Sakata la Haji Manara halikustahili kutikisa

Muktasari:

  • Mmoja wa watu walioshiriki kuiwezesha Manchester United mafanikio enzi za Alex Ferguson ni Peter Kenyon, ambaye mwaka 1997 aliteuliwa kuwa naibu ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo na baadaye mwaka 2000 kuwa mtendaji mkuu baada ya kuondoka kwa Martin Edwards.

Dar es Salaam. Mmoja wa watu walioshiriki kuiwezesha Manchester United mafanikio enzi za Alex Ferguson ni Peter Kenyon, ambaye mwaka 1997 aliteuliwa kuwa naibu ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo na baadaye mwaka 2000 kuwa mtendaji mkuu baada ya kuondoka kwa Martin Edwards.

Huyu mtu ndiye aliyeishawishi klabu hiyo ya Old Traford kuachana na uhafidhina wa ubahiri katika usajili na ndiye aliyefanikisha usajili wa kiungo nyota Muargentina, Juan Sebastian Veron na beki kisiki, Rio Ferdina walionunuliwa kwa bei mbaya, ikiwa ni alama ya Manchester United kuachana na woga wa kutumia fedha nyingi kusajili.

Wakati Ferguson anasema anataka kustaafu mwaka 2002, Kenyon ndiye aliyefanya kazi kubwa ya kumshawishi aghairi hadi muda sahihi utakapofika na alifanikiwa. Tena, huenda iliwezekana kwa sababu wakati huo Kenyon hakuwepo tena Old Traford.

Isingekuwa rahisi kwa klabu kumuachia CEO wa aina hii ambaye aliiwezesha klabu kupata mafanikio, aondoke kirahisi. Lakini muda ulipofika Kenyon aliondoka na kituo kilichofuata kilikuwa ni Chelsea, ambako pia aliiwezesha kupata mafanikio, kwa kusaidia kusajili wachezaji nyota na baadaye kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri sana.

Hakuna aliyeona kwamba Kenyon alifanya dhambi kuondoka Manchester United na kujiunga Chelsea, ingawa mashabiki walikuwa hawamuamini baada ya kiungo wao kipenzi, David Beckham kuuzwa Real Madrid na pia klabu kushindwa kumsajili nyota Ronaldhino na badala yake kuishia kumsajili kinda Christiano Ronaldo, ambao wote walikuwa wakihitajiwa Old Traford kwa wakati mmoja.

Hata kocha Syllersaid Mziray alipoondoka Simba kwa mara ya kwanza mwaka 1994, hakuna aliyeona alifanya dhambi. Alishushwa kutoka cheo cha kocha mkuu Simba na kuwa msaidizi, hivyo Yanga wakamfuata na dau kubwa lililomfanya avuke ng'ambo ya pili kwa kasi. Na huo haukuwa mwisho; alihama Simba kwenda Yanga na Yanga kwenda Simba kwa vipindi tofauti baada ya hapo.

Ukiachana na Simba na Yanga, wako watendaji wengi wa klabu ambao wamehama kutoka klabu moja kwenda nyingine, akiwemo Dismas Ten, ambaye alifanya vizuri Mbeya City kabla ya kuhamia Yanga.

Hata viongozi wapo ambao wamewahi kuhama, mfano kutoka Coastal Union kwenda Mtibwa Sugar.


Kama hayo yote ni ya kawaida, kwa nini shauri la Haji Manara kuachana na Simba na kujiunga Yanga limekuwa kubwa na kuonekana la ajabu?

Kuwa mtoto wa gwiji wa zamani wa Yanga, Sunday Manara, hakukumfanya Haji awe maarufu hadi kufikia huu alionao sasa. Alianza kuchomoza wakati akichambua masuala ya soka kituo Radio One Stereo na televisheni ya ITV mwishoni mwa miaka ya tisini, akionekana mwenye hoja nyingi, ufahamu mpana, historia na takwimu.


Na baadaye akajiunga na Uhuru ambako aliendelea kuwa mchambuzi, huku akijenga jina zaidi hadi alipotoweka kwa muda kabla ya kuibukia kuwa katibu mwenezi wa CCM mkoani Dar es Salaam, kazi ambayo aliiacha baada ya kukumbana na matatizo.

Amejitengenezea jina zaidi baada ya kuteuliwa kuwa ofisa habari wa Simba, tena katika kipindi ambacho klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi ilikuwa ina njaa ya mafanikio na ina uwezo wa kuyapata mafanikio. Hivyo haikuwa ajabu kwa jina la Haji kuongezeka umaarufu kadri Simba inavyopata mafanikio.

Tofauti na Kenyon na Mziray waliojihusisha zaidi na wajibu wa kazi zao tu,  Haji hakuishia kuwa mtoa taarifa za klabu kutoka kwa mamlaka na kuandaa mkakati wa mawasiliano wa klabu tu, bali aliweza kujipenyeza na kujijenga kuwa mmoja wa watu muhimu klabuni, aliyethubutu hata kumzuia ofisa mtendaji mkuu wa Simba asijibu swali la mwandishi wa habari na badala yake yeye ndio ajibu kwa kuwa aliamini anawamudu waandishi na si kwamba alikuwa na jawabu sahihi la swali hilo. Maana jibu laweza kuwa lolote, bali jawabu likawa na kile kilichotakiwa katika swali.

Wakati Mziray alijijenga kwa uwezo wake wa kufundisha na kuipa timu mafanikio na Kenyon akimudu kuishawishi bodi kukubali kuachana na mazoea katika usajili, Haji alikwenda mbali zaidi ya kuwa muajiriwa. Haikuwa rahisi kumtofautisha Haji na kiongozi anayesimamia kazi za kila siku klabuni.

Sakata la Haji Manara halikustahili kutikisa

Na mbali ya shughuli za sekretarieti, alikuwa na ujasiri hata wa kuzungumzia masuala ya ufundi, mara kadhaa akiahidi Simba kushinda mechi ambazo hata Fergusson angeogopa kutoa ahadi. Wakati mwingine aliibuka na screen katika mkutano na waandishi wa habari na kuchambua maamuzi ya marefa dhidi ya Simba, kitu ambacho kingefanywa na kocha au kiongozi anayejaribu kujenga hoja dhidi ya uamuzi kama walivyofanya Al Ahly mapema mwezi huu.

Alikuwa tayari hata kuzungumza na waandishi kuhusu hali ya mechi mara baada ya mchezo kuisha kana kwamba ndiye kocha anayewajibika kiufundi kwa matokeo yoyote ya timu.

Na wakati wa safari za timu, hakuwa mstari wa nyuma kama waajiriwa wengine wa sekretarieti. Alikuwa mstari wa mbele pamoja na wachezaji kuliko hata waajiriwa wengine wa benchi la ufundi. Tena alichagua wale nyota na kuchukua picha kwa ajili ya kuziweka kwenye akaunti zake mitandao kuonyesha ukaribu wake na timu-- na pengine kujiongezea umaarufu kwa kutumia nyota hao.

Hakuna shaka kwamba shabiki, mwanachama au mfuasi mwingine yoyote asiyejua masuala ya timu, angeamini kuwa hayo anayoyafanya Haji ndiyo yanastahili na bila shaka umaarufu wake uliongezeka kwa kufanya vitendo ambavyo hakutakiwa kuvifanya.

Kocha mweledi angezuia tabia hiyo ya muajiriwa wa sekretarieti. Angetaka wachezaji waachwe peke yao ili wajadili mambo yao na hivyo kusiwe na uwezekano wa mambo yao kuvuja.

Haikuwa rahisi kutofautisha anuani au kurasa zake katika mitandao ya kijamii na zile za Simba. Mara zote alikuwa mtandaoni akishambulia wanaompinga, wapinzani wa Simba, kusifia anaowataka kwa wakati huo na kubeza mipango ya wengine.

Nguvu ya Haji Manara Yanga

Na hakuishia hapo. Mara kadhaa aliapa kunyesha kuwa yeye ndiye Simba kindakindaki, ambaye hawezi kurubuniwa "hata kwa fedha zote za World Bank" ili aisaliti klabu na hata angefanyiwa nini asingeweza kuiacha "klabu yake kipenzi".

Alionekana ni kiongozi asiyeguswa na hata bosi wake, Barbara Gonzalez, ambaye baadaye akawa chanzo cha safari yake nje ya Simba.

Katika hali ya kawaida, isingekuwa habari kubwa wala ya kustua kwa Haji, ambaye alikuwa mkuu wa idara ya habari Simba, kuiacha klabu na hata kwenda kuajiriwa sehemu nyingine kama si vituko hivyo nilivyoanisha hapo awali.

Na kwa jopo lililokuwepo jana wakati wa kumtambulisha kwa muajiri wake mpya, nachelea kusema kuwa mambo hayo yanaweza kuhamia Yanga iwapo uongozi hawatakuwa makini na kumuwekea Haji an waajiriwa wengine adidu za rejea zinazoonyesha mipaka ya majukumu yake kwa kuwa tayari ameshaanza kuahidi makubwa hata kabla ya kukaa siku mbili makao mapya.

Yanga haina budi kutengeneza adidu za rejea za majukumu ya watendaji wake (JDs) vizuri ili wajue mipaka ya kazi zao na kuepuka muingiliano kama ulivyokuwa Simba, ili weledi uonekane na mageuzi inayoyafanya yaende katika mkondo bora ambao hautoi mwanya wa kuibuka migogoro.

Na kwa sababu ni lazima wapo watu ambao hawakubaliani na uamuzi wa kumchukua Haji, watakuwa wakifuatilia kila hatua kuona kama kinachofanyika ni sahihi ili pale ambapo hawaridhiki, waibuke kwa nguvu kubwa, hali inayoweza kuvuruga mambo.

Kama Yanga itakuwa makini katika masuala hayo, hata itakapotokea anaondoka, sakata lake halitakuwa kubwa wala la kushangaza kama lilivyo sasa.