Simba yaachiwa msala wa waarabu

USHINDI wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita umeifanya Simba kuepuka kukutana na vinara wenzake wa makundi, lakini bado wameachiwa msala wa kukutana na timu za Afrika Kaskazini maarufu kama Waarabu kwenye hatua ya robo fainali.

Hata hivyo, Simba wana faida ya kuanzia ugenini mechi ya kwanza na kumalizia nyumbani, tofauti na kama wangemaliza kwenye nafasi ya pili ambapo timu huanzia nyumbani na kumalizia mechi zake ugenini, kitu ambacho huwa na presha kubwa jambo alililokuwa akilikwepa kocha Didier Gomes.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Simba imefikisha pointi 13 na kujihakikisha uongozi wa Kundi A mbele ya Al Ahly, na hivyo kuikwepa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini ikiwa bado kwenye hatihati ya kukutana na vigogo wengine kulingana na matokeo ya mwisho ya makundi ya B, C na D.

Kwani mpaka sasa licha ya Wydad Casablanca, Esperance kuongoza makundi yao ya C na D bado wanaweza kupoteza uongozi kama matokeo ya mwisho ya timu walizonazo kundini yatakuwa tofauti na mipango yao.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kwa namna misimamo ilivyo kwa sasa, timu za CR Belouizdad ya Algeria au Al Hilal ya Sudan ni kati ya timu zinazoweza kupangwa na Simba zikitokea kundi B nyuma ya Mamelodi, lakini ikitegemea na mechi zao za mwisho wikiendi hii, huku Waalgeria wakiwa na nafasi kubwa zaidi.

Belouizdad ipo nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na alama 6 na itamaliza mechi yao Ijumaa ugenini dhidi ya Mamelodi, wakati Al Hilal ina pointi nne nayo itamaliza mechi ugenini dhidi ya vibonde wa kundi hilo, TP Mazembe. Kama Waalgeria watapasuka na Al Hilal ikashinda, basi Wasudan watafuzu na kujiandaa kuvaana na Simba, lakini matokeo ya sare kwa mechi zote mbili au kipigo kwa Wasudan itawanufaisha Waalgeria.

Katika Kundi C, Wydad inaongoza kundi na alama 10, huku timu za AC Horoya na Kaizer Chiefs zinafuata nyuma yao kila moja ikiwa na pointi 8 na matokeo yoyote baina yao Jumamosi, huku Wamorocco wakichemsha itafanya timu mojawapo kumaliza kama kinara na Wydad kupangwa na Simba, vinginevyo ni kwamba kati ya Waguinea na Wasauzi watavaana na Simba robo fainali.

Esperance inaongoza kundi D kwa sasa, ikiwa imeshafuzu kwa alama zao 10, lakini itacheza na MC Alger inayofuata nyuma yenye pointi nane na kama itafungwa nyumbani, Waalgeria wataongoza kundi na Watunisia hao watalazimika kucheza na Simba.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ikitokea Alger wakapasuka na Zamalek yenye pointi 5 ikiwa nafasi ya tatu ikashinda, itafikisha nao pointi 8 na kuungana na Esperance kwa matokeo ya wenyewe kwa wenyewe na MC Alger na hivyo Wamisri ndio watakaopangwa na Simba. Zamalek itaialika Teangueth ya Senegal ikiwa nyumbani.

Hivyo kwa hesabu hizo zilivyo ni kwamba Simba ni ngumu kuwakwepa Waarabu kwenye hatua hiyo ya robo fainali hata kama uamuzi zaidi unategemea droo itakayopangwa Aprili 30 mwaka huu.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alikaririwa kwamba kwa namna alivyojiandaa tangu alipochukuliwa na Simba ni kupambana na timu yoyote kwani kwa hatua iliyofikia kwenye michuano huwezi kukwepa timu ya kucheza nao.

“Tupo tayari kucheza na timu yoyote, tunataka kufika mbali zaidi,” alisema Gomes.