Siri imefichuka muonekano wa viatu vya Olise uwanjani
Olise uvaa wake wa viatu vya soka huhakikisha vinaendana kikamilifu na rangi ya jezi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Tofauti na wachezaji wengine, Olise ameonekana kuwa na aina yake ya uvaaji wa viatu vya soka ambao umekuwa wa kipekee uwanjani.a
Imekuwa ni kawaida kwa wachezaji maarufu kupata udhamini wa vifaa vya michezo wa kampuni mbalimbali duniani ili kuhakikisha nyota hao wa soka wanaitangaza chapa yao pale wanapokuwa kwenye viwanja vya michezo.
Nahodha wa Inter Miami, Lionel Messi anayedhaminiwa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidasi. Picha na Mtandao
Nyota kama Lionel Messi amekuwa anatumia viatu vya soka vya kampuni ya Adidas wakati Cristiano Ronaldo akifanya hivyo kwa viatu vya kampuni ya Nike, pia hata nyota chipukizi wameonekana kuingia katika mikataba ya udhamini huo ambayo imekuwa ikiwalipa fedha ndefu ukiachana na mishahara wanayolipwa na Klabu.
Kinda wa Barcelona, Lamine Yamal ambaye ni balozi wa kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas . Picha na Mtandao
Kinda anayechipukia kama Lamine Yamal wa Barcelona ni mmoja ya wanufaika wanaoingiza kiasi kikubwa cha fedha kutoka Adidas vilevile yupo kinda mwingine wa PSG, Désiré Doué ambaye anaudhamini huo kutoka Nike.
Lakini hali imekuwa tofauti kwa nyota wa Bayern Munich, Michael Olise, ambaye anaendelea kuvutia macho ya watazamaji ndani ya uwanja kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kuvaa viatu vya soka, huku siri yake ya uvaaji ikiwa imefichuka.
Nyota wa Al Nassr, Cristiano Ronaldo anayedhaminiwa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike. Picha na Mtandao
Tofauti na wachezaji wengine, Olise hana mkataba wowote wa kudhaminiwa na kampuni za vifaa vya michezo kama Nike au Adidas. Hali hiyo inampa uhuru wa kuchagua aina yoyote ya viatu anavyotaka kuvaa, jambo ambalo limekuwa nadra kwa wachezaji wa kiwango cha juu.
Inaelezwa kuwa makampuni makubwa ya uuzaji wa vifaa vya michezo kama Adidas na Nike yamekuwa yakitamani kumdhamini nyota huyo katika kuwatangazia bidhaa zao kupitia uvaaji lakini yamegonga mwamba kwani Olise hayupo tayari kufanya hivyo huku sababu kubwa ikiwa ni kujali mtindo wake binafsi wa uvaaji.
Moja ya mbinu zake za uvaaji ni kuhakikisha viatu vyake vinaendana kikamilifu na rangi ya jezi ambapo mara nyingi ameonekana akivaa viatu vyeusi pale timu yake ikiwa na jezi nyeusi na viatu vyekundu wakati timu yake ikiwa na jezi nyekundu.
Mtindo huu wa uvaaji umemfanya nyota huyo wa soka kuonekana tofauti na wachezaji wengine anapokuwa uwanjani jambo linalowafanya hata mashabiki kumtambua kwa wepesi zaidi kwani amekuwa akifanya hivyo tangu alipokuwa na Crystal Palace.
Olise mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akipendelea kutumia viatu vya modeli za zamani za Adidas F50 Tunit za mwaka 2008 pamoja na Nike Hypervenom III, akitanguliza zaidi mtindo wake binafsi wa uvaaji badala ya kukimbizana na mitindo mipya inayotangazwa sokoni.
Hata hivyo, licha ya Staa huyo kuwa anavaa viatu vya makampuni ya Adidas na Nike, huwa anavipaka rangi maalumu ili kuhakikisha viatu vinaendana na rangi ya jezi alizovaa na kwa kufanya hivyo rangi inayopakwa kwenye viatu huficha nembo za kampuni husika na ndiyo sababu ya kutotaka kudhaminiwa kwani endapo akifanya hivyo atalazimika kuacha mtindo wake wa uvaaji ili nembo ionekane kwa watazamaji.
Nyota wa Bayern Munich, Michael Olise. Picha na Mtandao
Kwa mtazamo wake, muonekano wa uwanjani ni sehemu muhimu ya utambulisho wa mchezaji, hivyo hulenga kuleta mvuto wa kipekee kwa kuhakikisha kila kitu anachovaa kinaendana vizuri.
Olise alizaliwa England lakini alichagua kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa kwa sababu ilikuwa ni ndoto yake kuja kuichezea timu hiyo tangu alipokuwa mdogo na hata kabla ya kuanza kucheza katika kikosi cha wakubwa, nyota huyo amewahi kuiwakilisha Ufaransa katika timu za watoto.
Nyota huyo alizaliwa London kwa wazazi wake Vincent Olise ambaye ni Baba yake mwenye asili ya Nigeria na Katherine Olise huyu ni Mama yake mwenye mchanganyiko wa asili ya Ufaransa na Algeria.
Nyota wa Bayern Munich, Michael Olise wakati alipokuwa na Crystal Palace. Picha na Mtandao
Olise aliwahi kuzichezea timu kadhaa za akademi za Arsenal ambako alianza kucheza akiwa bado na umri mdogo na mwaka 2009 alihamia kwenye akademi ya Chelsea ambako alicheza kwa miaka saba kutoka 2009 hadi 2016 kisha akajiunga na akademi ya Manchester City hadi 2017.
Michael Olise wakati alipokuwa katika akademi ya kukuza vipaji ya Man City. Picha na Mtandao
Baada ya kuondoka Man City, Olise alitimkia katika akademi ya Reading ambako alifanya makubwa katika ligi ya Championship akiwa na umri wa miaka 19 na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora Kijana wa EFL msimu wa 2020/2021 na kiwango hicho kilivutia vilabu vingi vya Ligi Kuu England vilivyotamani kumsajili na Crystal Palace ndio waliokuwa wepesi zaidi kufanikisha usajili wake.
Nyota wa Bayern Munich, Michael Olise. Picha na Mtandao
Staa huyo alijiunga na Bayern Munich, Julai 7, 2024 akitokea Crystal Place kwa dau la paundi 60 milioni (Sh211 bilioni) na mkataba wake utamalizika Juni 30, 2029. Hadi kufikia sasa Olise ameonyesha kiwango cha hali ya juu kwa mabingwa hao wa Ujerumani akiwa amehusika katika mabao 43 akifunga 18 na kutoa pasi za mwisho 25 katika michezo 43 ya mashindano yote aliyocheza.