Prime
Saa 48 za uamuzi mzito Yanga, Kocha atoa neno
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves. Picha na Yanga
Jana Machi 22, 2026 na leo Jumatatu, Machi 23, 2026, mabosi wa Yanga wamekuwa na muendelezo wa vikao ambavyo vinalenga kujadili mustakabali wa timu hiyo hasa wa miezi ya hivi karibuni.
Vikao hivyo huenda visimalizike vyema kwa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mreno, Pedro Goncalves ambapo habari kutoka chanzo cha ndani ya timu hiyo, zinafichua kwamba huenda kuna vichwa vikaondolewa katika benchi hilo ili kupisha ujio wa wengine.
"Mtu sahihi wa kutupa kwanza majibu ya kwa nini timu yetu imefika hapa ni kocha. Tutakutana naye lakini kwanza sisi wenyewe tutatangulia kukutana kwanza leo (jana Jumapili). Tutajadili kuhusu hili.
"Baadaye ndio tutakutana na huyu Kocha tumsikilize. Unajua ni kweli kwamba timu yetu imeshuka sana. Yanga haitakiwi kuzoeleka hivi na tukisema tubaki kuangalia tunaweza kupotea zaidi. Kwenye haya mapumziko ya mechi za FIFA, tunataka kubadilisha mambo," kilifichua chanzo ndanii ya Yanga kikizungumza na Mwanaspoti.
Hata hivyo wakati benchi la ufundi la Yanga likiwekwa kikaangoni, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mathew Silva amewataka mashabiki na wapenzi wake kuwa na subira na uvumilivu huku akiahidi mambo yatakaa sawa.
"Tupo juu ya msimamo na tunaendelea kufanya kazi kwa unyenyekevu, bidii na kujitolea kila siku. Ni heshima kubwa kuitumikia klabu hii.
"Hatua kwa hatua. Siku baada ya siku. Mechi baada ya mechi. Mafanikio hujengwa kwa uvumilivu. Roma haikujengwa kwa siku moja. Nasi tunaendelea kujenga kitu kikubwa," amesema Silva.
Yanga haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo zilizopita za Ligi Kuu.
Mechi hizo ni mbili dhidi ya Azam na TRA United ambazo ilipata matokeo ya sare tasa na dhidi ya Mtibwa Sugar ambao imepata sare ya bao 1-1.