VAR Ligi Kuu yaibua wadau

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amesema Serikali inakusudia kuwasilisha pendekezo la kuondoa kodi kwenye vifaa vya teknolojia inayomsaidia mwamuzi kufanya marejeo ya picha (Video Assistance Referee-VAR) kuanzia mwaka mpya wa fedha 2024/2025.
Amesema pendekezo hilo litawezesha viwanja vyote hapa nchini vinavyotumika kuchezwa ligi hiyo kufungwa VAR lengo likiwa ni kuhakikisha matokeo yanayopatikana yanakuwa ya haki.
Pia Serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya vya mpira wa miguu na kukarabati baadhi ya vilivyopo, kuhusu ubora wa eneo la kuchezea 'pitch' tayari Serikali ilitunga sheria inayotoa msamaha kwenye uingizaji wa nyasi bandia na vifaa vyake.
Mwigulu ameyasema hayo leo Alhamisi, Juni 13, 2024 wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2024/2025.
"Msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania tutaanza kutumia 'VAR' ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki maana kuna timu zimezidi - msimu mmoja penalti 10, halafu zikifungwa zenyewe magoli yanakataliwa. Na ili tuwe na 'VAR' za kutosha katika viwanja vyote, naleta pendekezo la kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za 'VAR' na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadae. Inawezekana," amesema Mwigulu.
Ikumbukwe kwamba, mpango wa matumizi ya VAR kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara umeshaanza kufanyiwa kazi ambapo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hivi karibuni liliendesha mafunzo ya kufunga vifaa vya VAR yaliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam yakiongozwa na Meneja wa Teknolojia ya Soka kutoka CAF, Wael Elsebaie.
Mafunzo hayo ya kuvifunga sambamba na kuviendesha vifaa hivyo yalishirikisha jumla ya watu sita wakiwemo Watanzania wanne na Wakenya wawili. Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, yataanza mafunzo kwa Waamuzi waweze kutumia VAR katika michezo mbalimbali.
VAR imekuwa ikitumika kwenye Ligi na mashindano mbalimbali duniani kwa sasa yakiwemo ya Euro ambayo yanaanza leo nchini Ujerumani.
Kwa Tanzania hii itakuwa mara ya kwanza kufanyika kwenye ligi lakini ikiwa imeshatumika kwenye michuano ya kimataifa, ukiwemo mchezo wa Yanga na Mamelodi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Al Ahly msimu uliopita, lakini pia Simba ilikumbana nayo tena kwenye mchezo wa African Football League ilipovaana na Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa.
Wadau wafunguka
Wadau wamekuwa na maoni tofauti kuhusu tangazo hilo, huku wengi wakiamini kuwa haki itakuwa inatendeka kwenye ligi.
Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola amesema kama hili likikamilika basi litasaidia mchezo huu hapa nchini kupiga hatua, lakini itapunguza lawama na malalamiko ambayo yamekuwepo huko nyuma.
"Nimefuatilia hata mimi, hili ni jambo zuri sana, waamuzi nao ni binadanu siyo kwamba kila mara wanapendelea, nafikiri kama ni kufungwa basi zifungwe viwanja vyote ili bingwa nchi apatikane kwa uhalali wake.
Kuna wakati unaonekana matukio kwenye ligi unasema kungekuwa na VAR pale siyo bao, hivyo ujio huo sasa utasaidia kwa sehemu kubwa," alisema Matola kocha wa zamani wa Lipuli.
Mkuu wa Kitengo cha habari wa Azam FC, Zacharia Thabith Zakazakazi, amesema ni jambo la kupongeza lakini VAR siyo suluhisho la moja kwa moja kwenye matatizo ya soka kwa kuwa wanaoamua bado ni waamuzi ndiyo maana bado kuna malalamiko dunia nzima.
"Tuboresje kwenye vifaa viwe bora, lakini pia watu wanatakiwa kufahamu kuwa ujio wa VAR siyo suluhisho la moja kwa moja kwa kuwa bado kumekuwa na malalamiko sehemu mbalimbali pamoja na kwamba wanatumia teknolojia hii.
"England tumeona mpaka walifikia hatua wanataka kupiga kura kama waendelee kuitumia au la, hivyo tunatakiwa kushukuru kwa hili, lakini tuwe na tahadhari ya kutosha," alisema Zaka.
Kwa upande wa mwamuzi Frank Komba yeye alisema: Ni jambo jema, litasaidia kuleta utendaji haki na litanufaisha ziadi timu ndogo, maana vilio vingi ni kwa timu kubwa kupendelewa.
"Kwa upande mwingine italeta heshima kwa waamuzi wa Tanzania kwa sababu haitatokea tena muamuzi kuonekana ni mjinga au mzembe maana maamuzi yote yatatolewa kwa mujibu wa picha za marudio."
Ofisa Habari wa Coastal, Abbas Elsabri, amesema ujio wa VAR katika Ligi Kuu Bara itawasaidia wengi katika kupata haki ndani ya uwanja baada ya kuwepo kwa matukio tata mengi yaliyoziacha timu katika maumivu makali.
"Ujio wa VAR katika ligi yetu itakuwa kitu kizuri kwa sababu hivi sasa dunia ipo kiteknolojia zaidi, hii itawasaidia waamuzi kwani nao ni binadamu kuna wakati wanapitwa na matukio ambayo wanashindwa kuyatolea uamuzi sahihi na kuleta utata," alisema Elsabri.