Slot sasa mambo ni magumu Liverpool
Muktasari:
- Nahodha huyo alidokeza kuwa baadhi ya wachezaji hawana uimara unaohitajika na mabingwa ili kutetea taji lao
Liverpool, England. Siku kadhaa nyuma hakuna ambaye alikuwa anafikiri kuwa kocha wa Liverpool Arne Slot kuna wakati ingeelezwa kuwa anaweza kutimuliwa kwenye kikosi hicho.
Pamoja na kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita kwa sasa kibarua cha kocha huyo kipo shakani na muda wowote anaweza kutimuliwa kwenye timu hiyo.
Chini ya Mholanzi huyo, timu iliyotawala ligi msimu uliopita sasa inazama katika wimbi la vichapo vya aibu.
Slot hawezi kuziba ufa uliopo. Badala yake, vidole vya lawama vinaelekezwa kwake.
Sehemu kubwa ya mashabiki ambao wengi wao juzi waliondoka uwanjani kabla ya filimbi ya mwisho iliyoashiria kichapo cha sita katika mechi saba za Premier League, hawana tena imani.
Beki Virgil van Dijk alitoa lawama kali baada ya Nottingham Forest ya Sean Dyche kuwachapa mabao 3-0 nyumbani.
Na nahodha huyo alidokeza kuwa baadhi ya wachezaji hawana uimara unaohitajika na mabingwa ili kutetea taji lao.
Wale aliowalenga kwa maneno hayo bila shaka walitambua kuwa, ingawa alisisitiza kwamba “sisi” tunapaswa kujitazama kwenye kioo na “sisi” tulipoteza bao kupitia mpira wa adhabu tena hakugusia makosa yake kama nahodha.
Wayne Rooney, aliyependekeza kuwa beki huyo wa kati na Mo Salah hawakuonyesha uongozi unaostahili, bila shaka naye alisikiliza kwa makini.
Wakati huo huo, Slot alikuwa akifanya kile ambacho makocha wengi huamini kuwa ni cha heshima kujilaumu mwenyewe.
Hata hivyo, juhudi zake za kuondoa lawama kutoka kwa timu ambayo ilisalimu amri mara tu Murillo alipoifungia Forest dakika ya 33 zilionekana kuwa zisizo na uzito.
Alikuwa hana mvuto, sawa na ulinzi unaoongozwa na Van Dijk.
Baada ya kutumia pauni milioni 426 majira ya kiangazi, wanachopata ni kidogo mno na lawama zote zinaishia kwa Slot.
Van Dijk yuko sahihi kusema kuwa wengi waliovalia jezi nyekundu sasa hukata tamaa mara tu wanapopitwa lakini ni kocha ambaye anapaswa kuwapa msukumo. Na hilo halitokei kwa sasa.
Wamarekani ambao ni wamiliki wa Liverpool wanaweza kuwa walithamini ukweli aliouongea kocha huyo wa zamani wa Feyenoord na hata kukosoa baadhi ya wachezaji ambao hawastahili tena kulindwa.
Inaelezwa kuwa sasa timu hiyo ambayo inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Premier inaweza kumtimua kocha huyo siku chache zijazo, lakini hofu kubwa ni nani atachukua nafasi yake kwenye timu hiyo yenye mahitaji mengi kwa sasa.