Sasa ni Simba dhidi ya ‘Yanga’ wa Afrika Kusini

Wednesday May 12 2021
yanga pic
By Edo Kumwembe

WAKUBWA wamegoma kuchutuma na wameanza kurushiana mpira baada ya kushindwa kuuheshimu mpira Jumamosi jioni katika Uwanja wa Mkapa. Wengine hatujali. Tunasonga mbele. Muda si mrefu nitaanza safari ya kwenda Johannesburg, Afrika Kusini.

Mnyama Simba ana kesi nyingine ya kujibu Afrika Kusini baada ya kupasha misuli moto bila ya kucheza dakika yoyote katika pambano dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga. Walinawa bila ya kula. Haikujulikana matokeo yangekuwaje.

Na sasa Simba wanalazimika kuingia uwanjani wikiendi hii kucheza na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika uwanja ambao ulichezwa fainali ya Kombe la Dunia kati ya Hispania na Uholanzi mwaka 2010 maarufu kwa jina la FNB.

Ni pambano la robo fainali ambalo mpaka sasa Simba wameuinamisha uwanja na wana matokeo ya aina moja tu, ushindi.

Kiburi na jeuri za Simba hii ni kwamba wana uwezo wa kushinda mechi hii ugenini na pia wana uwezo wa kushinda nyumbani.

Ni vigumu kuwabishia. Namba zao hazidanganyi. Miongoni mwa namba zao maarufu katika michuano ya mabingwa msimu huu ni kwamba waliwafunga AS Vita ya DR Congo katika ardhi ya Kinshasa. Hauwezi

Advertisement

kuwabishia wakikwambia kwamba wanataka kwenda kuwafunga Kaizer Chiefs kwao.

Miongoni mwa namba zao maarufu pia ni ile sare yao dhidi ya Al Merrikh ugenini pale Khartoum, Sudan. Sio kazi rahisi sana kupata sare Sudan hasa kwa timu kama Al Merrikh. Wanapokwambia wanataka kuifunga Kaizer Chiefs ugenini lazima uelewe.

Kiburi cha Simba kimetapakaa kuanzia kwa benchi la ufundi, viongozi, mashabiki lakini zaidi kwa wachezaji.

Kiburi kinapotapakaa kwa Clatous Chama, halafu kikaenea kwa Louis Miquissone, kisha kikafika kwa kina Rally Bwalya na Bernard Morisson, basi kumbuka kwamba Simba inaweza kufanya jambo lolote eneo lolote lile.

Kiburi kinapokuaminisha kwamba unaweza kufanya lolote katika uwanja wa ugenini ni jambo jema. Inatokea mara chache kwa timu ya Tanzania ikajiaminisha kwamba inakwenda kushinda pambano la robo fainali Ligi ya Mabingwa wa Afrika ugenini. Simba inaweza kuwa timu ya kwanza kufikia kiwango hiki cha kiburi na ukitazama vyema wanastahili.

Tatizo kubwa linaweza kuja upande wa pili. Kaizer Chiefs. Hawa jamaa ni sawa na watu wanaokufa maji. Wanataka kumng’ang’ania mtu yeyote ambaye atajitokeza mbele yao. Watajaribu kumgeuza kuwa gogo la kufika ufukweni.

Kaizer wamekuwa na msimu mbovu Afrika ya Kusini. Mpaka sasa wapo nje ya nane bora katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini. Kikubwa ambacho kimewakumba ni kwamba walifungiwa kusajili wachezaji mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kuvurunda kanuni za usajili.

Wamekuwa na msimu wa ovyo, lakini kuna mambo mawili ambayo Simba inabidi wajihadhari nayo kwa watu hawa wanaovaa jezi za njano kama watani zao, Yanga.

Kitu cha kwanza kabisa ni kwamba Kaizer wameelekeza nguvu zao katika michuano hii na sio kwenye Ligi Kuu.

Huwa inatokea mara kadhaa. Timu inawekeza nguvu zake katika michuano fulani baada ya kuchemsha katika ligi. Ni kama ambavyo Liverpool mwaka 2005 waliwekeza

nguvu zao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na wakaitwaa huku katika Ligi Kuu ya England wakishindwa kushika nafasi nne za juu. Mifano ni mingi.

Simba wahofie kucheza na timu ya namna hii na hasa unapokumbuka kwamba Kaizer ina wachezaji watatu ambao walikuwepo katika kikosi cha Mamelodi Sundwons kilichotwaa michuano hii mwaka 2016. Miongoni mwa mastaa hawa ni Kharma Billiat ambaye ni nyota wa kimataifa waZimbabwe.

Msimu huu Billiat amekuwa akisumbuliwa na majeraha na hajacheza mechi nyingi. Katika michuano hii amecheza mechi mbili tu, lakini hadi kufikia hapa walipofika inamaanisha kwamba wana wachezaji wengine ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri wakati yeye akiwa hayupo.

Kitu kingine ambacho kinashangaza kuhusu Kaizer Chiefs ni ukweli kwamba licha ya kwamba imekuwa na msimu mbovu Afrika Kusini ikiwemo kufungwa na timu ndogo, lakini wameshinda mechi mbili ngumu za kupania.

Msimu huu, Kaizer wamewachapa watani zao wa jadi, Orlando Pirates katika pambano la watani wa jadi wa Soweto.

Hili ni kama pambano ambalo liliota mbawa katika Uwanja wa Mkapa Jumamosi usiku. Ni miongoni mwa mechi bora za watani wa jadi barani Afrika.

Kama vile haitoshi, Kaizer ndio timu ambayo iliharibu rekodi nzuri ya Mamelodi Sundwons ya kucheza bila ya kufungwa katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Waliwachapa katika ligi. Hii inaonyesha kwamba Kaizer ni wataalamu wa mechi za kupania.

Kama waliweza kushinda mechi hizi mbili za kukamia nadhani Simba inabidi wajihadhari hasa kwa kuzingatia kwamba Kaizer wana uwezo mkubwa wa kukamia mechi hii kwa sababu ni mechi ambayo inaweza ghafla kuubadilisha msimu wao kutoka kuwa msimu mbaya na kuwa msimu mzuri.

Kitu kingine kibaya kwa Simba ni kwamba rekodi yao ya Ligi ya Mabingwa msimu huu inaweza kuzitisha timu nyingine za Afrika zikajikuta zikijiandaa mara mbili ya vile ambavyo zingeweza kujiandaa misimu kadhaa nyuma.

Timu yoyote ya Afrika ikitazama mikanda ya mechi za Simba za msimu huu ndani na nje ya uwanja wa Afrika, nadhani zitajiandaa mara mbili zaidi tofauti na ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.

Simba wamepambana kujiingiza kuwa miongoni mwa timu bora Afrika na lazima wawe makini na sifa ambazo wanajipatia.

Vinginevyo nitakuwepo Johannesburg kutazama Simba wanaweza kufanya nini dhidi ya Kaizer Chiefs. Kila la heri kwao.


Kwa maoni tuandikie SMS au WhatsApp kupitia namba 0658 376 417

Advertisement