Penalti ya Yanga yamponza refa, TPLB yavuna mamilioni
Muktasari:
- Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu ina jukumu la kusimamia uendeshaji/mwenendo wa michezo na matukio katika Ligi Kuu pamoja na Usimamizi wa Kanuni za Ligi Kuu.
Dar es Salaam. Wakati Refa Ahmada Simba akifungiwa kwa michezo mitano kutokana na kosa la kuipa Yanga penalti isiyostahili dhidi ya Fountain Gate, Kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendsshaji wa Ligi Kuu Tanzania kilichoketi Desemba 5, mwaka huu, kitaifanya Bodi ya Ligi Kuu kuvuna kiasi cha Sh27 milioni.
“Kamati imeridhia kuwa mwamuzi hakutafsiri vyema sheria husika na amepisha uamuzi uliokuwa na athari moja kwa moja kwenye matokeo ya mchezo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mbali na adhabu hiyo kwa Refa Simba, Kamishina wa mechi hiyo, Rehule Nyaulawa naye amesimamishwa kwa muda wa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kutoa taarifa kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuhusiana na mapungufu ya mwamuzi wa mchezo huo katika kutafsiri sheria za mpira wa miguu.
Katika hatua nyingine, kikao hicho cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, kimetoza faini za kiasi cha Sh27 milioni kutokana na makosa mbalimbali.
Fedha hizo ni faini kwa timu, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi ambao wamefanya makosa katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu, Ligi ya Championship na First League ambazo zilifuatiliwa na kutolewa uamuzi na kikao cha kamati hiyo.
Kwa mujibu swa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo, Desemba 8, 2025, adhabu zilizotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi zimehusu pia vifungo na onyo kwa timu au watu waliofanya makosa kwa mujibu wa kanuni.
Mchezo namba 058 uliochezwa Novemba 30, 2025 baina ya Mbeya City na Bodi ndio umeongoza kwa kiwango kikubwa cha faini ambapo wenyewe pekee utaipa Bodi ya Ligi Kuu kiasi cha Sh6 milioni.
"Klabu ya Namungo ya mkoani Lindi imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la wachezaji wake kuonekana wakimwaga kiwanjani vitu visivyofahamika, wakati wachezaji wa timu hiyo wakipasha moto misuli, jambo lililotafsiriwa kama kitendo kinachoashiria imani za kishirikina. Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
"Mchezaji Gabriel Daud Mwaipola wa klabu ya Mbeya City ya mkoani Mbeya amefungiwa michezo mitano (5) na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la kumpiga ngumi mchezaji Rajabu Abdallah Mfuko wa klabu ya Namungo wakati wa mchezo tajwahapo juu.
"Mwamuzi wa kati wa mchezo tajwa hapo juu, Ahmada Simba kutoka Kagera ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu ambapo mwamuzi huyo alitoa adhabu ya penati kwa klabu ya Fountain Gate katika tukio ambalo mlinzi wa timu hiyo hakuwa ameushika mpira huo," imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.