Pointi tatu kuirudisha Geita Ligi Kuu
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha Geita Gold FC wakishangilia moja ya ushindi katika Ligi ya Championship. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Ukiondoa mechi hiyo, kutakuwa na michezo mingine saba ambayo yote itaanza saa 10:00 jioni katika viwanja na miji tofauti.
Dar es Salaam. Ushindi wa aina yoyote wa Geita Gold ikiwa nyumbani leo dhidi ya Songea United utaifanya irejee katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kucheza katika Ligi ya Championship kwa misimu mmoja.
Ikiwa itaondoka na pointi tatu katika mechi hiyo ya leo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu kuanzia saa 10:00 jioni, Geita Gold itafikisha pointi 71 ambazo zitaihakikishia kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye Ligi ya Championship na kupanda Ligi Kuu.
Matokeo yakiwa hivyo, ni timu moja tu ambayo itaweza kuzifikia pointi hizo za Geita Gold ambayo ni Kagera Sugar iliyopo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 65 kwani Polisi Tanzania iliyo katika nafasi ya tatu itamaliza na pointi 69 tu iwapo itapata ushindi katika mechi zake tatu ilizobakiza.
Kiungo mkabaji wa Geita Gold FC, Isaya Kuzoza wakati akiwa katika moja ya mechi za Ligi ya Championship.
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zuberi Katwila amesema kuwa amewaandaa vizuri wachezaji wake kimbinu na kisaikolojia ili waweze kupata matokeo mazuri yatakayowavusha kwenda Ligi Kuu.
"Mchezo utakuwa wa ushindani. Sisi mechi zote tuanzocheza ni ngumu. Vijana tumewaandaa kisaikolojia. Lazima wapambane kwa kila hali ili tuweze kupata ushindi. Mashabiki waje kutusapoti, sisi tutajitahidi kuwapa wanachohitaji.
"Ni mpango ambao tulikuwa tumeuweka msimu huu. Viongozi na wadau wote tulikuwa pamoja kukamilisha huu mpango. Mchezo huu ni muhimu kwa sababu ndio utakaotufungulia mlango ambao tulikuwa tunagonga hodi kwa maana ya kupanda Ligi Kuu," alisema Katwila.
Baadhi ya wachezaji wa Geita Gold FC, wakishangilia moja ya ushindi katika moja ya mechi za Ligi ya Championship.
Ukiondoa mechi hiyo, kutakuwa na michezo mingine saba ambayo yote itaanza saa 10:00 jioni katika viwanja na miji tofauti.
Kagera Sura itaikaribisha Kengold katika Uwanja wa Kaitaba, Kagera na katika Uwanja wa Ilulu, Lindi, Bigman itakuwa mwenyeji wa Gunners na kule kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, Mbeya Kwanza itaumana na Stand United.
Barberian itacheza na B19 katika Uwanja wa Filbert Bayi, Pwani, Hausung itakuwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Amani, Njombe kucheza na Transit Camp, Mbuni itaikaribisha Polisi Tanzania katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na TMA itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Black Rhino kucheza na African Sports.