SIO ZENGWE: Motsepe ajisafishe na bao la Aziz Ki

Muktasari:

  • Mwishoni timu hizo zilishindwa tena kufungana na mchezo huo kuamulia kwa ‘matuta’ ambazo wenyeji walishinda kwa penalti 3-2, hivyo Yanga kuyaaga mashindano hayo kwa uchungu.

NI ajabu kwamba baadhi ya wachambuzi wameibuka na kudai kuwa mfumo wa Refa Msaidizi wa Video (V.A.R) ulionyesha mpira uliopigwa na Stephane Aziz Ki katika dakika ya 59 haukuvuka mstari wa lango na hivyo Yanga hawakustahili bao hilo katika mchezo wao wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns uliofanyika Ijumaa jijini Pretoria.

Mwishoni timu hizo zilishindwa tena kufungana na mchezo huo kuamulia kwa ‘matuta’ ambazo wenyeji walishinda kwa penalti 3-2, hivyo Yanga kuyaaga mashindano hayo kwa uchungu.

Kwa kawaida waendeshaji wa mfumo huo hutakiwa kuwapa watangazaji wa mchezo picha za marudio zinazoonyesha tukio kutoka pande zote na pale panapostahili picha zigandishwe au kutembea taratibu hufanya hivyo ili si tu mwamuzi aone kwa usahihi zaidi, bali hata watazamaji wa mechi wadhihirishiwe na hivyo uamuzi kuwa wa uwazi.

Lakini hakuna picha za marudio za mfumo huo zilizoonyeshwa kwenye runinga katika tukio hilo zaidi ya zile za marudio za shirika lililopewa haki ya kurusha moja kwa moja matangazo ya mchezo huo na ambalo linaweza kuwa na kamera za kutosha au pungufu.

Kibaya zaidi, refa msaidizi aliyekuwa anasimamia mfumo huo, hakumtaka mwamuzi wa kati aende kwenye runinga iliyokuwa uwanjani kujiridhisha kuwa mpira huo haukuvuka kama walivyowasiliana naye.

Mfumo wa V.A.R ni tofauti na teknolojia ya mstari wa goli (goal line technology) ambao haumpi mwamuzi nafasi ya kujiridhisha iwapo kuna utata kuhusu mpira kuvuka mstari wa goli, na badala yake refa hutumiwa ishara ndani ya sekunde kumi kumtaarifu kuwa mpira ulishavuka mstari.

Mwamuzi wa mchezo wa Ijumaa hakutumiwa taarifa na teknolojia hiyo na pengine haikuwa imefungwa kwenye uwanja huo wa Loftus Versfeld, badala yake alisimamisha mchezo wakati kipa alipouwahi mpira uliokuwa unaelekea nje ya uwanja baada ya kuokolewa na beki wake katika tukio hilo.

Kitendo cha refa kusimamisha mpira kilimaanisha kuwa alishakubali bao, lakini akataka kwanza kusikiliza maoni ya refa msaidizi wa video kama kanuni za V.A.R zinavyosema kuwa ni lazima kwanza kuwepo na uamuzi uliofanywa na refa na ndipo teknolojia hiyo itumike ili kuthibitisha uamuzi wa refa au kuonyesha kuwa haukuwa sahihi.

Baada ya kuwasiliana na refa msaidizi wa video (V.A.R), Jerson Dos Santos, refa wa kati Dahane Beida ama alikubaliana na msaidizi huyo kuwa mpira haukuvuka mstari wa goli, au alipuuza ushauri wake kuwa mpira ulishavuka lakini yafaa ajiridhishe mwenyewe kwenda kuangalia runinga iliyopo uwanjani na hivyo kuamua kuendelea na mchezo kwa kudunda mpira.

Imekuwa ajabu kwamba refa huyo kutoka Maurtania amekaririwa akisema kuwa hastahili kushtumiwa bali lawama hizo zielekezwe kwa mwamuzi msaidizi ambaye anadai alimthibitishia kuwa mpira haukuvuka mstari wa goli na hivyo aendelee na mchezo.

Kanuni moja kuu ya mpira wa miguu ni kwamba uamuzi wa refa ndio wa mwisho. Ni ajabu kwamba Beida anasukumia lawama kwa V.A.R wakati mwamuzi msaidizi wa video hutoa ushauri na pale anapoona utata sana, kumshauri mwamuzi ajiridhishe mwenyewe. V.A.R anaweza kumwambia mwamuzi wa kati aendelee na mchezo pale tu kunapokuwa hakuna utata wowote, kwa mujibu wa kanuni za V.A.R.

Tukio la Ijumaa ni tukio jingine lililoleta fedheha kwa mchezo wa mpira wa miguu barani Afrika katka zama ambazo teknolojia imerahisisha sana uamuzi na imeongeza uwazi ambao unatuliza mashabiki kutokana na kuona uhalisia wa matukio mbalimbali kwa kutumia televisheni.

Na kibaya zaidi timu iliyonufaika na makosa hayo ya waamuzi ni ile inayomilikiwa na rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kitu kinachojenga fikra kuwa huenda waamuzi walipokea maelekezo kutoka juu kutokana na Mamelodi kuhitaji sana kufika hatua za juu za Ligi ya Mabingwa ili kujiongezea pointi zitakazoiwezesha kupata pointi nyingi na hivyo kufuzu kucheza Klabu Bingwa ya Dunia, michuano iliyoboreshwa kwa kuongeza idadi ya timu na fedha.

Hisia pia zinaweza kuwa waamuzi hao walichezesha kwa hofu kuwa watashughulikiwa iwapo wataikatili timu ya bosi wao au woga tu kwamba Mamelodi ni timu ya rais wa Shirikisho la Soka Afrika.

Mara nyingi ni ngumu kuthibitisha hayo mapema na kama yanathibitishwa ni baada ya muda mrefu na hivyo ni vigumu kupindua matokeo na kuamuru mchezo urudiwe.

Lakini kilicho dhahiri ni kwamba kwa mara nyingine mpira wa Afrika umepata dosari ambayo ingeweza kuepukika kama wahusika wangeonyesha uwajibikaji wa hali ya juu.

Mechi za kuanzia robo fainali ni sehemu ya mechi muhimu za mashindano yoyote yale na ndio maana hatua ya makundi haikuwa na matumizi ya V.A.R kwa sababu teknolojia hiyo ni ghali na hivyo CAF wanaona ni bora wabebe gharama hizo katika hatua za mwisho ambazo huhusisha mechi chache.

Pamoja na CAF kuamua kubeba gharama hizo, bado mwamuzi wa kati haoni haja ya kuitumia kikamilifu ili kuliepusha shirikisho lake na aibu au lawama zozote, tena katika moja ya matukio muhimu ya mchezo ambayo teknolojia hiyo ya V.A.R ndiyo imejikita zaidi.

Awali, V.A.R ilikuwa inafungwa viwanjani, lakini haitumiki pale inapohitajika kama ilivyokuwa kwa mchezo wa Simba na Orlando Pirates, lakini kichefuchefu zaidi kikawa wakati wa fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Esperence ya Tunisia na Wydad Casablanca wakati mwamuzi aliposhindwa kujiridhisha uamuzi wake kwa kuangalia runinga ya V.A.R kuhusu tukio lililotokea dakika ya 58.

Wachezaji wa Wydad walichukizwa na tukio hilo na wakaamua kutoka uwanjani na hivyo mchezo huo kuvunjika katika dakika ya 58 huku Esperence wakitangazwa kuwa mabingwa.

Hiyo ilikuwa ni fedheha kubwa inayosababisha kila mara timu kutoka Afrika Kaskazini kuomba mechi zao zichezeshwe na waamuzi kutoka nje ya bara la Afrika.

Lawama na fedheha kama hizi hazistahili kuendelea katika soka la Afrika ambalo limeanza kupata wawekezaji wa uhakika wanaoweza kuupeleka mpira huu mbali zaidi ikiwa utatawaliwa na uwazi na haki.

Kwa maana hiyo, CAF wanatakiwa kukomesha uozo huu na kulisafisha soka la Afrika ili livutie wawekezaji zaidi na kuwapa imani zaidi mashabiki ambao katika baadhi ya viwanja wamekuwa adimu, pengine kutokana na kutoridhishwa na uendeshaji wa mchezo huu maarufu duniani.

Ni muhimu sana kwa rais wa CAF, Patrice Motsepe na timu yake kuchukulia suala hili kwa umuhimu zaidi kuliko hata hayo mambo ya kuanzisha mashindano mengine wakati bado bara linasuasua katika mambo muhimu ya uamuzi.

Tukio hilo linamuhusu zaidi Motsepe kama rais na kama mmiliki wa Mamelodi, ambaye amekuwa akifanya jitihada kubwa kuileta Ligi ya Mpira wa Miguu ya Afrika (AFL) na hata kupigia debe kupanuliwa kwa mashindano ya Klabu Bingwa ya Dunia.

Lakini pia linamuhusu Motsepe kama mmiliki wa Mamelodi Sundowns ambayo imenufaika na ubovu ama wa makusudi ama wa kizembe wa waamuzi waliochezesha mchezo huo.

Ili kujisafisha, Motsepe hana budi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na ukweli kuweka bayana badala ya jumba bovu kumuangukia au kuwaangukia waamuzi pekee.