Simba yajiweka katika wakati mgumu nyumbani

Muktasari:
- Mchezo wa marudiano wa hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utachezwa nchini Tanzania, Mei 25, 2025.
Berkane, Morocco. Simba ina mlima mgumu wa kupanda ili iweze kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya leo kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane kwenye mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane hapa Morocco.
Ushindi wa mabao 2-0 ambao RS Berkane imeupata katika mechi ya leo unailazimisha Simba kuibuka na ushindi wa kuanzia angalau mabao 3-0 ili iweze kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Bao la kwanza la RS Berkane lilifungwa katika dakika ya nane ya mchezo na Mamadou Camara akimalizia kwa kichwa mpira wa kona wa Hamza El Moussaoui.
Kabla Simba haijajipanga baada ya bao hilo, Oussama Lamlioui aliipatia RS Berkane bao la pili dakika sita baadaye lililotokana na shuti lake la wastani alilopiga baada ya kumalizia pasi ya Imad Riahi.
Dakika ya 23, Simba ilipata pigo baada ya beki wake wa kati Abdulrazack Hamza kupata maumivu yaliyolilazimisha benchi la ufundi la Simba kumfanyia mabadiliko na nafasi yake kuchukuliwa na Che Fondoh Malone.
Dakika nne baadaye, refa wa mchezo huo, Atcho Pierre kutoka Gabon alimuonyesha kadi ya njano kocha Fadlu Davids wa Simba kwa kosa la kumfokea mwamuzi msaidizi.
Kipindi hicho cha kwanza kilitawaliwa zaidi na RS Berkane ambayo ilipeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Simba lakini hadi filimbi ya kuashiria mapumziko, hakukuwa na mabadiliko katika ubao wa matokeo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko ya kumtoa Kibu Denis na nafasi yake kuchukuliwa na Valentine Nouma, ambayo yalionekana kulenga kupunguza nguvu ya RS Berkane upande wa kulia ambao ulionekana kuwa mwiba kwa Simba.
Katika kipindi hicho cha pili, Simba ilifanya mabadiliko mengine ya kuwatoa Elie Mpanzu na Charles Ahoua ambao nafasi zao zilichukuliwa na Joshua Mutale na Debora Fernandes.
Katika kipindi hicho cha pili, Simba angalau ilionyesha uhai na kulishambulia lango la Berkane mara kadhaa lakini wenyeji walikuwa imara na kulinda ushindi wao.
Kwa upande wa RS Berkane katika mchezo huo ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Hamza El Moussaoui, Imad Riahi, Mohamed El Morabit, Oussama Lamlioui na Yassine Labhiri ambao nafasi zao zilichukuliwa na Youssef Zghoud, Mohamed El Morabit, Mateus Santos, Bello Ilou na Reda Hajji.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema wana matumaini ya kupindua meza kwenye mechi ya marudiano nyumbani.
“Matokeo haya tuliyopata yanatupa ujasiri na mimi nikuambie hizi goli mbili walizopata hapa kwao, watakwenda kuzitapika tukiwa nyumbani,” amesema Ahmed Ally.