Rashford kubaki Barcelona bado pagumu
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alijiunga na klabu hiyo ya Hispania dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa mkopo wa msimu mmoja.
Barcelona, Hispania. Barcelona imeshafanya uamuzi wao juu ya hatma ya mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford anayecheza kwa mkopo katika kikosi chao.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alijiunga na klabu hiyo ya Hispania dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa mkopo wa msimu mmoja.
Tangu atue Rashford ameonyesha kiwango bora, akifunga mabao matatu na kutoa pasi tano za mabao katika mechi 10 alizocheza hadi sasa.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Hispania, klabu hiyo yenye maskani yake huko Catalonia iko tayari kutumia kipengele kilichopo katika mkataba wake kinachowapa nafasi ya kumnunua mazima ikiwa watahitaji.
Hata hivyo, dau la Pauni 26 milioni linalohitajika ili kufanikisha hilo linaonekana kuwa kubwa kwa Barca kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Barca ipo katika hali ngumu kifedha ambayo inawazuia kusajili wachezaji kwa uhuru, kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Hali hiyo imesababishwa na sheria ngumu za La Liga kuhusu usawa wa kifedha ambazo zinaeleza timu haitakiwi kutumia zaidi ya kile inachoingiza.
Ili kukamilisha dili hilo kwanza, Rashford huenda akalazimika kukubali kupunguzwa mshahara wake wa Pauni 325,000 kwa wiki, pia taarifa kutoka tovuti ya Tribal Football, inaeleza kwamba Barca inaweza kujaribu kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Manchester United, kuona kama inaweza kupunguziwa bei.
Ikiwa hatua hizo zote zitafeli, Barca inaweza kuomba tena kumpata Rashford kwa mkopo wakati ikijiweka sawa kimahesabu ili kumnunua baadae.
Staa huyu ana mkataba na Man United hadi mwaka 2028, jambo linaloifanya timu hiyo kutaka kiasi chochote inachohitaji kwa sababu mkataba bado ni mrefu.