Simbu, Gisemo wabeba dhamana ya Tanzania Japan
Muktasari:
Aprili 21, mwaka huu, Simbu alishinda medali ya shaba baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston Marathon.
Tanzania itawakilishwa na wakimbiaji wawili pekee, Aphonce Simbu na Josephat Gisemo katika mashindano ya Dunia ya Riadha yatakayofanyika kuanzia Septemba 13 mwaka huu Tokyo, Japan.
Awali, Tanzania ilitarajia kupeperusha bendera yake kwa wanariadha wanne, lakini mipango hiyo ikayumba baada ya bingwa wa marathoni wa Wanawake, Magdalena Shauri na Failuna Abdi Matanga, kushindwa kushiriki kutokana na kuchelewa kupima vipimo vya jinsia vinavyohitajika na Shirikisho la Riadha la Dunia (WA).
Simbu anarudi Tokyo akiwa na kumbukumbu ya kumaliza nafasi ya saba kwenye Olimpiki 2020 kwa muda wa saa 2:11:35, lakini zaidi akiwa na historia ya kutwaa medali ya shaba kwenye mashindano ya Dunia ya mwaka 2017 London Uingereza akitumia 2:09:51.
Nyota huyo kutoka timu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), anakwenda Japan na rekodi ya 2:04:38 kutoka Valencia marathon mwaka jana pia nafasi ya pili Boston marathon kwa 2:05:04 Aprili mwaka huu.
Gisemo wa Jeshi la Polisi anaingia Tokyo kwa mara ya kwanza, akiwa anabebwa na muda wa saa 2:10:23 alioupata Geneva marathoni, Uswisi mwaka jana, na anachukuliwa kama kadi mpya ya ushindi kwa Tanzania.
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Stephen Akhwari, amesema mashindano hayo ni sawa na Kombe la Dunia la Soka kwa sababu yanakusanya wakimbiaji bora kabisa duniani, lakini anaamini Simbu na Gisemo wanaweza kuwapa furaha nyingine.
Akhwari, aliyewahi kushiriki mashindano matano ya Dunia kati ya mwaka 2001 hadi 2009 katika mbio za mita 5000 na 10,000 aliongeza kuwa maandalizi ya mwisho ya wanariadha hao ni lazima yazingatie umakini.
“Huu sio muda wa mazoezi magumu, huu ni muda wa kupumzika na kujiweka sawa kisaikolojia kabla ya vita halisi”, amesema Akhwari.
Mwanariadha wa zamani wa Kimataifa, Zakia Mrisho, ambaye ameshiriki mbio hizo kuanzia 2003 hadi 2011 akikimbia mita 5000 naye ameweka bayana matumaini yake kwa nyota hao akiamini kutokana na maandalizi wanayoendelea kufanya watarudi na medali.
“Naamini Simbu na Gisemo wanaweza kutupa historia mpya ukizingatia Simbu alitupa medali ya shaba mwaka 2017”, amesema Mrisho.
Tanzania inajivunia medali mbili pekee tangu ilipoanza kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 1983 Helsinki Finland ikiwakilishwa na baadhi ya nyota akiwemo Gidamis Shahanga, Zakaria Barie na Abraham Mikumi.
Medali ya kwanza ni ya fedha ambayo ilipatikana mwaka 2005 huko huko Helsinki Finland kupitia kwa Christopher Isengwe ambaye alimaliza wa pili mbio ndefu akitumia saa 2:10:21.
Nyingine ni ya shaba kutoka kwa Alphonce Simbu mwaka 2017 London, Uingereza akitumia 2:09:51.