Safari ya Yanga huru kiuchumi

Safari ya Yanga huru kiuchumi

Muktasari:

  • Kutoka kutegemea ‘kutembeza bakuli’ kwa mashabiki wake miaka miwili iliyopita, Klabu ya Yanga imejiwekea mkakati wa kuwa na mapato ya uhakika yatakayoiongezea ushindani na kukaribisha uwekezaji wenye tija zaidi kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.


Kutoka kutegemea ‘kutembeza bakuli’ kwa mashabiki wake miaka miwili iliyopita, Klabu ya Yanga imejiwekea mkakati wa kuwa na mapato ya uhakika yatakayoiongezea ushindani na kukaribisha uwekezaji wenye tija zaidi kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Kwa msimu wa mwaka 2019 Yanga iliingiza zaidi ya Sh4.68 bilioni, lakini kiasi kikubwa zaidi kilitokana na michango ya wanachama na mashabiki wake waliotoa zaidi ya Sh21.07 bilioni ambazo ziliongezeka mpaka Sh1.64 bilioni mwaka 2020 klabu hiyo ilipoingiza Sh5.85 bilioni. Hata hivyo, nidhamu ya matumizi ilikuwa kubwa ndani ya klabu hiyo, kwani kwa miaka yote miwili walibakiwa na ziada.

Mwaka 2019 ilitumia Sh4.67 bilioni, hivyo kubakiwa na akiba ya Sh5.2 milioni na mwaka 2020 ikatumia Sh5.73 bilioni na kubakiwa na Sh126.41 milioni. Katika msimu ujao (2021/22), klabu hiyo imepanga kuingiza Sh8.14 bilioni ambazo kiasi kikubwa kitatumika kulipa mishahara ya wachezaji iliyoongezeka takriban mara tatu ya iliyolipwa mwaka huu.

Yanga imepanga kutumia Sh4.9 bilioni kulipa mishahara kutoka Sh1.96 bilioni ilizolipa msimu huu au Sh1.61 bilioni ilizowalipa msimu uliopita. Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 304 ndani ya misimu hii mitatu.

Bajeti itakayotumika kuboresha utendaji na uendeshaji wa klabu hiyo ya Mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam (Sh8.14 bilioni) zinakusudiwa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali, ukiwamo udhamini Sh4.23 bilioni, ada za wanachama Sh2.04 bilioni, mitandao ya kijamii Sh960 milioni, viingilio vya mechi Sh565 milioni na uuzaji wa vifaa vya michezo Sh350 milioni.

Kwenye mkakati wao, Yanga hawajapanga kuwaomba tena wadau wao isipokuwa wameweka mpango imara utakaowaingizia mapato ya uhakika ili kuwapa raha mashabiki wao ndani na nje ya nje.

Klabu hiyo imepanga kusajili walau wanachama 50,000 watakaolipa ada ya mwaka kwenye kanzidata yake ili kuingiza Sh1.2 bilioni pamoja na mashabiki 70,000 watakaolipa Sh800 milioni. Timu hiyo pia itaboresha programu yake (app) ili kuwavutia wengi zaidi. Inapanga kwamba, ikipata watumiaji wasiopungua 40,000 kila mwezi basi itajiingizia Sh960 milioni.

Kwa kuiweka bajeti yake wazi, Audax Kamala anasema “kunaondoa ubabaishaji na kujenga imani ya mashabiki huku viongozi wakitakiwa kuwajibika kwa walichokiahidi. Itasaidia kuvutia uwekezaji na kuongeza morali wa wachezaji, hasa wa kimataifa kujiunga na klabu.”

Kamala, ambaye ni mhasibu (CPA) anasema ili mtu afanye uamuzi makini wa uwekezaji, anahitaji kuona namba ambazo zinapatikana kwa taarifa zilizo wazi. “Iwapo klabu zetu zitajenga utamaduni wa kuchapisha taarifa zao za fedha, soka la Tanzania litabadilika na kukua,” anasema mhasibu huyo.

Bajeti inaonyesha Yanga itatumia zaidi ya Sh854.77 milioni kulipa bonasi kwa wachezaji wake na Sh365.64 milioni kujitangaza, huku Sh352.8 milioni zikielekezwa kwenye pango la makazi.

Baada ya kuingiza Sh120 milioni mwaka 2020 kutokana na mrabaha wa mauzo ya jezi iliyoingia na kampuni ya GSM ambao ndio wadhamini wakuu kwa sasa, timu hiyo inakusudia kuongeza mapato hayo mpaka Sh350 milioni msimu ujao.

Mabadiliko ya katiba

Ili kuendeshwa kisasa, Yanga imebadilisha ibara 62 za katiba yake na kutoa nafasi ya kuingiza mambo mapya au kuyaondoa yaliyopitwa na wakati.

Kwenye mabadiliko hayo, zimeelezwa sifa na wajibu wa wanachama na mashabiki, viongozi wa timu na kampuni za Yanga, usikilizaji na utatuzi wa migogoro ndani ya klabu.

Kati mambo yapya yaliyoongezwa kwenye katiba hiyo, ni uwezo wa mkutano mkuu kumfukuza mwanachama kutokana na uvunjaji wa katiba, kanuni na maagizo ya klabu na sasa anaweza kusimamishwa kulingana na makosa atakayoyafanya ambayo yameainishwa kwenye kanuni za klabu hiyo kongwe nchini.

“Hapakuwa na utaratibu wa kumsimamisha mwanachama,” yanasomeka maelezo yaliyofanywa kwenye ibara ya 12 ya katiba ya klabu hiyo iliyoongeza kifungu namba 2 kinachoweka utaratibu wa kumsimamisha mwanachama.

Yanga pia imerekebisha ibara ya 2, ibara ndogo ya 3 ili kuanzisha na kuendeleza klabu inayosimamiwa vizuri kwa kuajiri watendaji wenye weledi na ujuzi wa hali ya juu.

Mwanachama na shabiki

Kwenye maboresho ya katiba yaliyofanywa, Yanga sasa inawatambua na kuwatofautisha wanachama na mashabiki wake. Kwa mujibu wa ibara ya 5 ya katiba hiyo, mashabiki ni watu wenye mapenzi na klabu, lakini hawaruhusiwi kuhudhuria mikutano ya klabu ingawa watakuwa na kadi.

Tofauti kati ya kadi ya mwanachama na shabiki itakuwa rangi. Ya mwanachama itakuwa ya njano na ya shabiki itakuwa ya kijani. Mwanachama anaweza kuwa kamili au wa heshima. Maboresho haya yamefanywa kwa kuzingatia mapendekezo ya Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).

Yanga itakuwa na wanachama watakaojiunga kwenye matawi yatakayokuwapo nchi nzima. Matawi hayo yatakuwa na wanachama kuanzia 100 ila hawatazidi 500 kwa yatakayokuwa nchini wakati yale ya nje wataanzia 20 tu. Matawi yote yatasajiliwa makao makuu ya klabu.

Matawi haya, kila moja litatoa wajumbe watano watakaohudhura mkutano mkuu. Watakaokwenda mkutanoni ni mwenyekiti wa tawi, katibu, mweka hazina na wajumbe wawili kwa sharti kwamba walau mtu mmoja kati yao awe mwanamke.

Kwa watakaokuwa wanachama hai walau kwa miaka minne, katiba inawaruhusu kugombea nafasi ya uongozi wa klabu, ikiwamo urais au umakamu wa rais. Katika nafasi hizo mbili, mgombea ni lazima awe amehitimu chuo kikuu kinachotambulika na wajumbe wa kamati tendaji wasiwe na elimu chini ya kidato c ha nne.

Kutoka Sh15,000 iliyokuwa inalipwa, sasa mwanachama wa Yanga ambaye atatakiwa kulipia ada yake kielektroniki atalipa Sh36,000 itakayojumuisha Sh10,000 ya kadi, Sh24,000 ada ya mwaka na Sh2,000 ya fomu. Mwanzoni, kila mwanachama alilipia Sh2,000 wakati ada ya mwaka ilikuwa Sh12,000 na fomu Sh1,000.

Mashabiki na watoto hawajasahaulika, wao watalipia Sh5,000 kupata kadi ambayo haitakuwa na michango ya kila mwezi ila, pamoja na wanachama, watashiriki shughuli za klabu mikoani.

Uongozi wa klabu

Mabadiliko mengine yaliyofanywa kwenye katiba ya Yanga yameigusa kamati na sekretarieti. Ukubwa wa kamati ya utendaji umepunguzwa kutoka watu 13 mpaka tisa ambao ni rais na makamu wake, wajumbe watano wa kuchaguliwa na mkutano mkuu na wawili watakaoteuliwa na rais.

Awali, wajumbe waliochaguliwa walikuwa wanane na waliochaguliwa na kamati tendaji (sio rais) walikuwa watatu. Mabadiliko hayo yanaelezwa kuwa yanakusudia “kupunguza gharama za uendeshaji na kuleta ufanisi katika utendaji na uwajibikaji.”

Klabu hiyo sasa itaongozwa na mtendaji mkuu ambaye atawajibika kutoa taarifa ya uendeshaji wa kampuni kwa kamati tendaji na atahakikisha klabu inaendeshwa kwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Mtendaji huyu atazisimamia idara zote nne zitakazokuwa chini ya wakurugenzi, akiwemo wa Tehama atakayepaswa kusimamia miundombinu yote ya klabu, ukiwamo usajili wa wanachama na mashabiki, kutunza kumbukumbu za matawi, kuhifadhi takwimu za wanachama waliopo na wanaojiunga, na kugawa kadi za wanachama.

Kwa mikakati na mabadiliko yaliyofanywa, Asanterabi Barakael, mtaalamu mzoefu wa masuala ya benki, hasa mikopo mikubwa anasema Yanga inaweza kufanikisha miradi yake ya kipaumbele.

“Wanaweza kukopa fedha za ujenzi wa uwanja au kitu kingine cha maendeleo. Hilo huwa linafanyika kwenye taasisi za dini pia. Wanachotakiwa ni kubuni mradi unaoingiza mapato yatakayotumika kurejesha mkopo. Wanaweza kupewa mpaka miaka mitatu kabla ya kuanza kurejesha mkopo wa ujenzi wa uwanja wakiamua kuuchukua.”