Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Slot ampa masharti mawili Salah

Muktasari:

  • Kauli hiyo ya Slot imetolewa muda mfupi baada ya Liverpool kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa San Siro dhidi ya Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Milan, Italia. Meneja wa Liverpool, Arne Slot amemtaka nyota wake Mohamed Salah kufanya mambo mawili ikiwa anataka kumaliza tofauti zilizopo baina yao hivi sasa na ili aendelee kuwa sehemu ya mpango wake klabuni hapo.

Kauli hiyo ya Slot imetolewa muda mfupi baada ya Liverpool kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa San Siro dhidi ya Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mchezo huo, Liverpool haikuwa na Salah ambaye Slot aliamua kutosafiri naye kufuatia kitendo cha mshambuliaji huyo kumtuhumu Meneja na klabu hiyo kiujumla baada ya kutopewa nafasi ya kucheza katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Leeds United, Jumapili iliyopita.

Akizungumza baada ya mechi dhidi ya Inter Milan, Slot amemtaka Salah kwanza afahamu kwamba amekosea na jambo la pili ni mchezaji mwenyewe kuomba radhi kwake na klabu kiujumla.

“Mnasema kila mmoja anafanya makosa katika maisha hivyo jambo la kwanza linatakiwa kuwa ni je mchezaji anafikiria kuwa amefanya makosa?

“Na swali la pili ni, juhudi (za kumaliza mgogoro), zinapaswa kutoka kwangu au kwake? Hilo ni swali lingine la kujibu,” amesema Slot.

Nahodha wa Liverpool, Virgil Van Dijk amefichua kuwa klabu hiyo ipo tayari kumaliza suala hilo ikiwa Salah atakubali kuiangukia Liverpool.

“Nitawasiliana naye. Uhalisia pia ni kwamba Mo (Salah) anakwenda Afrika hivi karibuni. Nimemfahamu kwa muda mrefu sana. Sisi ni marafiki wazuri na tumepitia panda shuka. Tunazungumza na mambo aina hiyo yatabaki ndani kama inavyopaswa kuwa. Tunapaswa kujiimarisha na kupambana na  kelele za nje,” alisema Van Dijk.

Baada ya mchezo wa Leeds, Salah alilalama kuwa kwa sasa hapati heshima ndani ya klabu hiyo kwa vile hapewi nafasi ya kutosha ya kucheza na Slot.

"Nilisema mara nyingi hapo awali kwamba nilikuwa na uhusiano mzuri na meneja (Slot) na ghafla hatuna uhusiano wowote.

"Sijui kwanini lakini inaonekana kwangu, jinsi ninavyoiona, kwamba kuna mtu hataki niwe kwenye klabu.

"Inaonekana kama klabu imenitupa nje ya basi. Hivyo ndivyo ninavyohisi. Nadhani ni wazi kwamba kuna mtu alitaka nipate lawama zote,” alinukuliwa Salah.