Sababu ya Benitez kutimuliwa Celta
Muktasari:
- Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Liverpool, Chelsea na Newcastle alikabidhiwa mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya La Liga, Juni mwaka jana, aliporejea mzigoni baada ya kukosa kazi kwa miezi 18 tangu alipopigwa kibuti huko Everton.
Celta Vigo imemfuta kazi kocha Rafael Benitez baada ya timu hiyo kupata matokeo ya mabaya uwanjani.
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Liverpool, Chelsea na Newcastle alikabidhiwa mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya La Liga, Juni mwaka jana, aliporejea mzigoni baada ya kukosa kazi kwa miezi 18 tangu alipopigwa kibuti huko Everton.
Hata hivyo, Benitez amekuwa na wakati mgumu kwenye kikosi cha Celta, ambapo siku za karibuni alishinda mechi moja tu kati ya tano za mwisho.
Kwa kipindi chake alichokuwa Celta, Benitez ameshinda mechi tisa tu kati ya 33 na kuiweka timu hiyo kwenye nafasi yenye hatari ya kutumbukia kwenye timu zinazoweza kushuka daraja.
Celta inashika nafasi ya 17 baada ya kushinda mechi tano na sare tisa katika mechi 28, pointi mbili juu ya timu inayoshika nafasi ya 18, Cadiz.
Kutokana na hilo, Celta imeamua kumfuta kazi Benitez kutokana na matokeo yasiyofurahisha. Mchezo wao ujao watakwenda ugenini kukipiga na Sevilla wikiendi hii na itakuwa mechi muhimu katika vita yao ya kupambana kuhakikisha wanabaki kwenye La Liga msimu ujao.
Taarifa ya klabu hiyo ilisomeka:"Rafa Benitez na benchi lake la ufundi litaondoka RC Celta baada ya miezi minane ya kupambana na kujitolea kazini, lakini timu imekuwa haipati matokeo mazuri.
"Klabu inapenda kumshukuru Rafa Benítez na wasaidizi wake kwa kuonyesha kufanya kazi bila ya kuchoka. RC Celta inamtakia kila la heri na mafanikio kwenye majukumu yake mengine."
Benitez mechi yake ya mwisho Celta alishuhudia akichapwa 4-0 na Real Madrid, Jumapili iliyopita.