyingi, inaweza kuwa za ndani ya ulingo, hivyo wanakupumzisha kwa muda ili uimarike baada ya kupigwa KO (Knock Out) mbaya au vinginevyo,” alisema Emmanuel Mlundwa, bondia na mdau wa ndondi maarufu nchini na kuongeza.

“Sababu nyingine inaweza kuwa ya nje ya ulingo, labda kuna jinai umefanya, hicho ni kitu cha kawaida kwenye ngumi na ukifungiwa kwenye nchi moja unakwenda kupigana nchi nyingine, hakuna kinachokufunga,” alisema.

Hata hivyo, msimamo wa BBBC sasa huenda ukakwamisha pambano la marudiano la Smith na Mwakinyo kupigwa nchini humo kama litakuwepo Januari kama lilivyopangwa.

“Litakwenda kuchezwa kwenye nchi nyingine kama likiwepo, nje ya Uingereza na Marekani ambako Smith pia amefungiwa kupigana, licha ya kambi ya Mwakinyo kuwa nchini humo kwa zaidi ya miezi sita sasa.

Mwakinyo alipotafutwa jana kujua msimamo wake juu ya kifungo hicho, simu yake iliita bila kupokelewa, huku Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa akisisitiza kwamba kama Kamisheni inasubiri msimamo wa Serikali.

“Kama tutamchukulia hatua basi ni kutotumia kibali cha Tanzania kwenye pambano hilo, ishu ya matokeo hiyo ni ya Waingereza wenyewe, ingawa tayari tumeshapeleka maoni yetu kama ambavyo BMT ilitaka tufanye hivyo,” alisema Palasa.

Alisema Bodi ya Ngumi ya Uingereza ambayo ndiyo ilisimamia malipo ya pambano hilo ndiyo ya kumchukulia hatua kwenye suala la matokeo kwa kutomlipa.

“Kwenye matokeo katika ngumi za kulipwa ukidanganya kwa kujiangusha, adhabu yake ni kutolipwa au kupunguziwa malipo, hivyo hatujui kama kule alikuaje,” alisema.

Jana Mlundwa alisema kwenye ishu ya matokeo, kama alilipwa, maana yake waliona hilo si kosa, kama hakulipwa hiyo ndiyo adhabu yake tosha na mabondia wengi wamekumbana na ‘rungu’ hilo ikiwamo wa hapa nyumbani ambao aliwataja.

Mwakinyo alijibu kufungiwa kwake akiandika katika ukurasa wake wa Instagram akisema kufungiwa kwake ni kwa mujibu wa kanuni za BBBC, kwamba bondia anayepigwa kwa TKO anafungiwa kwa siku 45 hadi 60.