Simba ina sapraizi kubwa kwa mashabiki

Muktasari:

  • MASHABIKI wa Simba kwa sasa hawana raha mtaani kutokana na taarifa za kila mchezaji anayetajwa kutua Msimbazi kuyeyuka na wengine wakitajwa kusajiliwa kuonekana kutowavutia, lakini mabosi wa klabu hiyo wamewataka watulie kwani kuna sapraizi yao.

MASHABIKI wa Simba kwa sasa hawana raha mtaani kutokana na taarifa za kila mchezaji anayetajwa kutua Msimbazi kuyeyuka na wengine wakitajwa kusajiliwa kuonekana kutowavutia, lakini mabosi wa klabu hiyo wamewataka watulie kwani kuna sapraizi yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewataka wanasimba watulie kwani muda utafika watawatambulisha mastaa ambao wamekamilisha usajili wao na itakuwa sapraizi kwao tofauti na kelele za mitaani.

Simba imekuwa kimya tangu ilipomtangaza Moses Phiri kuitoka Zanaco ya Zambia, tofauti na ilivyozoeleka kwa misimu kadhaa nyuma, lakini Try Again alisema dirisha linafunguliwa Julai Mosi hadi Agosti 31, hivyo kuna sapraizi kwa mashabiki wao, watulie tu!

Try Again alisema katika mitandao ya kijamii ni mambo mengi yanazungumzwa lakini wao wanafanya kazi kwa masilahi mapana ya klabu yao.

Alisema hawawezi kukurupuka katika usajili wanachokifanya ni kumfuatilia vilivyo mchezaji kabla hawajaingia makubaliano naye.

“Ngoja tumalize ligi ndio tutashusha vitu wanasimba wasijali tupo kwa ajili yao, ndio maana wametuamini,” alisema Try Again na kuongeza;

“Hatuna kocha kwa sasa atakapokuja ndio tutaendelea kuwajulisha kama tulivyofanya kwa Moses Phiri kutoka Zanaco.”

Alisema msimu huu wamepoteza mataji matatu waliyokuwa wakiyashikilia, ni sehemu ya mchezo hivyo wanakisuka kikosi chenye ushindani zaidi msimu ujao ili kurejesha heshima yao ndani na kwenye anga la kimataifa na msimu huu ilifika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.