SIO ZENGWE: Mgunda na ile 'kiwango chake kimeishia hapo'

Kocha wa Simba, Juma Mgunda

MWAKA 1998, Tito Mwaluvanda aliiongoza Yanga kuichapa Coffee ya Ethiopia mabao 6-1 na hivyo vigogo hao wa Tanzania kuwa moja ya timu nane zilizofuzu kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika ambayo kwa mara ya kwanza ilichezwa kwa mtindo wa ligi na katika makundi.

Lakini ushindi huo ukawa mwisho wa kocha huyo mzawa kuifundisha Yanga; alionekana kiwango chake kimeishia hapo hivyo ni lazima atafutwe kocha mgeni anayelingana na ukubwa wa hatua hiyo.

Yaliyotokea katika mechi za makundi hayafai kukumbusha.

Miaka michache baadaye, John Simkoko akaiongoza Mtibwa kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza Kombe la Shirikisho. Uongozi wa Mtibwa Sugar ukaona kiwango cha kiungo huyo wa zamani kimeishia katika kufuzu. Ukawa mwisho wa kocha huyo na hivyo Raoul Shungu akachukuliwa kuinoa timu hiyo ambayo haikuwa na utamaduni wa kuajiri wageni.

Mtibwa ikaishia raundi ya awali baada ya kupigwa nje ndani na Cotonsport ya Cameroon.

Ukiacha hayo, Fred Felix Minziro amekuwa muathirika wa imani hiyo hadi Geita Gold walipoamua kuweka imani yao kwake na ameiongoza timu hiyo katika mechi za Kombe la Shirikisho kinyume cha matarajio ya wengi yaliyojengwa juu ya imani isiyo na misingi. Minziro alikuwa amejengewa imani kwamba ‘eti’ ni mtalaamu wa kupandisha timu daraja hadi Ligi Kuu. Akishasfanya kazi hiyo nzito, ama hupumzishwa au huondolewa na timu kupewa mtu mwenye utalaamu unaolingana na ukubwa wa Ligi Kuu.

Hata Simba ilipokuwa inahitaji matokeo mazuri nchini Misri dhidi ya Zamalek, ilimuongeza Talib Hilal kwa wiki moja kule Cairo na ilipofanikiwa kuwatoa Waarabu kwa penalti, sifa hazikwenda kwa yule kocha Mkenya, James Siang’a aliyeiongoza tangu ligi ya ndani hadi kufikia hatua ya 16 bora na kucheza mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam.

‘Kiwango chake kimefikia mwisho’ ndiyo imani inayojengwa baada ya timu kufikia hatua fulani na ndiyo kauli inayowanyima fursa makocha wazawa wengi kupata uzoefu wa ugumu wa mechi za kimataifa ili waongeze ujuzi wao na kuwa bora zaidi.

Ni makocha wachache wazawa ambao walionekana nje wakaitwa kwenda kufundisha, akiwemo Sunday Kayuni ambaye aliweza kuiongoza AFC Leopards na Bandari. Wako kina Mansour Magram ambao mara kadhaa waliitwa Arabuni, hasa kuifundisha Fanja, Charles Boniface Mkwasa na Dan Korosso aliyekwenda Botswana miaka mingi iliyopita.

Leo hii Pitso Mosimane anafundisha Saudi Arabia katika klabu ambayo Jose Mourinho anaweza kuitwa, au Pep Guardiola, au Frank Lampard na wengine ambao huwa tunawashuhudia kwenye runinga jioni kila mwisho wa wiki.

Mosimane aliaminiwa na Mamelodi Sundowns akaiongoza hadi kutwaa kombe la Ligi ya Mabingwa na baadaye kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia. Leo hii ni kocha mwenye heshima kubwa barani Afrika na sehemu ya ukanda wa dunia.

Hii pia iko kwa makocha kama Florent Ibenge, ambaye aliaminiwa na Vita FC na kupata nafasi ya kuonekana hadi kwenda kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika. Sasa amekuwa msafiri barani Afrika. Ikijulikana hana timu tu, klabu kibao zinaanza kumsaka kwa kuwa ameshajijengea jina baada ya kupata fursa ya kufundisha timu katika michuano ya Afrika.

Hata katika timu za taifa, ni nadra wazawa kuaminika kikamilifu, ingawa angalau huku kuna wengi waliopewa nafasi lakini kutofanya vizuri kukasababisha waondolewe bila ya kujali mazingira yaliyowafelisha. Lakini Senegal wameonyesha imani kubwa kwa kocha wao Aliou Cisse. Hata pale aliposhindwa kufanya vizuri, bado walimuachia jukumu hilo hadi akafanikiwa kuirudisha nchi hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Nchi za Kiarabu zina utamaduni huo wa kuamini wazawa. Mara kadhaa klabu za Misri, Morocco, Algeria na Tunisia huongozwa na makocha wazawa ingawa pia huajiri wageni. Makocha hao wametapakaa ukanda wao kwa kuwa wameshaonyesha uwezo Afrika.

Kwanini si Tanzania? Leo hii viongozi wa Simba wanaona ufahari kuzungumzia maombi yaliyopo mezani kwao kutoka kwa makocha wa nje ya nchi. Yaani anachofanya Juma Mgunda hakina thamani sana kwa kuwa walishaweka akilini kuwa baada ya Zoran Maki kuondoka, ataajiriwa koicha mwingine mgeni.

Mara kadhaa msemaji wa Simba amekuwa akizungumzia mipango ya kuajiri kocha mwingine bila ya kujali kauli zake zinaweza kuathiri vipi saikolojia ya Mgunda kuelekea kwenye mechi, na hata wachezaji ambao wameonyesha kumkubali kwa kwenda kumkumbatia wanapopata matokeo mazuri.

Sitaki kusema kwamba Simba isitafute kocha mwingine au isitafute mgeni, lakini ile imani kwa-mba makocha wazawa hawawezi kuimudu michuano mikubwa ya Afrika haina budi kuanza kuepukwa na kuangalia kinachoendelea sasa uwanjani.

Naanza kuona tofauti ndogo sana kati ya kocha mgeni anayeletwa na klabu za Tanzania dhidi ya mgeni mwingine. Na kwa kile anachokifanya Mgunda sasa uwanjani, sioni tofauti hata na hao wageni.

Kwa misimu miwili, Simba imekuwa ikipata matokeo mabaya ugenini kutokana na makocha wote kwenda huko na kucheza kwa kujiamini, kutoheshimu wapinzani. Ikicheza na Kaizer Chiefs, Simba ilishambulia tangu dakika ya kwanza hadi ya mwisho; ikalala 4-0.

Vivyo hivyo zile mechi za tano-tano. Lakini Mgunda alikuwa na woga wa maana alipocheza na Primero D’Agosto, akiwaagiza wachezaji wake watulie nyuma na kushambulia kwa kushtukiza. Kikosi alichokipanga kilikuwa na nidhamu ya kimbinu na akapata matokeo mazuri.

Ndio kuna kasoro anaweza kuwa amezionyesha, ambazo hata Pablo, Nabi na Maki wanazo. Hizi hazitoshi kumfanya asiaminiwe. Kama huwa tuna imani kwa wageni hata wanapofanya makosa, kwanini hatuvumilii ya wenyeji?

Tunahitaji kina Pitso Mosimane kutoka Tanzania, kina Florent Ibenge kutoka Tanzania, kina Benni MCarthy kutoka Tanzania. Lakini hawa hawawezi kupatikana bila kwanza kuaminiwa na klabu za ndani.

Makocha nao hawana budi kujijengea chapa, siku hizi wanaita brand. Wawe na mahitaji ya kiufundi katika makubaliano yao. Wageni wakija hutafutiwa wataalamu mbalimbali; wa takwimu, wa makipa, wa misuli na maeneo mengine. Wazawa huenda peke yao wasijue msaidizi atakuja nani na hata suala la wataalamu wa maeneo mengine kama golini, ulinzi na ushambuliaji kwao huwa si kitu.

Wanachojali ni mkataba. Lakini masuala hayo mengine yanaweza kuwasaidia zaidi kiufundi na kujenga jina na heshima yao. Badala ya kuponda kwamba Ten Hag hawezi bila ya MCarthy, tuone umuhimu wa kocha wa kikosi cha kwanza.