Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga ruksa Kagame

Muktasari:

Kabla ya kauli hiyo, Serikali ilitangaza kuzizuia timu hizo kwenda kushiriki kwenye mashindano hayo kwa sababu za kiusalama hasa katika jimbo la Darfur, moja ya kituo kilichopangwa kufanyika mashindano hayo.

Dodoma/Dar es Salaam. Serikali imetoa ruksa kwa timu za Simba, Yanga na Falcon za Tanzania kushiriki Kombe la Kagame litakalofanyika nchini Sudan, huku viongozi wa timu hizo wakishangazwa na taarifa hizo.

Kabla ya kauli hiyo, Serikali ilitangaza kuzizuia timu hizo kwenda kushiriki kwenye mashindano hayo kwa sababu za kiusalama hasa katika jimbo la Darfur, moja ya kituo kilichopangwa kufanyika mashindano hayo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Amos Makala amewaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kuwa Serikali ya Tanzania imewasiliana na Serikali ya Sudan na kuhakikishiwa usalama wa wananchi wake katika michuano hiyo iliyopangwa kuanza Jumanne ijayo.

“Serikali ilikuwa na kigugumizi kuhusu ushiriki wa timu zetu za Simba Yanga na Falcon, lakini leo (jana) nimepokea Fax kutoka Serikali ya Sudan ikihakikishia usalama kwa wachezaji na Watanzania watakaosafiri na timu kwenda nchini humo,” alisema Makala.

Aliongeza: “Wametueleza mikakati yao ya jinsi watakavyotekeleza suala la ulinzi wa timu kutoka uwanja wa ndege, hotelini na kwenda uwanjani bila shida yoyote.”

Makala alisema kutokana na uhakika wa usalama, wameamua kuziruhusu timu hizo kwenda Sudan.

Alisema awali walielezwa na Chama cha soka cha Sudan na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kuwa wachezaji watasafirishwa na helikopta toka Khartoum mpaka Darfur.“Walituambia hakuna wasiwasi wa usalama, kwamba timu zote zitapewa ulinzi wa kutosha kwenda uwanjani na kurudi hotelini,” alisema Makala.

Aliongeza: “Mbali na ulinzi na usafiri wa Helikopta, pia watatoa mavazi kuzuia risasi kupenya (bullet proof), lakini sasa Serikali ya Sudan imeongeza kutuhakikishia ulinzi na usalama wa wananchi wetu, sisi tunatoa Baraka zetu zote, washiriki mashindano hayo na waje na Kombe” alisema.

Makala alisema Serikali imebeba dhamana ya Watanzania watakaoenda nchini Sudan kwenye mashindano hayo na kuzitaka timu husika kuendelea na mashindano na kuhakikisha vinakuja na kombe.

Hata hivyo wakati Serikali ikiziruhusu timu hizo kwenda kushiriki Kagame, tayari Cecafa ilishapanga upya ratiba na kuteua timu nyingine kuziba nafasi ya timu za Tanzania.

Timu hizo ni kutoka Uganda (URA), Rayon kutoka Rwanda ambazo ni timu mwanachama wa Cecafa, na timu mwalikwa kutoka nchini Chad ya Elite Sports.

Viongozi wa Simba na Yanga walipoulizwa kuhusu taarifa hizo, walisema hawana taarifa kama alivyosema Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.

Laurance Mwalusako, Katibu Mkuu wa Yanga alisema: “Klabu haina taarifa zozote kutoka Serikalini au TFF. .

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alisema: “Sina habari zozote, nipo na Waziri (Makala) Dodoma, mbona hajanijulisha lolote.”

Uwezekano wa timu hizo kwenda ni mdogo kutokana na ukweli kuwa taarifa hiyo imekuja muda mfupi kabla michuano kuanza.

Lakini pia kuna wasiwasi kama Cecafa wanaweza kuziruhusu timu hizo kwenda kwa vile tayari walishaziteua timu nyingine kuchukua nafasi za timu za Tanzania.