Neymar aipa imani Brazil akirejea mazoezini
Nyota wa timu ya Taifa ya Beazil, Neymar. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Neymar ameitwa baada ya kukaa nje kwa zaidi ya miaka miwili kwani mara ya mwisho aliitumikia timu ya Taifa ya Brazil, Oktoba 18, 2023.
Kocha Mkuu wa Brazil, Carlo Ancelotti, bado ana matumaini kuwa nyota wa timu hiyo, Neymar, atapona majeraha ya misuli ya mguu wa nyuma na hivyo atakuwa tayari kushiriki Kombe la Dunia 2026.
Ancelotti amethibitisha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34 anaendelea vizuri katika programu yake binafsi ya mazoezi ya kupona na atafanyiwa uchunguzi muhimu wa MRI leo kabla ya uwezekano wa kurejea kwenye mazoezi ya pamoja na kikosi wiki ijayo.
Meneja huyo wa zamani wa Real Madrid na AC Milan, alieleza kuwa Neymar atalazimika kukamilisha hatua zote za kitabibu kabla ya kuruhusiwa kushiriki mazoezi yenye mgusano wa moja kwa moja.
"Nadhani hali yake iko wazi kabisa. Neymar anaendelea vizuri sana na mazoezi yake binafsi. Baada ya wikiendi atafanyiwa uchunguzi wa MRI, na ikiwa kila kitu kitaenda vizuri, ataweza kufanya mazoezi na kikosi wiki ijayo," alisema Ancelotti.
Brazil itaanza kuwania Kombe la Dunia kwa kuikabili Morocco, Juni 14 na kisha Juni 20 itacheza na Haiti na Juni 25 itamalizia mechi za kundi lake kwa kukabiliana na Scotland.
Ikiwa Neymar atashindwa kupona kabla ya wakati, huenda Ancelotti akakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wadau wa soka na mashabiki wa timu yake ya taifa kwani wengi walionekana kushangazwa na uamuzi wa kumuita kikosini.
Neymar ameitwa baada ya kukaa nje kwa zaidi ya miaka miwili kwani mara ya mwisho aliitumikia timu ya Taifa ya Brazil, Oktoba 18, 2023.