Namba za ushiriki Kili Marathon kutolewa Mlimani City

Namba za ushiriki Kili Marathon kutolewa Mlimani City

Muktasari:

  • Katika taarifa iliyotoelwa jana na kamati ya maandalizi ya mbio hizo za kimataifa, zoezi hilo litafanyika katika sehemu ya maegesho ya magari katika viwanja vya Mlimani City, karibu na mgahawa wa Pizza Hut siku ya Jumamosi na Jumapili hii kuanzia saa sita mchana mpaka saa kumi na mbili jioni.

Dar es Salaam.  Waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2021 zitakazofanyika wiki ijayo mjini Moshi, Kilimanjaro wametangaza kituo kitakachotumika kuchukua  namba za ushiriki kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotoelwa jana na kamati ya maandalizi ya mbio hizo za kimataifa, zoezi hilo litafanyika katika sehemu ya maegesho ya magari katika viwanja vya Mlimani City, karibu na mgahawa wa Pizza Hut siku ya Jumamosi na Jumapili hii kuanzia saa sita mchana mpaka saa kumi na mbili jioni.

“Tunawaomba waliojisajili mbio ndefu za kilomita 42, mbio za nusu marathon za kilomita 21 za Tigo na zile za kujifurahisha za kilomita 5 za Grant Malt wafike Mlimani City wikiendi hii ili kupewa namba zao za ushiriki tayari kwa mbio hizo mkoani Kilimanjaro Februari 28,’ ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa waandaaji wa mbio hizo, washiriki watahitajika kubeba vitambulisho au hati ya kusafiria wakati wa zoezi  hilo lakini pia watahitajika kuonesha ujumbe wa uthibitisho waliopokea wakati wa kufanya malipo. Kwa wale wanaochukua namba za  makundi wanatakiwa kubeba nakala za vitambulisho vya washiriki watakaowachukulia na watahudumiwa katika meza ya makundi.

“ Tunawaomba wale watakaokwenda kuchukua namba kuzingatia muda kwa sababu zoezi litafanyika kwa siku mbili  kwa mkoa wa Dar es Salaam kabla ya zoezi hilo kuhamia kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na kufanyika tarehe 23 na 24 mwezi huu katika hoteli ya Kibo Palace na baadae kuhamia Moshi kwa siku tatu kuanzia tarehe 25, 26 na 27 katika hoteli ya Keys,” walisema waandaaji.

Walisema kuwa zoezi la kujiandikisha kwa mbio za kilomita 42 na zile za kilomita 5 kwa ajili ya kujifurahisha linaendelea katika vituo vya kuchukulia namba lakini litafanyika kwa malipo ya papo kwa papo lakini zoezi hilo limefungwa kwa wale wanaotaka kukimbia mbio za kilomita 21.

Wakati huo huo, waandaaji wamesema maandalizi yamekamilika na wanafanya kazi kwa karibu kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine muhimu kama vile Chama Cha  Riadha Tanzania (AT) katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa kabla, wakati wa mbio na baada ya mbio.

 “Tutaweka sehemu za kunawa mikono za kutosha na kutakuwepo na vitakasa mikono (sanitizer) pamoja na kutoa barakoa kwa washiriki katika vituo vya kutolea namba ambazo watatumia kabla ya kuanza mbio kisha watazivua wakati wanakimbia na kukabidhiwa nyingine wakati wanamaliza mbio katika viwanja vya Chuo Kikuu Cha Ushirika (MoCU) ili wazivae pale uwanjani,” ilisema taarifa hiyo.

Mbio za mwaka huu zimedhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager-kwa upande wa mbio ndefu za kilomita 42km, Tigo wamedhamini mbio za kilomita 21km (Half Marathon) wakati Grand Malt wamedhamini mbio za kilomita 5km.