Ni Fei Toto tu, Nabi amzuia Yanga

WAKATI Yanga wakiwa mkoani Lindi kuvaana na Namungo kesho, takwimu zinaonyesha kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni mwamba haswa Ligi Kuu msimu huu katika chama lake akiliokoa katika nyakati ngumu.

Juzi, Fei aliifungia Yanga bao pekee katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kuirejesha kileleni.

Timu hiyo imecheza michezo 14, ikiwa imeshinda 11, imetoka sare michezo miwili na kupoteza mmoja ikiwa kileleni na pointi 35.

Fei ambaye anatajwa kati ya wachezaji bora zaidi nchini kwa sasa alifanikiwa kufunga bao hilo katika dakika ya 89, lakini takwimu zinaonyesha kuwa amekuwa mwamba kwa mabao ya dakika hizo ambayo yamekuwa yakiipa timu hiyo ushindi katika mechi husika.

Mabao matano ambayo amefunga kwenye ligi msimu huu dhidi ya Ruvu Shooting, KMC, Prisons na mawili dhidi ya Azam yameonekana kuwa ya jioni na timu hiyo kupata ushindi.

Kwenye mchezo dhidi ya KMC Oktoba 26, Yanga ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0, ambapo Fei alifunga katika dakika ya 80 ya mchezo kwa shuti kali la mguu wa kushoto.

Katika mchezo mwingine wa ligi Oktoba 3, Fei aliifungia Yanga bao la kwanza katika dakika ya 52 kwa kichwa walipopata ushindi wa mabao 2-1.

Septemba 6, Fei alionyesha umwamba wake tena wakati Yanga ilipopata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam ambapo alifunga bao la kwanza dakika ya 57 kwa shuti kali la mguu wa kulia, huku akifunga la pili dakika ya 76 kwa shuti kali tena la mguu wa kulia.

Mbali na hayo ya ligi pia alifanikiwa kufunga bao la kusawazisha kwenye mchezo wa Kombe Mapinduzi mwanzoni mwa mwaka huu walipopata sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKU.

Akizungumzia mabao hayo, Fei alisema ni jambo ambalo amekuwa akilifanyia kazi mazoezini ndiyo maana amekuwa hana wasiwasi anaposhindwa kufunga nje ya 18 kwani huingia ndani ya boksi na kujaribu kufunga.

“Ukiangalia mechi ya Prisons nilikuwa napiga mashuti nje ya boksi sikufanikiwa kufunga. Baada ya kuingia ndani ya boksi nilifunga si bahati mbaya bali nafanyia kazi mazoezini na hata nikiwa kwenye mazoezi yangu binafsi,” alisema Fei Toto.

“Tunahitaji kufanya vizuri kwenye mchezo wa Namungo ili kupata pointi tatu kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi tukiwa tumewaacha wapinzani wetu kwa pointi na si mabao ya kufunga na kufungwa.

“Kocha Nasreddine Nabi hakuwepo kwenye benchi ila tulikuwa naye kwenye mazoezi alituelekeza vingi vya kufanya kwenye mechi hiyo akishirikiana na Cedrick Kaze hadi kufanikiwa kufanya vizuri.

“Naamini hata kwenye mchezo wa Namungo itakuwa hivyo licha ya ugumu ambao nafahamu tutakutana nao, ila tutashinda na kupata pointi tatu kama malengo yetu yaliyotuleta huku Lindi yalivyo.”

Bao alilofunga Fei Toto kwenye mechi ya Tanzania Prisons linakuwa la tano kwake msimu huu.


MOLOKO FRESHI

Kwenye hatua nyingine winga Jesus Moloko hakufanya mazoezi na kikosi tangu alivyoumia kwenye mechi dhidi ya Ihefu na alishindwa kucheza mchezo uliopita dhidi ya Prisons.

Moloko alisema alikuwa anasumbuliwa na enka hadi kuvimba mguu wa kulia, ila baada ya kupata matibabu anaendelea vizuri na amesafiri na timu kwa ajili ya mchezo na Namungo.

“Nipo freshi kabisa sasa hivi sina shida yoyote wala maumivu. Nataka kurudi kuipigania timu yangu kufanya vizuri kwenye mchezo huo ili kupata ushindi,” alisema Moloko ambaye kiwango chake kimekuwa kikiimarika siku hadi siku.