Pamba ina jambo na Simba

Saturday May 14 2022
pamba pic
By Ramadhan Hassan

BAADA ya miaka 20 tangu Pamba FC (Tout Poisssant Lindanda) ya Mwanza iliposhuka Ligi Kuu, leo itaingia kwa Mkapa kucheza mechi ya mashindano tena dhidi ya Simba katika Kombe la Azam huku ikipanga kuwatibulia mabingwa watetezi hao wa ASFC.

Timu hizo mbili hazijakutana kwenye mechi ya kimashindano ndani ya miaka 20 iliyopita na inatarajiwa kuwa mechi ya kihistoria kwao kutokana na rekodi zao za miaka ya nyuma.

Pamba imepanga kuitibulia Simba kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa kushinda mechi hiyo huku ikiwa na kumbukumbu ya timu za Mashujaa na Green Warriors zilizoiondosha Simba kwenye michuano hiyo mwaka 2017 na 2018.

Licha ya Simba kuwa imara lakini timu hizo za majeshi (Mashujaa na Green) ziliifumua na kuiondoa mapema kwenye michuano ya ASFC hatua ya 64 bora ambapo Mashujaa ikiwa Daraja la Kwanza kwa sasa Championship ilishinda 3-2 mwaka 2018 na kusonga mbele huku Green ikiwa daraja la pili kwa sasa First League mwaka 2017 iliiondosha Simba kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 jambo linaloipa Pamba imani ya kufanya hivyo.

Ili kuhakikisha hilo linatokea Pamba ipo Dar es Salaam tangu Mei 5 mwaka huu, na baada ya kucheza mechi ya Championship Mei 8 ikapoteza dhidi ya DTB imeendelea kujifua kwenye Uwanja wa Azam Complex kwaajili ya mechi na Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Mkuu wa Pamba Wilbert Mweta alieleza lengo lao kuu ni kutinga nusu fainali hivyo lazima waifunge Simba ili kufanya hivyo.

Advertisement

“Hii ni mechi ya mtoano hivyo lazima tushinde, tunaendelea vyema na mazoezi na tutaingia kwenye mchezo huo kucheza kwa nidhamu zaidi ili kuhakikisha tunashinda na kusonga mbele.

“Tunajua Simba ni timu bora pia bingwa mtetezi wa michuano hii lakini tunaamini tutafanya vizuri dhidi yao,” alisema Mweta.

Mshindi wa mechi hiyo, ataivaa Yanga nusu fainali.

Advertisement