Yanga yachukua ubingwa wa tatu mfululizo Ligi Kuu
Muktasari:
- Katika msimu huu, Yanga imeibuka na ushindi katika mechi 23, imetoka sare mbili na imepoteza michezo miwili
Dar es Salaam. Yanga imejihakikishia rasmi ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar leo kwenye Uwanja wa Mangungu Complex, Morogoro.
Mabao ya Kenned Musonda, Nickson Kibabage na Clement Mzize katika kipindi cha pili cha mchezo yalitosha kuifanya Yanga ifikishe pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote hata kama itapoteza mechi zake tatu zilizobakia.
Dalili za Yanga kujihakikishia taji zilianza kuonekana kuanzia dakika ya 63, pale Kennedy Musonda alipoiandikia bao la kusawazisha akimalizia pasi ya Mudathir Yahya.
Kabla ya hapo, dakika ya 32 kipindi cha kwanza, Mtibwa Sugar walitangulia kupata bao kupitia kwa Charles Ilanfya aliyemalizia kwa Kichwa krosi ya Nickson Mushi.
Uhakika wa ushindi kwa Yanga ulianza dakika ya 67 baada ya 67 pale Yanga ilipopata bao la pili ambalo lilikuwa la kujifunga la Nasri Kombo alipokuwa kwenye harakati ya kuokoa shambulizi la Nickson Kibabage.
Jahazi la Mtibwa Sugar lilizamishwa katika dakika ya 81 na Clement Mzize aliyeifungia Yanga, bao la tatu akimalizia kwa mguu wa kulia pasi ya Bakari Mwamnyeto aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi.
Hilo linakuwa ni taji la 30 la Ligi Kuu kwa Yanga ambayo inaongoza kuchukua ikifuatiwa na Simba iliyotwaa mara 22.
Yanga pia imejihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Yanga kutwaa taji la Ligi Kuu baada ya kuchukua katika misimu ya 2021/2022 na 2022/2023.