Prime
Simba, Yanga pigo la makipa Stars
Muktasari:
- Kipa huyo ikiwa ni mara ya kwanza anaidakia Taifa Stars kwenye mechi za mashindano, amefanikiwa kuonyesha kiwango cha juu kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024)
Tetesi zinasema kuwa tayari klabu ya Simba imeshafanikiwa kumsajili kipa namba moja wa JKT Tanzania na Taifa Stars, Yacoub Suleiman kwa mkataba wa miaka miwili.
Yacoub ambaye alidaka katika michezo mingi ya JKT Tanzania msimu uliopita na kuiongoza timu hiyo kumaliza kwenye nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu Bara akiwa ndiye kipa mzawa aliyefanya vizuri zaidi, inadaiwa kuwa ameshamalizana na Simba kwa sehemu kubwa.
Kipa huyo ikiwa ni mara ya kwanza anaidakia Taifa Stars kwenye mechi za mashindano, amefanikiwa kuonyesha kiwango cha juu kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) akiwa ndiye ambaye hadi sasa ameruhusu mabao machache ambalo ni moja tu kwenye michezo minne.
Awali mashabiki wengi hawakuwa na imani naye kwa kuwa alikuwa hajatumika sana kwenye kikosi cha Stars au michuano ya kimataifa, lakini uwezo wake umeonyesha kuwa ni mmoja kati ya makipa tegemeo kwenye timu ya taifa kwa sasa na baadaye.
Hata hivyo, taarifa za kusajiliwa na Simba ni pigo kubwa kwenye kikosi cha Stars kwa kuwa ni aidha ataachwa kwenye kikosi hicho au ataitwa lakini ubora wake utakuwa wa chini.
Yacoub mwenye miaka 25, anakwenda Simba ambapo kipa wake namba moja ni Moussa Camara ambaye msimu uliopita alionyesha kiwango cha juu zaidi uwanjani akimaliza kinara wa clean sheet akikusanya 19 katika michezo 28 huku akiifanya timu hiyo ishike nafasi ya pili kwa kuruhusu mabao machache nyuma ya Yanga baada ya kufungwa 13 pekee.
Ni dhahiri kuwa kipa namba moja wa Simba kwa msimu mwingine atakuwa Camara na Yacoub atasubiri kwenye benchi, au atacheza endapo staa huyo anayeichezea timu ya Taifa ya Guinea ataumia, atapewa kadi au atapumzishwa na kocha wake Fadlu Davids jambo ambalo limekuwa likitokea mara chache sana.
Hii ina maana kuwa ubora wa Yacoub ambaye aliruhusu mabao 27 akiwa na JKT msimu uliopita utashuka, lakini kutocheza kwake mara kwa mara kutamfanya kocha wa Stars kutomjumuisha kwenye kikosi chake kwa kuwa hapati nafasi ya kubwa ya kucheza klabuni.
Ni sahihi kusema kuwa kipaji hiki ambacho kinaonekana kwa sasa kulibeba Taifa kipo njiani kupotea ingawa maisha yake binafsi yanaweza kustawi na kuongeza uzoefu zaidi.
Picha halisi inaonyesha kuwa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam imani yao ipo kwa makipa wageni zaidi kwa sasa kuliko wazawa, jambo ambalo linasababisha kuwe na chaguo dogo kwenye kikosi cha Taifa Stars endapo huyu angebaki alipo msimu ujao angekuwa kipa namba moja wa Stars mwenye uzoefu.
Ally Salim, alikuwa mmoja kati ya makipa ambao alipata mafanikio akiwa Simba ambapo alionyesha kiwago bora kwenye mchezo wa Dabi ya Kariakoo uliochezwa Aprili 26, 2023 katika ushindi wa 2-0, ambapo alipata nafasi ya kuidakia timu hiyo baada Aishi Manula kuwa na majeraha na baadaye kuonyesha ubora wa juu kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2022-2023 dhidi ya Wydad Casablanca kwenye Uwanja wa Mkapa na nchini Morocco.
Ubora huo ulimfanya Salim akaitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ambapo alionekana kuwa mkombozi wa timu hiyo kwenye michezo kadhaa kwani alikuwa pia akipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara, lakini baada ya kusajiliwa Camara msimu uliopita kipa huyo hakupata nafasi jambo ambalo lilimlazimisha kocha Hemed Suleiman Morocco kumweka pembeni kwenye kikosi chake.
Achana na Salim, Aishi Manula ambaye naye msimu uliopita alikuwa bado kwenye kikosi cha Simba, hakupata nafasi ya kucheza mchezo hata mmoja wa kiushindani kwenye kikosi hicho kutokana na uwepo wa Camara, hali hiyo ilimfanya kwa mwaka mzima akaitwa kwenye kikosi cha Stars mara mbili na alitumika kwenye kikosi cha Stars kilichofuzu AFCON na baadaye benchi la ufundi la Taifa Stars lilimweka nje kwa maelezo kuwa hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye klabu, jambo ambalo ni sahihi na kulipoteza rasmi jina la Tanzania One akiwa ndiye kipa kwa sasa ambaye ameshatumika kwenye michezo mingi ya Stars.
Mwingine ambaye alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kuonyesha ubora kwenye kikosi cha Stars ni kipa namba mbili wa Yanga, Aboutwalib Mshery, ambaye amefunikiwa na uwepo wa Djigui Diarra kwenye kikosi hicho.
Pamoja na kwamba makocha wamekuwa wakimwita mara chache kwenye kikosi cha Taifa Stars, lakini wameshindwa kumtumia kwa kuwa hapati nafasi ya kuonyesha uwezo kwenye klabu anayoitumikia ambapo katika michezo mingi amekuwa akidaka Diarra ambaye anaitumikia timu ya Taifa ya Mali na ubora wake umekuwa mkubwa zaidi tangu alipojiunga na Yanga kwani anacheza michezo mingi, huku wazawa, Mshery na Khomeiny Abubakar wakiendelea kushuka.
Hata kipa namba namba tatu wa sasa wa Taifa Stars, Hussein Masalanga yupo kwenye kikosi kwa kuwa makocha hawakuwa na chaguo lingine, lakini inavyoonekana hawezi kudumu kwenye timu hiyo endapo atapatikana mwingine bora kwani hapati nafasi kubwa ya kuichezea Singida Black Stars mara kwa mara.
Msimu uliopita, Masalanga hakupata nafasi kubwa ya kucheza ndani ya Singida Black Stars kutokana na uwepo wa kipa raia wa Nigeria, Amas Obasogie ambaye amekuwa akitumika mara kwa mara kwenye kikosi cha Nigeria tangu atue kipindi cha dirisha dogo.
Ni rahisi kusema kuwa sasa anaweza kuitwa, Zubeir Foba wa Azam FC kwa kuwa msimu uliopita alipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha klabu anayoitumikia kuliko makipa wengine wote wazawa ambao wameitwa, lakini hata yeye sasa hayupo tena salama baada ya timu hiyo kumsajili Issa Fofana kutoka Al Hilal.
Hii inaonyesha kuwa nafasi chache pia ambazo alikuwa anazipata Foba msimu uliopita zitamalizika rasmi na endapo Fofana ataanza vyema kwenye timu hiyo ambayo msimu ujao itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, itaifanya Ivory Coast kupata chaguo lingine kupitia kwake.
Wadau wanasemaje?
Kipa na kocha wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Idd Pazi 'Father' alisema kitendo cha klabu kongwe kutowajenga makipa wazawa kinaliweka taifa katika changamoto ya watu imara katika nafasi hiyo.
"Nikianza na Simba ilikuwa na utaratibu wa kutengeneza makipa Tanzania One kuanzia kipindi chetu, nakumbuka wakati nataka kwenda nje nilimpendekeza Mohammed Mwameja alikuwa Coastal Union, nikawa nampa nafasi akaiendeleza ile Tanzania One, naye nyuma yake akawaacha kina Juma Kaseja, nilitegemea kabla ya Aishi Manula kuondoka angemtengeza Ally Salim wakati anacheza angekuwa anamuachia nafasi mara moja moja," alisema na kuongeza;
"Simba na Yanga kwa kuwa ndizo zinazotoa wachezaji tegemeo katika timu za taifa zingeweka kipengele cha kuwapa nafasi wazawa ili wawe katika viwango, nikiangalia Aboutwalib Mshery pale Yanga ni kipa mzuri ila hapati nafasi, ukiachana na viongozi, wachezaji wenyewe wanapaswa kupambana sana ili wawashawishi makocha kuwaamini."
Mdau mkubwa wa mpira wa miguu Tanzania, Heri Chibakasa a.k.a Heri Mzozo ambaye ameibua vipaji vingi akiwa na timu ya Friends Rangers, alisema: "Simba na Yanga zijaribu kuthamini wachezaji wazawa kama inavyofanya kwa wageni, pia wachezaji wenyewe wanapaswa kujua aina ya timu hizo ni shindani muda wote."