Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba kupambania rekodi mpya kwa Raja

Dar es Salaam. Ushindi au sare dhidi ya Raja Casablanca, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa utaifanya Simba kuboresha rekodi yake ya kucheza idadi kubwa ya mechi mfululizo za nyumbani za hatua ya makundi ya mashindano ya klabu bila kupoteza.

Ikiwa inashiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika kwa awamu ya tano, Simba haijawahi kupoteza mechi yoyote kati ya 12 zilizopita ambapo imeibuka na ushindi mara 11 na kutoka sare moja tu.

Katika mechi hizo 12 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo Simba ilicheza kwa nyakati tofauti, imefunga jumla ya mabao 25 na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu.

Mara ya kwanza kwa Simba kucheza hatua ya makundi ilikuwa ni mwaka 2003 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika mechi tatu za nyumbani, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast na ikaifunga Enyimba ya Nigeria kwa mabao 2-1 na ikatoka suluhu na miamba ya Misri, Ismaily.

Simba ilitinga tena katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019 ambapo ilipata ushindi katika mechi zote tatu za nyumbani, ikiifunga mabao 3-0, JS Saoura ya Algeria, 1-0 Al Ahly ya Misri na mechi nyingine ikaichapa AS Vita Club ya DR Congo kwa mabao 2-1.

Utemi wa Simba nyumbani katika mechi za hatua ya makundi ya klabu Afrika uliendelea tena katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020/2021 walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly, wakaichapa Al Merrikh ya Sudan kwa mabao 4-1 na kisha wakaichakaza AS Vita kwa mabao 4-1.

Msimu uliopita, Simba walitinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo katika mechi tatu za nyumbani, waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Asec Mimosas, wakaichapa RS Berkane ya Morocco kwa bao 1-0 na wakashinda mabao 4-0 dhidi ya USGN ya Niger.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendeleza ubabe wao nyumbani katika mechi dhidi ya Raja Casablanca na akawasihi mashabiki wao wajitokeze kwa wingi ili kuwapa hamasa wachezaji.

“Dhumuni letu (viongozi) tunataka uwanja ujae. Kwa namna tulivyozungumza na wachezaji na benchi la ufundi wako tayari kutupa ushindi,” alisema Mangungu.