Serengeti Boys na hesabu za Afcon U17
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Yusuf Mossi, Mkurugenzi wa Mashindano wa CECAFA, nchi tisa zitashiriki kwenye michuano hii ya kufuzu, ambazo ni Uganda, Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini na Tanzania.
Kikosi cha Serengeti Boys, kinaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya michuano ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) U17 kwa kanda ya CECAFA, itakayofanyika kuanzia Desemba 14 hadi 28, 2024, Uganda.
Katika maandalizi hayo, kocha wa kikosi hicho, Aggrey Morris, alieleza kuwa wachezaji wanazidi kuimarika kila siku na wanajua kabisa umuhimu wa michuano hiyo kwa ajili ya maendeleo ya soka la vijana Tanzania.
"Tunafanya kila kitu kwa bidii ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na timu imara kwa michuano ya kufuzu AFCON. Wachezaji wanajitahidi na wana ari kubwa ya kushinda. Lengo letu ni kufuzu kwa michuano ya AFCON U17 na tutahakikisha tunafanya kila lililo bora ili kulifikia hilo," alisema Morris.
Katika kuwapa hamasa wachezaji wa kikosi hicho, siku chache zilizopita Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliwatembelea wachezaji hao na kuwatia moyo katika maandalizi yao wakiwa chini ya Morris na Boniface Pawasa.
Kwa mujibu wa Yusuf Mossi, Mkurugenzi wa Mashindano wa CECAFA, nchi tisa zitashiriki kwenye michuano hii ya kufuzu, ambazo ni Uganda, Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini na Tanzania.
Nchi hizo zitakuwa na nafasi ya kupigania moja ya nafasi mbili za juu (fainali) zitakazowapa tiketi ya kushiriki AFCON U17 2025.
Mashindano ya kufuzu yatachezwa kwenye miji ya Bukedea, Mbale na Kampala nchini Uganda na timu zote zitakuwa na jukumu la kufanya vipimo vya Magnetic Resonance Imaging (MRI) kwa wachezaji wao kabla ya kuingia uwanjani.