Simba, Yanga zapeleka timu nne CAF

SIMBA na Yanga zinahitaji ushindi tu katika mechi za klabu Afrika dhidi ya Horoya na Monastir mwishoni mwa wiki hii ili zitinge robo fainali.

Lakini kabla ya hilo kutimia, tayari timu hizo zimeshaipa neema Tanzania baada ya kuingiza timu nne kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu ujao kwa mara ya tatu mfululizo.

Kitendo cha Simba kuwepo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hadi sasa kimeihakikishia Tanzania pointi moja wakati kwa Yanga kuwepo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika hadi sasa kimeihakikishia Tanzania pointi 0.5.

Timu hizo mbili zimefanya Tanzania iwe na pointi 29 na kushika nafasi ya tisa katika viwango vya mafanikio ya nchi kutokana na ushiriki kwenye mashindano ya klabu Afrika ambavyo nchi 12 zilizo juu ndizo kila moja inapata nafasi nne za uwakilishi kwenye mashindano ya Afrika.

Katika mfumo wa ukokotozi wa kuamua idadi ya timu za kuwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa ambao unafanywa kwa kuangalia ushiriki wa misimu mitano iliyopita, alama ambazo timu inapata katika mashindano ya msimu unaoendelea zinazidishwa na tano hivyo moja ya Simba ikijumlishwa na 0.5 ya Yanga zikizidishwa kwa tano unapata pointi 7.5.

Pointi hizo 7.5 zitajumlishwa na nane (8) ambazo Tanzania ilipata msimu uliopita baada ya Simba kumaliza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, zitaongezwa na pointi 10.5 ilizopata msimu wa 2020/2021 na tatu za msimu wa 2018/2019 kufanya Tanzania iwe na pointi 29.

Tanzania kusogea hadi nafasi ya tisa katika orodha ya nchi zilizopata mafanikio kwenye mashindano ya klabu Afrika ambayo hutumika kupata nchi 12 zinazowakilishwa na timu nne, kumechangiwa pia kwa kiasi kikubwa na kutofanya vizuri pia kwa klabu kutoka nchi nyingine.

Libya ina pointi 28, Guinea ina pointi 24 huku Nigeria ikiwa ya 12 na pointi zake 20. Pointi hizo 29 za Tanzania zinaweza kuongezeka zaidi ikiwa Simba na Yanga zitatinga robo fainali ya mashindano hayo msimu huu.

Simba na Yanga zikitinga robo fainali, itaihakikishia Tanzania pointi tatu

Hapana shaka uhakika wa Tanzania kuingiza timu nne kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu ujao utazidi kuongeza ushindani wa kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hasa ya tatu na ya nne.

Hiyo ni kutokana na matakwa ya kikanuni ambayo yanatoa fursa kubwa kwa timu zilizofanya vizuri kwenye ligi kushiriki mashindano ya kimataifa kulinganisha na zile za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu msimu huu, kama Tanzania inapata fursa ya kuingiza timu nne kwenye mashindano ya kimataifa, ni bingwa tu wa Kombe la Shirikisho la Azam ndiye anayepata fursa ya kuwakilisha nchi kwenye mashindano hayo na nafasi nyingine tatu zinaenda kwa washindi watatu wa ligi.

“Iwapo Klabu Bingwa ya Ligi Kuu ndiye pia Bingwa wa Kombe la Shirikisho la TFF, mshindi wa pili wa Ligi Kuu atawakilisha Tanzania Bara kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la CAF (CAF Confederations Cup).”

“Uteuzi wa Uwakilishi wowote wa Mashindano yoyote ambao msingi wake unatokana na Ligi Kuu utafuata ubora wa nafasi ya timu husika katika msimamo wa Ligi Kuu,” inafafanua kanuni ya nane ya Ligi Kuu msimu huu.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya alisema Simba na Yanga zimeipa heshima nchi.

“Watanzania tuziombee Yanga na Simba ili zifanye vizuri na kuzidi kuibeba nchi. Tunahitaji kuwa na uwakilishi wa timu nyingi kwenye hayo mashindano,” alisema Nyambaya.