Porter atimuliwa West Ham, Santo kumrithi
Muktasari:
- West Ham United inashika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England (EPL) ikiwa na pointi tatu ilizokusanya katika mechi tano.
London. Graham Porter amekuwa meneja wa pili kutimuliwa katika Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya West Ham United leo Jumamosi, Septemba 27, 2025 kuamua kuvunja mkataba naye.
Kabla ya Porter, kocha wa kwanza kuvunjiwa mkataba alikuwa ni Nuno Espirito Santo ambaye alifungashwa virago na Nottingham Forest, Septemba 9, mwaka huu.
Kutimuliwa kwa Porter kumetokana na muendelezo wa matokeo mabaya ambao timu hiyo imekuwa nayo katika EPL msimu huu kama taarifa ya QWest Ham ilivyofafanua.
"Matokeo na kiwango cha mzunguko wa pili wa msimu uliopita na mwanzoni mwa msimu wa 2025/2026 haviendani na matarajio na Bodi ya Wakurugenzi inaamini mabadiliko ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya timu katika ligi haraka iwezekanavyo.
"Klabu inathibitisha kwamba Kocha Msaidizi Bruno Saltor, Makocha wa Kikosi cha Kwanza, Billy Reid na Narcis Pelach, Kocha Kiongozi wa Makipa, Casper Ankergren na Kocha wa Makipa, Linus Kandolin wameondoka pia.
"Bodi inapenda kumshukuru Graham na benchi lake la ufundi kwa kazi nzito wakati wao wakiwa na Wagonga Nyundo na tunawatakia mafanikio kwa siku za usoni," imesema taarifa ya West Ham United.
Kwa mujibu wa taarifa ya West, Klabu hiyo imepanga kumtangaza na kumpata meneja mpya haraka iwezekanavyo kabla ya mchezo wake dhidi ya Everton kesho Jumapili.
Inaripotiwa kwamba timu hiyo ipo katika hatua za mwisho kumalizana na Santo kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Porter ambaye amewahi kuinoa Chelsea.