Onana kurejea Man United mshahara wake ukiongezeka
Golikipa wa Man United, Andre Onana, anaripotiwa kurejea Old Trafford baada ya msimu kumalizika akitokea Trabzonspor alipokuwa kwa mkopo. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kipa huyo anaripotiwa kurejea Old Trafford baada ya msimu kumalizika akitokea Trabzonspor alipokuwa kwa mkopo huku mshahara wake ukitarajia kuongezeka iwapo United itafuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Manchester, England. Klabu ya Manchester United inakabiliwa na changamoto juu ya mustakabali wa kipa wake Andre Onana, kufuatia uwezekano wa mshahara wake kupanda endapo timu hiyo itafanikiwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kwa mujibu wa taarifa, Onana alijiunga na klabu ya Trabzonspor kwa mkopo wa msimu mmoja mwezi Septemba, lakini mkataba huo hauna kipengele cha kununuliwa moja kwa moja. Hivyo, anatarajiwa kurejea Old Trafford mwishoni mwa msimu huu.
Inaelezwa kuwa makubaliano ya mkopo huo yaliwezeshwa na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa mshahara wa Onana, baada ya United kushindwa kufuzu mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2025-26.
Hata hivyo, chini ya kocha Michael Carrick, United kwa sasa wanashika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England na wako kwenye nafasi nzuri ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Hali hiyo inamaanisha mshahara wa Onana unaweza kurejea katika kiwango chake cha awali.
Vyanzo kutoka ndani ya Klabu vinaeleza kuwa hali hiyo inaleta wasiwasi ndani ya klabu, kwani ongezeko hilo la mshahara linaweza kupunguza uwezekano wa klabu nyingine kuvutiwa kumsajili kipa huyo mwenye umri wa miaka 29.
Hivyo, United wanaweza kujikuta wakilazimika kulipia sehemu ya mshahara wake iwapo watataka kumuuza au kumtoa kwa mkopo tena.
Onana bado ana miaka miwili katika mkataba wake aliosaini mwaka 2023 alipohamia United akitokea Inter Milan chini ya kocha wa zamani Erik ten Hag.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa watu wa karibu na kipa huyo zinaeleza kuwa anapendelea kurejea United kwa maandalizi ya msimu mpya na kupigania nafasi yake kikosini.
Wakati huo huo, klabu hiyo imefurahishwa na kiwango cha kipa mpya Senne Lammens aliyesajiliwa kutoka Royal Antwerp, na anatarajiwa kuwa kipa namba moja msimu ujao.
United pia wanaweza kutafuta kipa mwingine iwapo kipa namba mbili, Altay Bayındır ataondoka. Kipa huyo alikuwa akiwaniwa na Beşiktaş mwezi Januari, akitaka kupata muda zaidi wa kucheza ili kuongeza nafasi ya kuitwa timu ya taifa ya Uturuki kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Kwa upande wa kipa namba tatu, Tom Heaton, ambaye ana umri wa miaka 39, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwezi Juni baada ya kuongeza mwaka mmoja msimu uliopita.