SIO ZENGWE: Yanga iliingia katika mageuzi na dosari

Muktasari:
- Na katika kuonyesha serikali yake imepania kuhakikisha katiba mpya inaandikwa, Rais Jakaya Kikwete aliwahi kunukuliwa akisema Watanzania, hasa wana-CCM wenzake hawana budi kujiandaa kisaikolojia kwa kuwa maoni ya wananchi yanaweza kwenda tofauti na matarajio yao.
Wakati Serikali ya Awamu ya Nne iliporidhia kuandika katiba mpya inayoendana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961, Watanzania walifurahi sasa kuna nia ya dhati ya kuondoka hapa tulipo na kujenga utamaduni mpya utakaoongozwa na nyaraka ambayo imeshirikisha kila sehemu ya jamii.
Na katika kuonyesha serikali yake imepania kuhakikisha katiba mpya inaandikwa, Rais Jakaya Kikwete aliwahi kunukuliwa akisema Watanzania, hasa wana-CCM wenzake hawana budi kujiandaa kisaikolojia kwa kuwa maoni ya wananchi yanaweza kwenda tofauti na matarajio yao.
Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ilipomaliza mchakato wa kukusanya na kuchambua maoni ya wananchi na kuandika Rasimu ya Katiba, mpira ulirushwa kwa Bunge la Katiba ambalo lilitakiwa kutoa nyaraka ya mwisho ambayo ingetoa Katiba Pendekezwa ambayo ingepigiwa kura ya maoni kukubaliwa au kukataliwa.
Lakini mpira ulikwamia hapo. Mfarakano uliotokea ndani ya Bunge la Katiba hadi baadhi ya wajumbe kujitoa na kususia mchakato huo, ulitosha kukwamisha nia njema ya kuandika makubaliano ya kusimamia uendeshaji wetu wa nchi.

Katika kutafakari, ilionekana mchakato ulishapata matatizo tangu awali. Ama Bunge la Katiba lisingeundwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi ama wajumbe hao wangewekewa sheria ambayo ingewazuia kugombea nafasi zao hadi baada ya kipindi cha miaka mingi.
Yaani kuchukua wajumbe wengi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano na Wawakilishi na kuwajumuisha pamoja na wajumbe wachache kutoka taasisi za kijamii na nyinginezo, kulimaanisha wanasiasa hao kuwa na nguvu zaidi ya wajumbe wengine na hivyo kukikamata chombo hicho muhimu. Ndivyo ilivyokuwa. Wajumbe walitumia muda mwingine kuonyesha nguvu yao kisiasa kuliko kufikiria watu waliokuwa wakiwatungia katiba.

Bila ya kuweka sheria ya kuwazuia wajumbe kutetea nafasi zao au zile za juu, maana yake akili za wajumbe wa Bunge la Katiba ingejikita zaidi kwenye masilahi binafsi kuliko ya taifa. Ndivyo ilivyokuwa. Mijadala mingi haikuwa na afya zaidi ya kulinda masilahi binafsi hadi yale ya kiwango cha chini cha elimu kwa mgombea ubunge.
Kwa hiyo, mabadiliko ya katiba kuhusu uendeshaji wa chombo chochote cha kijamii, ni muhimu sana yakaangalia mambo mengi, ikiwa ni pamoja na wanaofanya maamuzi na wanaopewa jukumu la kusimamia mabadiliko hayo.
Klabu ya Yanga inajinasibu imebakiza sehemu ndogo kumalizia mabadiliko ya muundo na umiliki wa klabu yaliyoanzishwa na Kocha Mshindo Msolla wakati akiwa rais wa klabu hiyo.
Mabadiliko hayo yalifanywa kwa kubadili katiba ambayo iliruhusu kuwe na bodi na kutaja aina ya watu watakaoingia kwenye chombo hicho, yaani wajumbe watano kutoka klabu na wanne kutoka kwa wawekezaji ambao watanunua asilimia 49 ya hisa za umiliki wa klabu.
Pia yalibadili muundo wa mkutano mkuu, kurejesha nafasi ya rais na kupunguza idadi ya wajumbe wa kamati ya utendaji. Lakini mchakato wa mabadiliko haukuunda chombo cha kuyasimamia na kuyaongoza kwa mujibu wa makubaliano ambayo yangewekwa na mkutano mkuu.
Badala yake uchaguzi uliofanyika baada ya muda wa Dk. Msolla kuisha ukaingiza viongozi wapya, ambao baadhi walikuwa kwenye mchakato wa mabadiliko na hivyo hao ndio wameshika mchakato huo na wanaamua jinsi watakavyo kwa kuwa haikuwekwa sheria ya kuyaongoza na muda wa kuyahitimisha ili kuwa na Yanga mpya.
Mwezi Aprili, Rais wa Yanga, Hersi Said alitangaza kamati ya wajumbe wanne aliosema watakuwa na kazi rahisi ya kumalizia mchakato huo, ikiongozwa na Alex Mgongolwa.
Hata hivyo, kumekuwa hakuna taarifa zozote za maendeleo ya kumalizika kwa “sehemu ndogo” iliyosalia, lakini si wengi wanaohoji kwa sababu klabu hiyo imekuwa ikipata matokeo mazuri uwanjani yanayosababisha yeyote anayehoji apuuzwe, akiwambiwa “tunachotaka ni ushindi”.
Katika kipindi hicho, Yanga imetwaa ubingwa wa Bara mara tatu mfululizo na kuondoa unyonge wa miaka minne uliotawaliwa na mtani wake wa jadi, Simba SC.
Haya ni matokeo ambayo yamewafanya viongozi wa sasa wakae kwa Amani, wasionekane kutishika na ahadi kibao za mabadiliko na maendeleo kama ujenzi wa uwanja pale Jangwani na uundwaji wa kampuni inayotajwa kwenye katiba mpya.

Haya yote yasingekuwa mepesi kama kungekuwa na sheria inayoongoza mabadiliko na yenye muda wa kuyamaliza. Pamoja na kutafuta matokeo mazuri ya uwanjani, viongozi wangejikita kuhakikisha muda waliopewa na sheria wa kukamilisha mabadiliko unakaribia kuisha.
Sheria pia ingezuia baadhi ya maamuzi makubwa kufanyika hadi bodi itakapoundwa kwa ajili ya kuwakilisha masilahi ya wanahisa, ambao ni klabu na wawekezaji ambao wanatakiwa kumiliki asilimia 49 ya hisa.
Lakini tayari kuna ahadi ya ujenzi wa uwanja, ambayo kimsingi ingepitishwa na chombo maalum kama bodi ya wakurugenzi baada ya kushawishiwa na mkakati wa ujenzi, vyanzo vya mapato kwa ajili ya kugharimia ujenzi huo na mambo mengine na baadaye kupata ridhaa ya wanahisa.
Hata suala la kuacha rangi asilia ya klabu katika jezi tatu zitakazotumiwa na Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, lilitakiwa lijadiliwe kwa makini na chombo kama bodi kabla ya kushushwa kwa sekretarieti kwa ajili ya utekelezaji.
Lakini suala hilo limegeuzwa kama ni dogo sana na sekretarieti imeachiwa iwajibu wanaohioji kwa mizaha, wakati ni kitu muhimu katika utamaduni wa klabu yuoyote duniani. Asili ni asili haiachwi kimizaha mizaha.
Ukianza kuona mambo makubwa yanachukuliwa kimizahamizaha ujue liko kubwa Zaidi litafanywa kwa njia hiyo na litatetewa kwa kejeli kana Wana-Yanga ni majuha.

Nani atawazuia viongozi kufanya maamuzi makubwa yanayoweza kuondoa asili ya Yanga? Hakuna kwa sababu wameshika hatamu kama hali ilivyokuwa kabla ya mchakato wa mabadiliko kuanza. Yaani viongozi wana mamlaka kamili kwa sababu walichaguliwa kihalali, hata kama walichaguliwa katikati ya mchakato unaoitengeneza Yanga mpya.
Yaani vionghozi ndio wana dira na wanaitafsiri vizuri dira ya mabadiliko hayo na inapobidi wanaweza kuamua lolote kwa kuwa hawabanwi na sharia yoyote ya mabadiliko ya katiba.
Kwa maana hiyo, wanaweza kuwa wanaendesha mabadilioko hayo kwa kuangalia maslahi yao na si maslahi mapana ya klabu. Kwa hiyo kuna haja ya ama viongozi kuwajibika zaidi kwa wanachama walioridhia kufanya mabadiliko kwa kumalizia hatua zilizobaki bila ya kuweka mbele ubinafsi.
Viongozi wa sasa ni sehemu ya mabadiliko na hivyo waonyeshe kuwa wanawajibika kwa mabadilko na hatua za mabadiliko zinaonekana.
Pengine msomaji anaweza kujiuliza huyu kaibukia wapi mpaka anarejea mwanzo wa mabadiliko? Kwangu mimi mtu anayefanya jamb o kubwa kimzahamzaha, anawaandaa watu kwa jambo kubwa Zaidi litakalofanyika kimzahamzaha na watakapokuja kuzinduka, litakuwa limeshafanyika.
Ukianza kutetea rangi asili iliyoachwa katika jezi tatu za michuano ya klabu bingwa ya Afrika, yaani rangi ya njano iliyoachwa na kutumika ya dhahabu, unaona kabisa mizaha imeanza kufanyika katyika jambo kubwa.
Ukiona matawi maarufu kama la Mwembe Yanga yamefutwa eti kwa sababu hayajatimiza wanachama 100, unajua tunataka kusahau historia mapema. Kama Wales, England, Scotland na Ireland ya Kaskazini zimepewa uanachama Fifa kwa sababu ya umuhimu wake katika historia, kwa nini matawi yenye historia yafutwe. Tunaifuata hiostoria ipi?
Na hapo ndipo unapokumbuka kumbe Yanga iliingia kwenye mabadiliko bila ya kuwa na tahadhari kwa wajumbe waliokuwa na maslahi binafsi, na bila ya kuwa na sheria ya kuongoza mabadiliko, kutoithamini historia hali kadhalika kutokuwa na kamati ambayo ingeratibu mabadiliko hayo kisheria huku uongozi wa klabu ukiendelea na shughuli za kimichezo.
Bila ya hivyo, utaonyeshwa matokeo mazuri ya uwanjani na kuelezwa kuwa yanatokana na mabadiliko hayo kana kwamba huko nyuma Yanga haikuwahi kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo na kumgeuza mtgani wao kuwa mteja hata bila ya kuwa na mageuzi.
Hili ni fundisho kwa wengine wengi wanaofanya mabadiliko na ndio maana hata upande wa pili nako wanasuasua kumalizia mageuzi hayo ambayo kwa kweli kama yangefanikiwa kwa Simba na Yanga yangeleta sura mpya katika soka la Tanzania.
Unapomaliza kusoma usikumbuke matokeo ya Yanga ya mechi nne zilizopita; zinaweza kukuchanganya ukapoteza uelewa wako wa shauri hili.