Okwi, Okwi, Okwi!

“Nimejiunga na Simba ili kulinda kipaji changu kisishuke kwani ningechelewa kusaini Simba ningekosa mahali pa kwenda kucheza kutokana na muda wa usajili kumalizika. Hata wao Yanga walinichukua SC Villa ambako nilikuwa nacheza baada ya kupata matatizo Tunisia.”Okwi
.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
Klabu za Simba na Yanga zipo katika mgogoro wa kumgombania mshambuliaji Emmanuel Okwi.
Dar es Salaam. Mshambuliaji Emmanuel Okwi anaweza akafungiwa kucheza soka na hivyo kushindwa kuitumikia Simba aliyojiunga nayo hivi karibuni kutokana na kukiuka kanuni ya 13 ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Kwa mujibu wa kanuni hiyo inayozungumzia masuala ya usajili, mkataba kati ya mchezaji na klabu yake unaweza kuvunjwa kama mkataba umemalizika au pande hizo mbili zimeafikiana kuuvunja. Okwi, ambaye ana mkataba wa miaka miwili na Yanga hajafanya yote hayo.
Hata hivyo, Yanga nayo inaweza kupoteza haki zake kwa vile kati ya barua ambazo wameziandika TFF kuhusu mshambuliaji huyo kuna barua ambayo wametaka kuvunja mkataba na Okwi bila ya kumlipa fidia yoyote na badala yake wamemtaka Okwi arudishe fedha zote za usajili ambazo amechukua, kurejesha mishahara ambayo amechukua na kuilipa Yanga fidia ya Dola za
Kimarekani 200,000 (zaidi ya Sh 340,000 milioni) kwa madai amewatia hasara ikiwa pamoja na kuwakosesha ubingwa.
Klabu hiyo ya Jangwani pia katika barua hiyo imeomba mchezaji huyo na wakala wake Edgar Agaba ambaye pia ni mwanasheria wafungiwe kujihusisha na masuala ya soka nchini, kwa sababu walikwishaingia kwenye mazungumzo na klabu ya Wadi Galde ya Misri wakati bado Okwi akiwa na mkataba na Yanga.
Kwa upande wa Simba na wenyewe wanaweza kukosa huduma ya mshambuliaji huyo kwa sababu viongozi wake walimtangaza Okwi kuwa ni mchezaji wao kinyume cha taratibu, kwa kuwa ili mchezaji aweze kutoka klabu moja kwenda nyingine lazima apitie katika mfumo wa Teknolojia ya Uhamisho wa Wachezaji kwa Kompyuta (TMS) kwa makubalino ya klabu mbili, anayotoka mchezaji na ile anayokwenda.
Yanga walipotaka kumsajili Okwi walikubaliana na SC Villa ambayo ilikuwa na mkataba wa miezi sita na mchezaji huyo ambaye aliingia kwenye mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Kutokana na mgogoro na klabu yake ya Tunisia ilibidi Shirikisho la Soka Uganda (Fufa), liombe kibali maalumu Fifa ili mchezaji huyo aweze kulinda kipaji chake wakati mgogoro wake na Etoile du Sahel ukiwa unatafutiwa ufumbuzi hata hivyo baada ya miezi mitatu Okwi alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili na nusu ambao utakwisha mwaka 2016.
Hoja za Okwi
Katika moja ya hoja za Okwi alisema: “Nimejiunga na Simba ili kulinda kipaji changu kisishuke kwani ningechelewa kusaini Simba ningekosa mahali pa kwenda kucheza kutokana na muda wa usajili kumalizika. Hata wao Yanga walinichukua SC Villa ambako nilikuwa nacheza baada ya kupata matatizo Tunisia.
“Nisingeenda SC Villa sidhani kama Yanga wangenichukua bila mimi kutokuwa na timu yoyote, hivyo hili ni suala linalokubalika mahali popote duniani,” alisema Okwi.
Kwa upande wa Simba, hoja ambayo wanaitoa kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope ni kwamba Okwi aliomba kujiunga na timu hiyo mwenyewe baada ya kuelezwa kuvunjwa kwa mkataba wake na Yanga.
“Mbinu walizotumia Yanga kumsajili Okwi wakati ana mgogoro wake na Etoile du Sahel ya Tunisia ndiyo hizo hizo tulizotumia kumrejesha Simba. Walivyowafanyia Tunisia wakati wana mgogoro na Okwi walijiona washindi sasa na sisi kwa mantiki hiyo hiyo tumeamua kumrudisha kundini, kwani wakati wao wanamsajili hawakujua kuwa Okwi ana mkataba na Etoile du Sahel hadi 2015?” alihoji Hans Pope.
Kamati ya sheria ya TFF
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ndiyo itakayotoa uamuzi wa suala hilo la Okwi na Simba na Yanga katika kikao chao kitakachokaa kuanzia Septemba 6 hadi 8. Kamati hiyo inayoongozwa na Richard Sinamtwa, Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Zacharia Hanspoppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega kama itafuata sheria, Simba na Yanga zitakutwa na makosa, lakini kama wataenda kwenye utaratibu wa kupiga kura basi kuna klabu moja kati ya hizo itashinda kwa vile kamati hiyo inaundwa na watu wengi walio mashabiki wa timu moja kati ya hizo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alishawahi kusema TFF bado inatambua mkataba wa Okwi na Yanga na kwamba hakuna nyaraka yoyote ya kuvunja mkataba kati ya Yanga na Okwi.
“Tumeshawaandikia Yanga barua kuwaita kwenye shauri hili, madai yaliyopo mpaka sasa ni Yanga kumlalamikia Okwi kushindwa kuripoti kwenye klabu yake, hakuna madai yoyote ya Okwi kuwa anaidai Yanga,”alisema Mwesigwa.
Naye katibu wa zamani wa TFF Frederick Mwakalebela alisema, “Kamati ya sheria ya TFF inapaswa kufanya uamuzi ambao hautakuwa na fikra za upendeleo kwani kanuni zipo.”
Alisema kama Yanga itabainika ilivunja sheria kwa kutomlipa mchezaji huyo au Simba kumsajili wakati bado ana mkataba na timu nyingine kama ambavyo sheria inasema viongozi waliohusika kufanya ubabaishaji huo nao wawajibishwe na si kuangaliwa mchezaji peke yake.
Wakati Mwakalebela akisema hayo, katibu mwingine wa zamani wa TFF, Angetile Osiah naye alisema,”Nawashauri viongozi wa Simba na Yanga kuamua kuyamaliza bila kufikishana mbali. Migogoro kwenye soka haijengi, hakuna sababu ya kuvutana kisa mchezaji, mbona wapo wachezaji wengi wazuri zaidi ya huyo? Cha msingi wakubali kukaa meza moja wayamalize.”