Simba wabadilishiwa Uwanja Misri

Simba wabadilishiwa Uwanja Misri

Muktasari:

  • Wakati msafara wa Simba ukitua Misri leo tayari kwa mechi dhidi ya Al Ahly  itakayofanyika Ijumaa (saa 4.00 usiku kwa saa za Tanzania), wenyeji wametangaza mabadiliko ya uwanja utakaotumika kwa mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Wakati msafara wa Simba ukitua Misri leo tayari kwa mechi dhidi ya Al Ahly  itakayofanyika Ijumaa (saa 4.00 usiku kwa saa za Tanzania), wenyeji wametangaza mabadiliko ya uwanja utakaotumika kwa mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Tofauti na mechi mbili zilizopita dhidi ya Al Merrikh na AS Vita ambazo zilichezwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, mchezo dhidi ya Simba utachezwa katika Uwanja wa Al-Salam WE mbao unamilikiwa na Al Ahly
Mkurugenzi wa Mpira wa Miguu wa Al Ahly, Sayed Abdelhafiz amethibitisha mabadiliko hayo ya Uwanja jana kupitia tovuti na kituo cha luninga cha klabu hiyo.
"Wachezaji wetu watakusanyika El Tetsh leo (jana) kuanza maandalizi yao kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Ijumaa kuanzia saa 3.00 usiku (saa 4.00 usiku kwa muda wa Tanzania).
Kikao cha kiufundi cha mechi kitafanyika Alhamisi Saa 8.00 Alasiri katika makao makuu ya Al Ahly yaliyopo, Gezira, Cairo," amethibitisha Abdelhafiz.

Mara ya mwisho kwa Al Ahly kuchezea Uwanja wa Al-Salam WE katika Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni Januari 5 mwaka huu wakati Al Ahly ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya AS SONIDEP kutoka Niger.
Baada ya hapo, mechi mbili zilizofuata za hatua ya makundi ilichezea katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo ambapo mechi ya kwanza waliibamiza Al Merrikh kwa mabao 3-0 na kisha wakaja kutoka sare ya mabao 2-2 na AS Vita Club ya DR Congo.