Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MZEE WA FACT: FIFA Series ituamshie mjadala wa Zanzibar

Beki wa Kulia wa Taifa Stars, Haji Mnoga wakati akijaribu kuwatoka wachezaji wa  Liechtenstein katika mechi ya kirafiki ya FIFA Series 2026 iliyofanyika katika Uwanja wa Pele, Kigali, Rwanda, Machi 26, 2026. Picha na Tanfootball

Tanzania imeshiriki mashindano ya FIFA Series yaliyofanyika Rwanda juma lililopita. Katika kundi lake, kulikuwa na timu mbili za taifa ambazo kimsingi sio za mataifa kamili.

Timu hizo ni Macau na Aruba. Japo sio mataifa kamili, lakini wameshiriki mashindano haya kwa sababu ni wanachama wa FIFA.

Hiki ndicho kimekuwa kilio cha Zanzibar kwa miaka mingi sasa. Zimefanyika jitihada mara kadhaa na mwanga ukaanza kuonekana.

Ilianza mwaka 2004 pale CAF walipoita Zanzibar uanachama kivuli, uliosaidia vilabu vyale kushiriki mashindano ya Afrika kutokea Zanzibar moja kwa moja.

Mwaka 2016 matumaini yakawa makubwa zaidi pale CAF ilipoipatia Zanzibar uanachama kamili.

Lakini haukudumu sana mabadiliko ndani ya uongozi wa CAF mwaka 2017 yakaja na viongozi wapya waliopindua maamuzi ya awali.

Kuanzia hapo ikaonekana kama haiwezekani tena kwa Zanzibar kupata uanachama wa FIFA.

Lakini ujio wa Macau na Aruba kwenye FIFA Series kutuamshie tena mapambano yale, kwa sababu Zanzibar inazo sifa zote zaidi Macau na Aruba.


MACAU

Ni sehemu ya nchi kubwa ya China. Macau kwa miaka mingi ilikuwa chini ya ukoloni wa Ureno hadi mwaka 1999 ilipokabidhiwa rasmi kwa China.

Lakini hata hivyo, ilipata uanachama wa FIFA tangu mwaka 1978 ikiwa bado koloni la Ureno.

FIFA waliipa Macau uanachama kwa sababu mwaka 1976 Ureno ilipitisha sheria ya kuipa nchi hiyo mamlaka ya utawala wa ndani (Organic Statute of Macau).

 Sababu nyingine ni kwamba walikuwa na chama chao cha mpira kilichoanzishwa mwaka 1938.


ARUBA

Aruba ni mwanachama wa FIFA tangu mwaka 1988. Lakini hata hivyo, hii sio nchi kamili...ni jimbo lenye utawala wa ndani wa nchi ha kifalme ya Uholanzi.

Ilipata utawala wake wa ndani tangu mwaka 1986. Aruba ambayo inapatikana Amerika ya kati, ni moja kati ya majimbo mengi ya Uholanzi katika eneo hilo yenye utawala wa ndani.

Mengine ni Curaçao na Sint Maarten. Katika majimbo haya, ni moja tu la Sint Maarten ndio halijapata uanachama wa FIFA. Curacao imeenda mbali zaidi hadi kufuzu kwa Kombe la Dunia lijalo, 2026.


KWANINI SIO ZANZIBAR

Nadhani FIFA wanatakiwa waulizwe maswali magumu zaidi safari hii, ilitolewa mifano timu hizi. Zanzibar ina chama chake cha soka ambacho mwaka huu, 2026 kinafikisha miaka 100, tangu kiundwe 1926.

Maana yake wana chama kikongwe kuliko hao wengine.  Wakati hao wengine ni majimbo tu, Zanzibar ni nchi yenye serikali yake imara na yenye madaraka yote ya ndani.

Mojawapo wa sifa za kuwa mwanachama wa FIFA ni kutambuliwa na mashirika ya umoja wa mataifa. Zanzibar inatambuliwa na mashirika kadhaa ambayo hadi yana ofisi zake visiwani.

Kifupi ni kwamba Zanzibar ina sifa sahihi zaidi kuwa mwanachama wa FIFA kuliko akina Macau na Aruba, tuliocheza nao pale Kigali.


WITO KWA SERIKALI YA MUUNGANO

Waziri mwenye dhamana ya michezo serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Paul Makonda, hebu livae hili. Kwa nchi yenye sifa kama Zanzibar, FIFA wananchotaka ni ridhaa ya serikali kuu.

Wewe kama waziri wa serikali kuu, simama imara paganism hili...nenda kathibitishe kwamba serikali kuu inaridhia Zanzibar kupata uanachama.

Ukweli ni kwamba japo harakati za Zanzibar kupata uanachama wa FIFA zilianza muda mrefu, lakini hakujawa na msukumo wa kutosha, ikiwemo hata kufungua kesi mahakama ya rufaa za michezo, CAS.

Gibraltar, ambayo ni nchi inayogombaniwa na Uingereza na Hispania, iliomba uanachama ikanyimwa kwa sababu kama za Zanzibar.

Wakaenda kufungua kesi CAS, wakashinda ma kupata uanachama wao. Kama FIFA hawataki kuelewa njia za kidiplomasia, sheria itumike..ikafunguliwe kesi CAS.


KWANINI MUHIMU ZANZIBAR KUPATA UANACHAMA FIFA?

Zanzibar kupata uanachama wa FIFA ni jambo lenye afya kubwa sana kwa Tanzania kama nchi kwa sababu tutakuwa na wigo mpana wa kuendeleza vijana wetu kama taifa.

Zanzibar itapata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, kama kufuzu Kombe la Dunia na AFCON, na kupata moja kwa moja mgao wa fedha, program za maendeleo ya ufundi na miundombinu kutoka FIFA.

Uanachama utaipatia ZFF (Zanzibar Football Federation) (ZFF) mamlaka kamili, uhuru na haki ya kupiga ndani ya FIFA na CAF, lakini kubwa zaidi ni uwezo wa kuibua vipaji na kuviweka kwenye soko la dunia.